Timu ya mpira wa miguu ya Tanzania (TAIFA Stars) imeshindwa kutumia uwanja wake wa nyumbani kwa kukubali kulazimishwa suluhu na DR Congo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa ulitoa nafasi kwa makocha wa timu zote kuangalia ubora wa vikosi vyao kabla ya kucheza mechi zao za kuwania kufuzu kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika 2013.
Taifa Stars itawakaribisha Msumbiji kwenye uwanja huo Jumatano ijayo katika kampeni yake ya kusaka tiketi ya kwenda Afrika Kusini.
Stars ilianza mchezo huo kwa taratibu na kuwaruhusu DR Congo kufanikiwa kufika langoni kwa Taifa Stars mara mbili ndani ya dakika 5, kupitia kona ya Mutombo na mpira wa adhabu wa Kasusula Kilisho uliogonga mwamba na kutoka baada ya Tresor Mputu kufanyiwa faulo na Stephano Mwasika.
Katika mechi hiyo nahodha Shadrack Nsajigwa nusura amchape makofi mshambuliaji Hussein Javu baada ya kupiga shuti hafifu akiwa yeye na kipa Bolongo kwenye mchezo huo ulioshudiwa na mashabiki wachache wa Tanzania, pia kulikuwa na kikundi cha mashabiki kutoka DR Congo.
Stars walijitahidi kutawala mchezo huo, lakini Congo inayoundwa na nyota wengi wa TP Mazembe walionekana kumiliki vizuri zaidi sehemu ya kiungo, ila washambuliaji wake walikosa umakini kwenye umaliziaji.
Katika dakika ya 22 kipa Juma Kaseja alifanya kazi kubwa ya kumzuia Deo Kanda asifunge baada ya mshambuliaji huyo kuwatoka mabeki wa Stars na kupiga shuti la pembeni vilevile dakika ya 24 Mwasika aliushika mpira katika harakati za kuokoa na mwamuzi Israel Mujuni aliamuru faulo iliyopigwa na Kasusula na kutoka nje.
Ngome ya Stars ikiwa chini ya Agrey Morris, Juma Nyoso, Nsajigwa na Mwasika katika kipindi cha kwanza ilikuwa imara na kucheza vizuri ili kuhakikisha wanawazuia vilivyo washambuliaji wa Wakongo.
Mshambuliaji Mrisho Ngasa alifanya juhudi binafsi katika dakika ya 32, ambapo alipiga shuti la mbali la mita 35, lakini shuti hilo lilipaa juu kidogo ya goli la DR Congo.
Pia John Boko alijitahidi kufunga baada ya kutuliza mpira vizuri na kupiga shuti kali akiwa nje ya 18 katika dakika ya 45, ambapo shuti lake lilipaa sentimita chache kwenye lango la Congo.
Mwanzoni mwa kipindi cha pili kocha wa DR Congo, Claude Le Roy alimpumzisha kipa Bolongo na kumwingiza Kidiaba Muteba wakati Jan Poulsen aliwatoa Ngasa, Kaseja, Javu na Nsajigwa na kuwaingiza Mwadini Mwadini, Said Nasoro, Uhuru Selemani na Nsa Job.
Dakika ya 56, kipa Mwadini alithibisha ubora wake kwa kuokoa kwa ufundi mkubwa mpira wa kichwa uliopigwa na Kayiba, ambapo Stars ilijibu mapigo dakika moja baadaye baada ya Boko kujirusha vizuri kujaribu kufunga kwa kichwa krosi iliyopigwa na Abdi Kassim.
Kocha Poulsen alifanya mabadiliko mengine katika dakika ya 58 kwa kuwatoa Mwinyi Kazimoto, Kassim na kuwaingiza Jonas Mkude na Abubakar Salum 'Sure Boy' nao Congo waliwatoa Mputu na kumwingiza Amomo Ngoy.
Pamoja na makocha wote kufanya mabadiliko hayakuweza kuwasaidia kwani hadi filimbi ya mwisho inapulizwa na mwamuzi Mujuni matokeo yakulikuwa suluhu.