Kocha mpya wa Brazil, Dunga
Shirikisho la soka la Brazil CBF limemtangaza
aliyekuwa mchezaji wa Brazil Dunga kuwa kocha wa timu ya taifa kwa
mara ya pili.
Dunga aliyeiongoza Brazil kutwaa kombe la dunia la mwaka wa 1994 aliwahi pia kuwa kocha katika mwaka wa 2006 hadi 2011.
Dunga amechukua pahala pake Luiz Felipe Scolari, ambaye alijiuzulu
kufuatia kimbunga cha mabao 7-1 ambayo timu hiyo ililazwa na Ujerumani
katika hatua ya nusu fainali .
Sadfa ni kuwa Kocha huyo mwenye umri wa miaka 50 naye alifutwa kazi
baada ya selecao kubanduliwa nje ya kombe la dunia la mwaka wa 2010
katika hatua ya robo fainali.
Carlos Alberto Parreira ndiye aliyechukua pahala pake lakini hata naye haku dumu Scolari alipotajwa kuwa Kocha.
Scolari mwenye umri wa miaka 65 aliiongoza
Brazil katika semi fainali za kombe la dunia ambapo timu hiyo ilipata
kichapo kibaya cha mabao masaba kwa moja dhidi ya mabingwa wa kombe la
Dunia Ujerumani.
Dunga amewapiku mkufunzi wa kilabu ya Corinthians Tite,Mkufunzi wa
kilabu ya Sau Paulo Muriciy Ramalho na Vanderlei Luxembourg ambaye
aliwahi kuifunza timu hiyo kutoka mwaka 1998 hadi mwaka 2000.
Wakati huohuo kocha wa Argentina Alejandro
Sabella, 59, amesema kuwa atatangaza hatima yake juma lijalo baada ya
kushindwa bao moja kwa nunge na Ujerumani katika fainali ya kombe la
dunia huko Brazil mapema mwezi huu .
Wachezaji wanamtaka kocha Sabella kuiongoza timu
hiyo katika kipute cha kuwania ubingwa wa mataifa ya Amerika ya Kusini
yaani 2015 Copa America mashindano yatakayoandaliwa huko Chile.