Friday, August 5, 2011

CHELSEA YASAJILI MBRAZIL WA BARCELONA

Chelsea imemsajili mchezaji wa kiungo Oriol Romeu kwa mktaba wa miaka minne kutoka klabu ya Barcelona kwa kitita cha paundi milioni 4.35.

Oriol Romeu
Ada hiyo ya uhamisho iliafikiwa siku 11 zilizopita.
Romeu atawasili Stamford Bridge mara atakapomaliza kuichezea timu ya taifa ya Hispania iliyo katika mashindano ya Kombe la Dunia chini ya umri wa miaka 20 nchini Colombia.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 ameshacheza mechi zote hadi sasa katika mashindano hayo ikiwemo waliyoshinda mabao 4-1 dhidi ya Costa Rica na walipoilaza Ecuador 2-0.
Romeu msimu uliopita alicheza mara mbili katika kikosi cha kwanza cha Barca, akicheza mechi yake ya kwanza kwa timu ya wakubwa mwishoni mwa msimu uliopita, lakini hakuwemo katika kikosi cha muda mrefu cha kocha Pep Guardiola.
Kiungo huyo ambaye alikuwa zaidi akicheza katika kikosi cha pili cha Barcelona, alisema wiki hii: "Chelsea ni chaguo muhimu kwangu.
Kusajiliwa kwa Romeu ni faraja kubwa kwa bosi mpya wa Chelsea Andre Villas-Boas ambaye kwa muda wa miezi sita ijayo atamkosa kiungo muhimu Michael Essien.
Essien aliumia goti wakati wa mazoezi ya kujiandaa na msimu.


MWANASOKA NAOKI WA JAPAN AFARIKI DUNIA

Mwanasoka mashuhuri wa Japan Naoki Matsuda amefariki dunia siku mbili baada ya kupoteza fahamu uwanjani akiwa mazoezini ikidhaniwa ni matatizo ya moyo.

Marehemu Naoki Matsuda

Matsuda aliyekuwa na umri wa miaka 34, aliyeiwakilisha Japan katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2002, siku ya Jumanne alikimbizwa.
Alianguka na kuzimia akifanya mazoezi na klabu yake ya Matsumoto Yamaga, na tangu wakati huo hakuweza kurejewa na fahamu.
Meneja wa zamani wa timu ya taifa ya Japan, Philippe Troussier akitoa rambirambi zake kwa familia ya mchezaji huyo, alisema alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha nchi hiyo kilichoshiriki Kombe la Dunia.
"Inasikitisha sana kuona mtu anafariki dunia akiwa na umri mdogo kama wake," Bw Troussier alieleza Shirika la Reuters.
"Ni pigo kubwa. Alikuwa kijana mzuri sana na nilikuwa karibu naye. Niko pamoja na jamaa zake katika msiba huu mkubwa."
Mashabiki, marafiki na wachezaji wenzake wa zamani, walikusanyika katika hospitali ya Matsumoto kumtakia apone haraka alipokuwa amepoteza fahamu.
Matsuda aliichezea Japan mara 40 na kushinda mataji mara mbili katika Ligi ya nchi hiyo katika kipindi cha miaka 15 cha uchezaji wake na timu ya Yokohama F-Marinos.
Mapema mwaka huu alijiunga na timu ya Matsumoto inayocheza ligi ya chini.