Monday, January 16, 2012

Swansea yaiadhiri Arsenal,Man U mbele kwa mbele

Robin Van Persie aliifungia Arsenal bao la kwanza
Van Persie mfungaji wa bao la kwanza la Arsenal

Matumaini ya Arsenal kusogelea nafasi nne bora za juu za Ligi ya kandanda ya England yalivurugwa na Swansea waliosakata kandanda murua na kuweza kupata pointi tatu muhimu kwa kuilaza Arsenal mabao 3-2 katika mchezo uliokuwa wa kusisimua.
Arsenal walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya nne kwa bao la Robin van Persie, lakini wageni hao walionekana kuzidiwa katika kila idara na vijana wa Swansea.
Swansea ilipoiadhiri Arsenal
Scott Sinclair aliisawazishia Swansea kwa mkwaju wa penalti baada ya Aaron Ramsey kumkwatua Nathan Dyer ndani ya eneo la hatari.
Nathan Dyrea aliipatia Swanse bao la pili katika kipindi cha pili kwa makosa ya walinzi wa kati wa Arsenal
Theo Walcott aliisawazishia Arsenal kwa bao la pili na dakika moja baadae Danny Graham akaipatia Swansea bao la tatu la ushindi."Ni wazi kuwa Swansea walistahili ushindi kwani walicheza kwa kujituma na kwa kasi ileile mwanzo mwisho tofauti na Arsenal walioonekana kuwa wachovu"
Na bao maridadi lililofungwa na Leon Best katika kipindi cha kwanza liliinua Newcastle hadi nafasi ya sita ya msimamo wa Ligi Kuu ya England na kumvurugia meneja mpya wa QPR Mark Hughes mechi yake ya kwanza.
QPR mara mbili mikwaju yao iligonga mwamba katika kipindi cha kwanza kwa michomo ya Shaun Wright-Phillips na Jay Bothroyd.
Lakini Newcastle walizinduka kutoka usingizini mwanzoni mwa kipindi cha kwanza na Best alifunga bao maridadi baada ya kuwazunguka walinzi wa QPR.
Bothroyd alipoteza nafasi mbili nzuri kuipatia QPR mabao katika kipindi cha pili lakini walinzi wa Newcastle walionekana kukaa imara.

MAN UNITED YAILAZA BOLTON
Paul Scholes amefunga bao lake la kwanza baada ya kurejea tena kuichezea Manchester United ambayo imesogea na kuwa na pointi sawa na Manchester City baada ya kuilaza Bolton mabao 3-0.
Mkongwe Paul Scholes aifungia Man United bao la kwanza
Paul Scholes

United ilipoteza nafasi nyingi za kufunga kipindi cha kwanza lakini kazi nzuri aliyoifanya mlinda mlango wa Bolton Adam Bogdan iliisaidia Bolton kuepuka kipigo kikali zaidi. Alifanikiwa kuokoa mkwaju wa penalti uliopigwa na Wayne Rooney katika kipindi cha kwanza.
Lakini Scholes, ambaye sasa amefika umri wa miaka 37, alifanikiwa kupachika bao sekunde chache kabla mapumziko baada ya kuunganisha pasi ya pembeni ya Rooney.
Matukio na magoli kati ya Man na BOLTON

Bolton ilionekana kuimarika kipindi cha pili na Manchester United walionekana kusinzia kidogo, lakini alikuwa Danny Welbeck aliyeizindua tena Man United kwa kupachika bao la pili kabla ya Michael Carrick kufumua mkwaju wa umbali wa yadi 20 na kuandika bao la tatu.
Matokeo hayo yameonekana kuipa faraja Man United baada ya kupoteza michezo miwili ya Ligi Kuu ya England, pia kuzidi kuipa changamoto mahasimu wao Man City ambao siku ya Jumatatu watasafiri hadi Wigan kuikabili timu hiyo.
Bao pekee alilofunga Frank Lampard mapema katika kipindi cha kwanza, limeiwezesha Chelsea kuipunguzia kasi Sunderland iliyoanza kucharuka baada ya kumpata meneja mpya Martin O'Neill.
Lampard alitumia uamuzi wa haraka kuuwahi mpira na kupachika bao kwa mkwaju wa karibu baada ya fataki aliyoachia Fernando Torres kugonga mwamba na kurejea uwanjani.
Torres, Lampard na Juan Mata wote walikosa nafasi nzuri za kufunga kipindi cha kwanza.
Lakini Sunderland walipata nafasi nyingi kipindi cha kwanza na walikosa nafasi muhimu ya kupachika bao dakika za mwisho ambapo Craig Gardner na Nicklas Bendtner walishindwa kufunga.
Blackburn waliweza kuhimili vishindo licha ya mfungaji wao mashuhuri Yakubu kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika za mwanzo na kutoka eneo la hatari la kushuka daraja kwa mara ya kwanza tangu mwezi wa Septemba kwa ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Fulham.
Mshambuliaji Yakubu alioneshwa kadi nyekundu kipindi cha kwanza baada ya kumfanyia rafu mbaya Danny Murphy.
Lakini wakicheza nyumbani Blacburn walifanikiwa kupata bao la kwanza lililofungwa na Morten Gamst Pedersen kwa mkwaju wa adhabu ya moja kwa moja kabla ya David Dunn kupachika bao la pili.
Damien Duff aliipatia Fulham bao la kufutia machozi, kabla ya Mauro Formica kuikamilishia kazi Blackburn kwa kuandika bao maridadi la tatu.
Victor Anichebe akiingia mchezaji wa akiba alifanikiwa kuipatia Everton pointi moja baada ya Aston Villa kuonesha kandanda ya ovyo wakicheza uwanja wa nyumbani.
Darren Bent aliipatia Aston Villa bao la kwanza baada ya kupokea pasi ya Stephen Ireland katika dakika ya 56.
Meneja wa Everton David Moyes aliona hakuna cha kuikomboa timu hiyo bila ya kumuingiza Anichebe ambaye alifanikiwa kuisawazishia Everton baada ya Landon Donovan kumchezesha kwa pasi murua.
Robbie Keane aliingia kipindi cha pili kwa Villa ikiwa ni mchezo wake wa kwanza tangu ajiunge na timu hiyo kwa mkataba wa muda mfupi, lakini hakuweza kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi.
Bao la kichwa la dakika za mwisho lililofungwa na Steve Morison liliisaidia Norwich kushinda kwa kuilaza West Brom mabao 2-1.
Mkwaju wa juu wa Andrew Surman uliiwezesha Norwich kuandika bao la kwanza muda mfupi kabla ya mapumziko wakati West Brom wakionekana kukosa nafasi nyingi za wazi kupachika mabao.
Shane Long alizinduka haraka na kuipatia bao West Brom kwa kwaju wa penalti baada ya Jerome Thomas kuchezewa rafu.
Lakini Morison aliangushia kipigo cha nne mfululizo West Brom kwa kuandika bao la pili.
Liverpool imekosa nafasi ya kuingia katika timu tano bora za juu baada ya kubanwa na Stoke na kuandika sare ya saba kwa michezo iliyocheza uwanja wa nyumbani wa Anfield.
Dirk Kuyt alipoteza nafasi nzuri ya kuipatia bao Liverpool wakati mpira wake wa kichwa ulipotoka nje.
Martin Skrtel alidonyoa mpira wa kichwa dakika za mwisho lakini Liverpool walikuwa wamejipanga zaidi kwa kuachia mikwaju ya mbali ambayo haikuzaa matunda.
Mkwaju alioupiga Matthew Etherington kwa kumlenga mlinda mlango wa Liverpool Jose Reina ulikuwa ni moja ya majaribio machache ambayo Stoke iliyafanya. Hadi mwisho timu hizo hazikufungana.
Tottenham nayo ilikosa nafasi nyeupe ya kufikisha pointi sawa na vinara wa ligi baada ya kubanwa na kutoka sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Wolves.
Steven Fletcher alikuwa wa kwanza kuipatia Wolves bao kwa mkwaju wa karibu baada ya mlinda mlango Brad Friedel kupangua mpira wa kichwa uliopigwa na Roger Johnson.
Luka Modric aliisawazishia Spurs kwa mkwaju wa yadi 20 baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Gareth Bale ambaye alikosa kuuweka mpira wavuni na ukamkuta mfungaji ambaye hakufanya ajizi.
Wolves walijihami vizuri huku mlinda mlango Wayne Hennessey akiokoa michomo ya Aaron Lennon na Jermain Defoe.
Matumaini makubwa ya Tottenham yaliyoanza kuchomoza hivi karibuni ya kushinda ligi baada ya miaka 50 yalivurugika ambapo kama wangeshinda wangekuwa pointi sawa na Manchester zote mbili huko kileleni wakitenganishwa na wingi wa mabao.