Wednesday, February 15, 2012
Zambia yaingia 50 bora viwango vya FIFA, 43 Duniani ya 4 Afrika
Timu ya soka ya Zambia maarufu kama Chipolopolo wamepanda kwa nafasi 28 juu na kuingia katika 50 bora za viwango vya soka vya FIFA baada ya miaka 11 tangu ilipowahi kuwa katika 50,sasa Zambia inashika nafasi ya 4 kwa ubora wa soka barani Afrika, Zambia imepata mafanikio hayo baada ya kunyakua ubingwa wa Afrika kwa kuinyuka Ivory Coast kwa mikwaju ya penati 8 kwa 7 katika fainali kali na ya kusisimua iliyochezwa nchini Gabon katika jiji la Libraville.
Katika viwango hivyo vya soka vilivyotolewa na FIFA Ujerumani imeivuka Uholanzi na kuwa ya pili wakati huohuo Ureno(6) imepanda nafasi 1,Ivory Coast(15) imepanda nafasi 3,Mali(44) imepanda kwa nafasi 25, Ghana (23) imepanda nafasi 3 na Italy(8) imepanda nafasi 1 nazo zikipata maendeleo mazuri katika viwango vya soka Ulimwenguni.
Barcelona yaichakachua Bayer Leverkusen 3-1
Alexis Sanchez akipigilia msumari wa pili
Katika mechi hiyo magoli ya Barcelona dhidi ya Bayer Leverkusen wafungaji wa magoli ya Barca ni Alexis Sanchez (2)dk 41,54 ,Messi(1)dk 88 na la kufutia machozi la Bayer Leverkusen lilifungwa na Kadlec dk 50
Beki wa Bayer Leverkusen akiokoa mpira mbele ya Messi aliekuwa akisubiri kuutupia wavuni.
Leonel Messi akichanja mbuga katikati ya beki za Bayer leverkusen
Bayer Leverkusen 1-3 Barcelona
Arsenal AC Milan kivumbi ligi ya mabingwa ulaya
Kocha wa Arsenal Arsene Wenger
AC Milan watakuwa na lengo moja la kuifunga timu ya England kwa mara ya kwanza tangu walipofanya hivyo dhidi ya Liverpool kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2007, wakati watakapowakaribisha Arsenal katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora ya mashindano hayo.
Milan iliyotwaa taji hilo mara saba kwa kuifunga Liverpool 2-1 jijini Athens miaka mitano iliyopita, baada ya hapo wamekuwa wakitolewa kwenye mashindano hayo na Arsenal, Manchester United na Tottenham Hotspur na alifanikiwa kupata sare dhidi ya Portsmouth kwenye hatua ya makundi ya Europa Ligi mwaka 2009.
Sasa wanakutana na Arsene Wenger kwa mara nyingine baada ya timu hiyo ya London kuwatoa Milan kwenye hatua ya 16 bora mwaka 2008.
Vinara hao wa Serie A, Milan watamtumia mshambuliaji wake Zlatan Ibrahimovic aliyefungiwa kucheza ligi kwa kumpiga kibao mchezaji baada ya kumaliza kifungo Jumamosi waliposhinda 2-1 dhidi ya wapinzani wao mbio za ubingwa wa Italia, Udinese huku chipukizi Stephan El Shaarawy na Maxi Lopez wakionyesha uwezo mkubwa wa kufunga.
Chipukizi El Shaarawy huenda akawekwa benchi ili kumpisha Ibrahimovic pamoja na kuwa kwenye kiwango cha juu kwa sasa na inavyoonekana kama mshambuliaji wa Sweden wataanza pamoja na Robinho.
Kocha Massimiliano Allegri ana wachezaji wengi majeruhi, lakini kumeonekana na mabadiliko kidogo na kutoa nafasi ya kurejea kwa kipa Christian Abbiati na beki wa kati Alessandro Nesta kuivaa Arsenal, ambayo imeshinda mechi zake zote za Ligi ya Mabingwa ilizocheza San Siro dhidi ya Milan.
Gennaro Gattuso na Alberto Aquilani bado ni majeruhi, lakini kuna nafasi ya Alexandre Pato na Kevin-Prince Boateng kuwepo kikosi leo.
Mabingwa watetezi Milan wanaongoza Serie A kwa tofauti ya pointi mbili, lakini Juventus inayoshika nafasi ya pili ina mchezo moja mkono.
“Ushindi wetu dhidi ya Udinese una maana kubwa, tumetoka kufungwa mechi tatu kati ya tano,” alisema kocha Allegri.
Milan, iliyofuzu kwa hatua hiyo pamoja na mabingwa watetezi Barcelona, hadi sasa wameshindwa kurudia mafanikio yao ya mwaka 2007.
MBINU za WENGER
Mafanikio katika mchezo huo ni mbinu atakayotumia Wenger kama atacheze kwa kujilinda zaidi na kutaka sare au kujaribu kushambulia ili kupata ushindi wake wa tatu dhidi ya Milan.
Wenger anatakiwa kujihadhari pia na mashambulizi ya Milan kwa kucheza kwa uangalifu zaidi, lakini kiungo wake Aaron Ramsey anaamini bao la ugenini linaweza kuwa jibu la mafanikio yao.Aliimbia Arsenal TV Online: “Kama tutacheza na kufanikiwa kupata bao na kurudi Emirates hayo yatakuwa matokeo ya kujivunia zaidi kwetu.
“Ni matumaini yangu, tutaweza kupata mabao mengi ya kuweza kuwaondoa kwenye mashindano.”
Vikosi:
AC Milan: 32-Christian Abbiati; 20-Ignazio Abate, 33-Thiago Silva, 5-Philippe Mexes, 15-Djamel Mesbah; 23-Massimo Ambrosini, 4-Mark Van Bommel, 10-Clarence Seedorf; 27-Kevin-Prince Boateng; 11-Zlatan Ibrahimovic, 70-Robinho
Arsenal: 13-Wojciech Szczesny; 3-Bacary Sagna, 5-Thomas Vermaelen, 6-Lauren Koscielny 17-Alex Song; 8-Mikel Arteta, 7-Tomas Rosicky, 16-Aaron Ramsey, 15-Alex Oxlade-Chamberlain; 10-Robin van Persie, 14-Theo Walcott
Mwamuzi: Viktor Kassai (Hungary).
RAGE 'AWARUHUSU' MASHABIKI WA SIMBA KUISHANGILIA ZAMALEK
Mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage
WAKATI Zamalek wakichekelea kurejea juu kiwango cha mshambuliaji Amr Zaki, tayari kuivaa Yanga, Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage amesema klabu yake hawezi kuwazuia mashabiki kushangilia timu wanayoipenda, kwani kinyume chake ni kuingilia uhuru mtu.
Simba na Yanga mwishoni mwa wiki hii zitakuwa kwenye michezo ya kimataifa, wakati mabingwa wa Tanzania watakuwa wenyeji wa Zamalek kwenye Uwanja wa Taifa katika Ligi ya Mabingwa, watani zao Simba inayocheza Kombe la Shirikisho itakuwa Rwanda kuivaa Kiyovu.
Akijibu malalamiko ya Yanga kuhusu baadhi ya mashabiki wa Simba kununua jezi za Zamalek kwa nia ya kuishangilia timu hiyo, Rage alisema si kitendo cha uungwana, lakini hawezi kuwazuia kufanya hivyo.
Viongozi wa Simba na Yanga mwaka jana walikubaliana kuzungumza na mashabiki wao ili timu hizo zinapocheza mechi za kimataifa wawe kitu kimoja jambo lililoshindakana.
"Unajua ni vigumu kuingilia uhuru wa mtu. Ni kweli nimeshuhudia mashabiki wa timu yangu wakianza kuvaa jezi za Zamalek, lakini na Yanga nao wakumbuke wakati sisi tukicheza na TP Mazembe hali ilikua kama hii.
"Sasa napenda kutoa tu wito kwamba pamoja na hili kushindikana, lakini kila mmoja atambue juhudi za wachezaji ndio pekee zitakazowainua kusonga mbele," alisema Rage.
Aidha kwa upande wa Yanga kupitia msemaji wao, Luis Sendeu alisema hawana shaka na hilo kwani wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanashinda na kuwataka mashabiki wao kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao ili iweze kufanya vizuri.
"Ni kweli wapinzani wetu wameanza kununua jezi zenye jina la Zamalek mahususi kuvaa katika pambano letu Jumamosi, lakini sisi tunasema hatutakata tamaa kwa hilo ingawa uongozi unalaani kitendo hicho," alisema Sendeu.
Wakati hali ikiwa hivyo hapa nyumbani mambo ni tofauti kwa Zamalek baada ya kocha msaidizi wa timu hiyo Ismail Youssef kusifu kiwango kilichoonyesha na wachezaji wake waliposhinda 4-1 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Itisalat.
"Tumefaidika sana na mchezo huu wa kirafiki kabla ya mechi yetu dhidi ya Yanga," alisema Youssef.
Mshambuliaji Zaki alifunga mabao mawili tangu aliporejea dimbani baada ya kumaliza matatizo yake ya kudai mishahara iliyomweka nje ya uwanja kuanzia mwezi Desemba.
Kumuona mshambuliaji huyo mwenye miaka 29 akiwa kwenye kiwango cha juu kimetoa faraja kwa Youssef kuwa sasa lengo la klabu hiyo kurudisha heshima yake Afrika litafanikiwa.
"Zaki amerudi kwa kiwango kizuri utakuwa msaada mkubwa kwetu dhidi ya Yanga," alisema kocha huyo.
Zamalek wanatarajiwa kutua nchini Ijumaa alfajiri na baadaye jioni kufanya mazoezi katika Uwanja wa Taifa kabla ya pambano lao siku inayofuata.
Subscribe to:
Posts (Atom)