Beki wa Moro United Eric Mawala akiwa makini kuzuia mashambulizi ya Okwi
Simba sports Club, imeendelea kutakata kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya jana kuigaragaza Moro United mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, huku mchezo mwingine wa ligi hiyo kati ya Azam na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi kuvunjika dakika 88 matokeo yakiwa sare ya 1-1.
Wawakilishi hao wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, sasa wamefikisha pointi 59 akiwa na mechi moja mkononi dhidi ya Yanga wenye ndoto ya kupata nafasi ya pili kama watashinda kesho dhidi ya JKT Olojro na kuomba Azam ipoteze michezo yake iliyosalia.
Vinara hao iliwachukua dakika 10 kupata bao kwanza lililotiwa kambani kwa mkwaju wa penalti na Mafisango, Haruna Moshi kutupia bao la pili dakika 33 na Felix Sunzu alipigilia msumari wa mwisho dakika ya 74.
Ushindi huo unaiweka Simba kwenye mazingira mazuri kabla ya mechi yake ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Al Alhy Shendi.
Chamazi, Mwamuzi Rashid Msangi alilazimika kumaliza mchezo dakika ya 88, baada ya wachezaji Mtibwa Sugar kugomea penalti katika mchezo ulioshuhudia ubabe mwingi.
Dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho mwamuzi Msangi alilazimika kumaliza pambano baada ya wachezaji wa Mtibwa Sugar kutoka uwanjani wakigomea penalti.
Beki wa Mtibwa Juma Abuu aliunawa mpira kwenye eneo la hatari wakati akijaribu kuokoa na mwamuzi kuamua adhabu hiyo, ndipo wachezaji wa Mtibwa walipomzonga kupiga uamuzi huo.
Wenyeji Azam walipata bao la mapema bao la dakika ya kwanza kupitia kwa mshambuliaji Mrisho Ngasa baada ya kuingia ndani ya 18 na kumlamba chenga kipa wa Mtibwa Sugar, Deogratius Mushi 'Dida'.
Vijana wa Manungu walisawazisha bao hilo dakika 18, kwa mpira wa adhabu uliopigwa na beki mkongwe Salum Swed na kwenda moja kwa moja wavuni.
Katika kipindi cha kwanza Mtibwa Sugar walionekana kucheza kibabe na kutembeza viatu kwa wachezaji wa Azam na kusababisha mwamuzi Msangi kutoa kadi za njano kwa Swed, Hassan Ramadhan na Hussen Javu waliomchezea vibaya John Boko na Ngasa dakika 27,30 na 35, huku Said Bahamuzi akipewa kadi ya njano kwa kupiga mpira nje wakati filimbi imeshapigwa.
Mwamuzi Msangi alitoa kadi ya pili ya njano na nyekundu kwa Bahamuzi aliyemchezea vibaya Salum Abubakari.
Awadhi Issa alifungia Mtibwa Sugar bao dakika 63, lakini mwamuzi alikataa kwa madai alishapulizi filimbi ya kuotea kabla ya mfungaji kupiga mpira huo.
Kwenye Uwanja wa Taifa, Furaha ya mashabiki wa Simba ilifutika ghafla baada ya kusikia mchezo kati ya Azam na Mtibwa Sugar umevunjika.
Simba ilifanya kile kilichosubiriwa na wengie kwa kuichakaza Moro United kwa kupata bao la kwanza dakika 10 kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Mafisango baada ya beki wa Moro United, Omary Gae kunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
Vinara hao walitawala zaidi sehemu ya kiungo na kufanya mashambulizi mengi langoni kwa Moro United iliyoingia uwanjani ikiwa na wachezaji wanne wanaolipwa mshahara na Simba waliowachukua kwa mkopo ni beki Meshack Abel, Salum Kanoni, Godfrey Wambura na Kelvin Charles.
Kiungo Haruna Moshi alifunga bao la pili kwa Simba katika dakika ya 33 akiunganisha vizuri krosi ya Uhuru Seleman.
Mshambuliaji Emmanuel Okwi alipoteza nafasi nzuri ya kuifungia Simba bao la tatu kwa kushindwa kumalizia kwa umakini krosi ya Uhuru katika dakika ya 36.
Moro walijibu mapigo dakika moja kabla ya mapumziko kwa shuti la beki Erick Mawala kugonga mwamba wa juu, lakini kipa Juma Kaseja alikuwa makini na kuwahi kudaka.
Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic aliwapumisha Shomari Kapombe, Gervais Kago na kuwaingiza Nasoro Masoud na Felix Sunzu, wakati Moro Utd alitoka Benedict Ngasa na kuingia Simon Msava.
Mabadiliko hayo yalikuwa na faida kwa Moro waliorudi mchezoni na kufanya mashambulizi mengi, lakini wakajisahau na kutoa nafasi kwa Sunzu kufunga bao la tatu dakika 74 akiunganisha krosi ya Okwi.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana aliipongeza Simba kwa kufanikiwa kuingia raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Akiongea bungeni, Pinda alisema hatua waliyofika Simba kwenye michuano hiyo wanahitaji pongezi na ameomba wapenda michezo kuisapoti.