Moussa Dembele
Klabu ya Tottenham Hotspurs imepata idhini ya kuendelea mbele na mchakato wa kumnasa kiungo wa kati wa klabu ya Fulham, Moussa Dembele,
kufuatia vilabu hivyo kuafikiana juu ya malipo ya kumnunua mchezaji huyo.
Mchezaji huyo wa Ubelgiji yuko katika mwaka wake wa mwisho
katika mkataba wa kukipiga Fulham inayochezea uwanja wa Craven Cottage, na
hakushiriki katika mechi ya kombe la Capital One dhidi ya Sheffield Wednesday,
wakati timu yake ilipochapwa.
Meneja wa Fulham, Martin Jol, amesema Dembele, mwenye umri wa miaka 25, yumo
katika vipimo vya afya yake ndani ya klabu ya Tottenham.
Dembele alijiunga na Fulham kutoka klabu ya Uholanzi ya AZ Alkmaar, kwa gharama
ya pauni milioni 5, mwaka 2010.
Hayo yakiendelea, Fulham imekuwa katika hali ya kushauriana na Kieran
Richardson, baada ya kuelewana na Sunderland kuhusu kitita kinachohitajika
kumpata mlinzi huyo.
Meneja wa Sunderland, Martin O'Neill alithibitisha kwamba tayari
wamekubaliana juu ya kiwango cha pesa ambazo Fulham watatoa kumnunua mchezaji
huyo mwenye umri wa miaka 27.