Tuesday, September 11, 2012
SIMBA USO KWA MACHO NA AZAM TAIFA LEO HII
Leo ndio leo wakati Mrisho Ngassa wa Simba anatarajia kuwa kiini cha utamu wa mchezo wa soka, pale atakaipoikabili kwa mara ya kwanza timu yake ya zamani, Azam FC katika mechi ya Ngao ya Jamii, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mrisho Ngassa
Simba, mabingwa wa soka Bara walimsajili Ngassa kutoka kwa washindi hao wa pili wa Ligi Kuu Azam. Kabla ya kutua Simba, Ngassa alikuwa akiwaniwa na Yanga ya Dar es Salaam.
Mbali na Ngassa, mwingine ambaye leo huenda akawa kivutio, ni Ramadhan Chombo 'Redondo' atakayekuwa na timu yake mpya Simba.
Redondo ambaye usajili wake ulizua utata, alisajiliwa na Simba kutoka Azam FC, ambao nao awali walimsajili kutoka kwa Wekundu hao wa Msimbazi.
Pambano la timu hizo ni ishara ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu mwishoni mwa wiki hii, kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Ramadhan Chombo "Redondo"
REKODIKwa mwaka huu pekee, Simba na Azam zimekutana mara tano katika mechi za mashindano mbalimbali. Hazijawahi kutoka sare, huku Simba ikishinda michezo mitatu na Azam miwili.
Mechi ya karibuni ni ile ya nusu fainali ya michuano ya Super8, ambapo Simba iliyochezesha kikosi 'B' dhidi ya kikosi kamili cha Azam, ilishinda mabao 2-1.
"Majembe"
Kwa kiasi kikubwa Simba itakuwa na mwonekano tofauti kwa vile ina sura kadhaa mpya kutoka ndani na nje ya nchi.
Miongoni mwa nyota wapya mbali na Redondo na Ngassa kwenye jeshi la Simba leo, wengine ni mshambuliaji wake mpya kutoka Ghana, Daniel Akufo na beki raia wa Mali Komanbill Keita na Mkenya, Pascal Ochieng.
Nayo Azam kama ilivyo kwa wenzao wa Simba, inatarajiwa kuwa na mabadiliko kidogo hasa hasa katika mpangilio wa kikosi na hii ikitokana na kutokuwapo kwa Ngassa na Redondo.
Mfumo:
Wakati Simba itakuwa na kocha mwenye uzoefu na timu hiyo Milovan Cirkovic, Azam itaongozwa na kocha wake mpya Boris Bunjak aliyeukwaa ubosi, baada ya kutimuliwa Mwingereza Stewart Hall.
Timu zote zinatumia mfumo mmoja wa 4-4-2 na hata aina ya soka lao pia linafanana, likipingwa pasi nyingi fupifupi.
Wakizungumzia pambano baina yao, makocha wa timu hizo wakiwa katika hali ya kujiamini walijinasibu kila moja kufanya kweli na kuibuka na ushindi.
"Itakuwa mechi ngumu, lakini ni wakati wa sisi kulipa kisasi baada ya wao kutufunga Kombe la Kagame. Tupo vizuri kiakili na kisaikolojia," alisema Cirkovic.
Naye Bunjak alisema, "Ili ushinde unahitaji maandalizi, na kwa upande wetu tumejiandaa kikamilifu kuhakikisha tunashinda mechi hiyo na kutuongezea morali katika ligi."
Kwa upande mwingine, wachezaji wa kuchungwa zaidi leo ni pamoja na mshambuliaji nyota wa Simba Mganda Emmanue Okwi, kama itakavyokuwa kwa mpachika mabao hatari wa Azam John Boko 'Adebayor'.
Rekodi kamili Simba/ Azam mwaka 2012.
Mapinduzi Cup: Azam 2-0 Simba
Ligi Kuu: Simba 2-0 Azam
Urafiki Cup: Simba 3 -1 Azam (pen)
Kagame Cup: Azam 3- 1 Simba
Super 8: Simba 2- 1 Azam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment