Thursday, February 9, 2012
Kocha Fabio Capello abwaga manyanga England, kisa...Terry
Fabio Capello
Fabio Capello amejiuzulu kama meneja wa timu ya taifa ya soka ya England, chama cha FA kimethibitisha habari hizo.
Capello amejiuzulu baada ya kukutana na mwenyekiti wa chama cha FA cha England, David Bernstein, na katibu mkuu Alex Horne, katika afisi za uwanja wa Wembley.John Terry
Taarifa ya FA ilielezea: "Chama cha soka cha FA kinathibitisha kwamba Fabio Capello leo amejiuzulu kama meneja wa timu ya England."
Siku ya Jumatatu, Capello, ambaye ni raia wa Italia, katika magazeti ya Italia alielezea kutopendezwa na hatua ya chama cha FA kumvua John Terry unahodha wa timu ya taifa ya England.
Taarifa ya FA iliendelea kueleza; "Katika mkutano ulioendelea kwa zaidi ya saa nzima, hatua ya Fabio kujiuzulu ilikubaliwa, na ataacha madaraka hayo mara moja".
Bernstein alielezea: "Ningelipenda kusisitiza kwamba wakati wa mkutano, na katika wakati wote ambao Fabio amekuwa meneja wa timu ya taifa, tabia yake imekuwa ni ya mtu aliyesimamia kazi yake kwa heshima".
Mkutano wa Bernstein akiwa na maafisa wakuu wa timu ya England, kukutana na waandishi wa habari, unatazamiwa kufanyika Alhamisi, saa sita mchana za Uingereza, katika uwanja wa Wembley.
Chama cha FA kimeelezea hakitatoa maelezo zaidi hadi baada ya mkutano huo.
John Terry, mchezaji wa Chelsea, na mwenye umri wa miaka 31, inadaiwa alitumia matamshi ya ubaguzi wa rangi dhidi ya mchezaji wa QPR, Antonio Ferdinand.
Terry anakanusha madai hayo, na kesi yake itasikilizwa mwezi Julai.
Siku ya Jumapili, Capello akizungumza katika kituo cha matangazo cha RAI nchini Italia, alisema haamini uongozi wa michezo unafaa kumuadhibu mtu, huku akisubiri uamuzi kutolewa na mahakama.
Ivory Coast yaichapa Mali yaifuata Zambia fainali kombe la mataifa ya Afrika
Ivory Coast itakutana na Zambia kwenye fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya timu hizo mbili kushinda mechi zao za nusu fainali.
Ivory Coast imefuzu baada ya kuishinda Mali 1-0 katika nusu fainali yao mjini Libreville, nchini Gabon.Ivory coast 1-0 Mali
Awali katika mji wa Bata nchini Gabon Zambia iliibandua Ghana kutoka mashindano hayo kwa kuifunga 1-0.
Bao la Zambia lilifungwa katika dakika ya 78 na mshambuliaji Emmanuel Mayuka.
Katika kipindi cha kwanza mshambuliaji wa Ghana Asamoah Gyan alikosa kufunga penalti, mlinda mlango wa Zambia akautema nje mpira.
Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika itachezwa siku ya Jumapili mjini Libreville, nchini Gabon, mechi ambayo itatangazwa moja kwa moja kupitia Idhaa ya Kiswahili ya BBC.
Ghana yafungashwa virago na Zambia katika nusu fainali kombe la mataifa ya Afrika
Wachezaji wa Zambia wakishangilia goli la Mayuka
Zambia imeifunga Ghana 1-0 na kufuzu fainali ya Kombe la mataifa ya Afrika kwenye mechi ya nusu fainali mjini Bata, Equatorial Guinea.
Mshambuliaji Emmanuel Mayuka ambaye aliingia kipindi cha pili ndiye aliyeifungia Zambia bao la ushindi katika dakika ya 78.Zambia 1-0 Ghana
Ghana walimaliza wachezaji 10 baada ya Derek Boateng kupewa kadi nyekundu kuelekea mwisho wa mechi.
Mayuka ni mchezaji pekee katika timu ya Zambia anayecheza soka ya kulipwa ulaya.
Zambia haijapata kushinda Kombe la mataifa ya Afrika, lakini mara mbili wamefika fainali, na sasa wamefuzu fainali mara ya kwanza tangu mwaka 1994.
Subscribe to:
Posts (Atom)