Leo, Serikali itawasilisha bungeni muswada wa Sheria ya Makosa ya
Mtandao wa mwaka 2015 kwa hati ya dharura unaoorodhesha adhabu
mbalimbali, ikiwamo ya faini ya Sh50 milioni au kifungo kisichopungua
miaka saba kwa mtu atakayebainika kusambaza picha za ngono mtandaoni.
Baadhi ya makosa yaliyoanishwa katika sheria hiyo ni kutuma
taarifa bila ridhaa ya mtu, kusambaza picha za ngono na za utupu,
udanganyifu unaohusiana na kompyuta, makosa yanayohusiana na utambuzi,
kughushi kunakohusiana na masuala ya kompyuta na kusambaza picha za
utupu za watoto.
Mengine ni unyanyasaji kwa kutumia mtandao,
kuchapisha taarifa yoyote ambayo itasababisha mauaji ya kimbari, uongo
na matusi ya kibaguzi.
Sheria hiyo katika Kifungu cha 48 inaipa Mahakama
mamlaka ya kutaifisha mali iliyopatikana kutokana na kosa lililofanywa
na mhusika. Sheria hiyo pia itawataka wote watakaobainika kufanya makosa
hayo kuwasilisha hati zao za kusafiria kwa mamlaka husika hadi hapo
watakapolipa faini au watakapokuwa wamemaliza kutumikia vifungo.
Muswada huo ambao ukipitishwa utakuwa sheria, unawasilishwa
bungeni katika kipindi ambacho kina matukio mengi ya watu kusambaza
picha za ngono na utupu mitandaoni, kuingilia mawasiliano ya kompyuta ya
watu wengine bila ridhaa yao.
Pia, kifungu hicho kinaeleza kuwa mtu
atakayebainika kusambaza picha za ngono, uasherati na matusi, atatozwa
faini isiyopungua Sh30 milioni au kwenda jela miaka 10, mtu
atakayesambaza picha za utupu atalipa faini isiyopungua Sh20 milioni au
kwenda jela miaka saba.
Inawabana pia watoa taarifa za uongo. Katika
Kifungu cha 16, inasema mtu atakayetoa taarifa, takwimu au maelezo kwa
njia ya picha au maandishi au aina nyingine yoyote zikiwa ni za uongo,
akipatikana na hatia atalipa faini isiyopungua Sh3 milioni au kifungo
kisichopungua miezi sita.
Kuhusu mauaji ya kimbari, inakataza mtu kuchapisha
au kusababisha kuchapisha vitu vinavyochochea au kuhalalisha matendo
yanayosababisha mauaji ya kimbari na adhabu yake ni faini ya Sh10
milioni au miaka mitatu jela .