Wednesday, September 7, 2011

LIGI KUU YA VODACOM KUTIMUA VUMBI LEO SIMBAvsVILLA,YANGAvsMTIBWA

Ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara itaendelea tena leo katika michezo kadhaa ambapo MABINGWA watetezi wanaoshikilia mkia katika Ligi Kuu hiyo watoto wa jangwani Yanga watakuwa na kibarua kigumu leo mbele ya Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro, huku Simba wakiwakaribisha Villa Squad kwenye Uwanja wa Mkwakwani katika muendelezo wa ligi hiyo.

Lakini wakati mikikimikiki ya Ligi Kuu ya Bara ikizidi kushika kasi kwenye viwanja mbalimbali nchini, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana limeifanyia mabadiliko ratiba ya ligi hiyo kufuatia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha kutakiwa kutumika kwa shughuli za dini na mashindano ya riadha ya Safari International Marathon.

Kutokana na mabadiliko hayo mechi kati ya JKT Oljoro na Azam imesogezwa mbele na sasa itachezwa keshokutwa Ijumaa mjini Arusha.

Baada ya mapumziko Yanga wanashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu mbaya ndani ya uwanja wa Jamhuri kwa kufungwa na JKT Ruvu na Moro United iliyowapa pointi moja mkiani, huku nje ya uwanja uongozi wa klabu hiyo kongwe upo njia panda baada ya mahakama kutaka uondolewe.

Kocha wa Yanga, Sam Timbe na vijana wake wanajua ushindi wa leo dhidi ya Mtibwa Sugar utarudisha hali ya utulivu ndani ya klabu ya Yanga inayoshikilia mkia wa ligi pamoja na kuwa na kikosi kilichojaa nyota kutoka kona zote za Afrika.

Mganda Timbe anajua mara mbili alinusurika kipigo kutoka kwa mashabiki kwenye uwanja huo hivyo analazimika kupigana kurudisha heshima yake.

"Sina wasiwasi na mchezo huo tumeshafanya marekebisho matatizo madogo madogo yaliyojitokeza katika michezo ya nyuma, lakini hiyo ilitokana na kuwa na majeruhi wengi.

Naye kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime alisema wamejipanga vyema katika mchezo wao wa leo dhidi ya mabingwa hao na wanategemea matokeo mazuri ili waendelee kujitengenezea mazingira mazuri ndani ya msimamo wa ligi hiyo.

Mtibwa ina pointi saba wakiwa nafasi ya pili katika msimamo wa ligi na imepania kuendeleza rekodi ya ushindi katika mchezo wa leo baada ya kuifunga Toto African ya Mwanza mabao 3-2 katika mchezo wao uliopita ikiwa nyumbani.

Jijini Tanga mabingwa wa Ngao ya Jamii, Simba walioanza msimu kwa kishindo kikubwa watakuwa na kazi nyepesi dhidi ya Villa Squad timu yenye rekodi ya utovu wa nidhamu kwa kuwa na kadi 12, moja nyekundu na njano 11 katika msimu huu.

Mshambuliaji Mohamed Kijuso wa Villa atakuwa na kazi ya kumthibishia kocha Moses Basena wa Simba kwamba alifanya kosa kumtoa kwa mkopo msimu huu.

Kijuso mwenye mabao mawili hadi sasa akisaidiana na Nsa Job watakuwa na kazi nzito mbele ya ukuta imara wa Simba chini Victor Costa na Juma Nyoso pamoja na kipa Juma Kaseja mwenye nia ya kuendeleza rekodi yao ya kutoruhusu bao.

Safu ya ushambuliaji wa Simba itamkosa Felix Sunzu,mzambia huyo anayetumikia adhabu ya kutocheza mechi tatu na Salum Machaku majeruhi, huku Emmanuel Okwi akiitumikia timu yake ya taifa Uganda kwenye Michezo ya Afrika nchini Msumbiji.

Kocha Basena atalazimika kubadili mfumo wa ushambuliaji leo kwa kuwatumia  Ulimboka Mwakingwe, Gervais Kago wakiunganishwa na Haruna Moshi"Boban".

 TFF imefanya mabadiliko ya ratiba ya ligi hiyo kwa mara nyingine kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Hahari wa shirikisho hilo Boniface Wambura.

Mabadiliko ya ratiba yanahusisha mechi zifuatazo na tarehe mpya zikiwa katika mabano; Septemba 7 mwaka huu mechi namba 20- Oljoro JKT vs Azam (Septemba 9), Septemba 10 mwaka huu mechi namba 22- Azam vs Simba (Septemba 11), Septemba 11 mwaka huu mechi namba 26- Ruvu Shooting vs Yanga (Septemba 10).

Septemba 17 mwaka huu mechi namba 38- Oljoro JKT vs African Lyon (Septemba 19), Septemba 21 mwaka huu mechi namba 43- Kagera Sugar vs Oljoro JKT (Septemba 22), Septemba 21 mwaka huu mechi namba 49- Ruvu Shooting vs African Lyon (Septemba 20) na Septemba 24 mwaka huu mechi namba 54- Toto Africans vs Oljoro JKT (Septemba 25).


Vermaelen aumia tena Arsenal kumkosa kwa wiki 4

Mlinzi wa kati wa Arsenal Thomas Vermaelen hatacheza soka kwa muda unaokisiwa mwezi mmoja baada ya kufanyiwa upasuaji mdogo wa kifundo cha mguu wake wa kushoto.
Thomas Vermaelen
Thomas Vermaelen

Mlinzi huyo mwenye umri wa miaka 25 aliumia wakati wa mechi ya marudiano ya kufuzu kwa Ubingwa wa Ulaya dhidi ya Udinese.
Ni pigo jingine kwa Gunners, ambayo imeuanza msimu kwa kuchechemea na hivi karibuni mchezaji mwengine Jack Wilshere ameumia na hatacheza soka kwa miezi mitatu kutokana na matatizo ya kifundo cha mguu.
Vermaelen msimu mzima uliopita hakucheza kutokana na kuumia kifundo cha mguu mwengine, ambao pia ulifanyiwa upasuaji.
"Haya ni matibabu yanayofanana na aliyopata katika kifundo cha mguu wa kuume mwezi wa Januari mwaka huu na hayahusiani na kuumia kwake kwa msimu uliopita," taarifa ya Arsenal ilifahamisha zaidi.
"Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya mashauriano na daktari bingwa aliyeshauri afanyiwe upasuaji kuzuia tatizo lisiwe la kudumu."
Vermaelen aliumia wakati Arsenal ilipoishinda udinese mabao 2-1 tarehe 24 mwezi wa Agosti na klabu hiyo ilikuwa na matumaini asingehitajika kufanyiwa upasuaji.
Lakini alipasuliwa mjini Stockholm siku ya Jumatatu na sasa atakosa mechi dhidi ya Swansea, Borussia Dortmund, Blackburn, Shrewsbury, Bolton, Olympiakos na Tottenham.
Mlinzi huyo wa zamani wa Ajax hakucheza tarehe 28 mwezi wa Agosti siku Arsenal ilipoadhiriwa na Manchester United kwa kutandikwa mabao 8-2, lakini licha ya kukosa mechi hiyo msimu huu amecheza karibu mechi zote za Arsenal.
Per Mertesacker, aliyejisajili na Arsenal muda mfupi kabla ya kufungwa dirisha la usajili, huenda akaitwa haraka kuziba pengo la Vermaelen, wakati walinzi wengine wa kati Laurent Koscielny, Johan Djourou na Sebastien Squillaci huenda mmoja wao akawa matumaini ya Arsene Wenger kwenye safu ya ulinzi.
Arsenal msimu huu imeshafungwa mabao 11 na hadi sasa inashikilia nafasi ya 17 ya msimamo wa Ligi Kuu ya England ikiwa na pointi moja tu baada ya mechi tatu.