Tuesday, July 3, 2012
ANDRE INIESTA MCHEZAJI BORA EURO 2012 TORRES MFUNGAJI BORA
Andre Iniesta Mchezaji bora EURO 2012
Kiungo wa Uhispania, Andres Iniesta amenyakua tuzo ya uchezaji bora wa Euro 2012, huku mwenzake Fernando Torres akinyakua tuzo ya ufungaji bora iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Ulaya ( UEFA).
Kiungo huyo wa Hispania mwenye miaka 28, aliyechangia ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Italia usiku wa Jumapili iliyopita, alitajwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo ya fainali na Kamati ya Ufundi iliyoundwa na watu 11.
Nyota huyo wa Barcelona alishindwa kufunga bao na kutegeneza moja katika fainali hiyo, lakini amepata tuzo hiyo kutokana na mchango wake wa jumla ulivyowawezesha Hispania kutetea taji lao.
Iniesta alitegeneza bao muhimu lililofungwa na Jesus Navas likiwa ni bao pekee dhidi ya Croatia kwenye mchezo wa mwisho wa makundi, huku pasi yake nyingine kwa Cesc Fabregas katika mchezo wa fainali ikimsaidia Fabregas kupiga krosi iliyomkuta David Silva aliyefunga bao la kwanza.
Katika tuzo hiyo Iniesta alifanikiwa kuwapiku Andrea Pirlo wa Italia na nyota mwezake wa Barcelona, Xavi aliyetwaa tuzo hiyo mwaka 2008.
Iniesta amekuwa miongoni mwa wachezaji 10 wa Hispania wanaounda kikosi cha wachezaji 23 wa mashindano hayo.
Naye mshambuliaji wa Hispania, Fernando Torres amefanikiwa kutwaa Kiatu cha Dhahabu kufuatia kuibuka mfungaji bora na kumpiku mwenzake wa Ujerumani,Mario Gomez.
Mshambuliaji huyo mwenye miaka 28, alifunga bao moja katika ushindi wao wa mabao 4-0 dhidi ya Italia na kumfanya kuwa mchezaji pekee aliyefunga mabao katika mechi mbili tofauti za fainali.
Bao hilo lilimfanya kuwa sawa na Gomez aliyefunga mabao matatu na kutegeneza bao moja kwenye michuano hiyo iliyofikia tamati jana.
Hata hivyo, Uefa iliamua kumpa Torres zawadi hiyo kutokana na kutumia muda mchache uwanjani na kufunga mabao.
Nyota huyo wa Hispania alitumia dakika 189 kucheza mashindano hayo kulinganisha na Gomez aliyetumia dakika 280.
Wachezaji wengine wanne waliofunga mabao matatu ni Mario Balotelli (Italia), Cristiano Ronaldo (Ureno), chipukizi wa Russia, Alan Dzagoev na nyota wa Croatia, Mario Mandzukic.
Tuzo hiyo inamfanya Torres kumaliza vizuri zaidi msimu wa 2011/12 baada ya kutwaa Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa akiwa na klabu yake ya Chelsea, lakini ameshindwa kuingia kwenye kikosi cha wachezaji 23 wa michuano ya Euro 2012 kilichotajwa jana na Uefa.
Hispania imekuwa timu ya kwanza ya taifa kutwaa mataji matatu mfululizo tangu, Euro 2008, Kombe la Dunia 2010 na Euro tena mwaka huu.
A.Iniesta akitiririka
Huwa anakusanya Vijiji kama hivi
Fernando Torres mfungaji bora EURO 2012
Torres akitupia kambani mechi ya fainali dhidi ya Italia
Baba na wana
Famili inahusika katika ushindi bhanaa
Torres akiwa amebeba "ndoo" ya EURO 2012
Subscribe to:
Posts (Atom)