Rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud
Bunge la Somalia limemchagua Hassan Sheikh Mohamud kuwa Rais
mpya wa nchi hiyo.
Hassan ameshinda kinyang'anyiro hicho kutoka wagombea 22 walioshiriki uchaguzi huo, akiwemo Rais anayeondoka Shariff
Sheikh Ahmed na waziri mkuu Abdiweli Mohamed Ali.
Hassan Sheikh Mohamud alishinda kufuatia duru ya tatu ya upigaji kura, ambapo
alikuwa anachuana na Rais anayeondoka Shariff Sheikh Ahmed.
Katika raundi ya kwanza Sheikh Ahmed alikuwa amepata ushindi mwembamba wa
kura 64 dhidi ya 60 alizopata Sheikh Mohamud.
Kwa jumla wabunge 271 walipiga kura.
Katika duru ya mwisho wabunge wengi waliowaunga mkono wagombea waliochujwa
walimuunga mkono Sheikh Mohamud , akapata kura 190 dhidi ya 70 alizopata Rais
anayeondoka.
Hii ni mara ya kwanza kwa uchaguzi wa Rais kufanyika katika mji mkuu wa
Somalia Mogadishu, tangu kuondolewa kwa serikali ya kijeshi mwaka 1991.