Tuesday, August 9, 2011

CHAMBERLAIN ATUA RASMI ARSENAL

Kiungo wa Southampton Alex Oxlade Chambarlain ameafikiana na timu ya Arsenal baada ya timu hiyo kumfukuzia kwa miezi sita. Chamberlain alifanyiwa vipimo vya afya baada ya kuhitimisha uhamisho wake kutoka Southampton kwenda Arsenal kwa Dau la paundi za uingereza milioni 12.
"Nimekuja Emirates kuangalia mechi chache,nimevutiwa na mazingira pamoja na mashabiki na kila kitu hapa,hivyo ni vigumu kukataa ofa hii"alisema Chamberlain.

ARSENAL USO KWA USO NA UDINESE LIGI YA MABINGWA

Arsenal imepangwa kukipiga na Udinese katika mechi za kutafuta timu zitakazoingia kwenye makundi ya Ligi ya Ubingwa wa Ulaya.

The Gunners kama wanavyojulikana zaidi kwa mashabiki wao, wataanza kampeni hiyo nyumbani kwao uwanja wa Emirates dhidi ya timu hiyo ya Italia siku ya Jumanne tarehe 16 Agosti, na mchezo wa marudio utafanyika baada ya siku saba zijazo.
Bayern Munich watacheza na FC Zurich, FC Twente ya Uholanzi wataoneshana kazi na Benfica na Lyon watapepetana na Rubin Kazan ya Urusi.
Arsenal wanamatumaini ya kuungana na Manchester United, Chelsea na Manchester City katika mechi za makundi.
The Gunners wanakabiliana na kibarua cha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Ubingwa wa Ulaya kwa msimu wa 14 kwa sababu msimu uliopita wa ligi ya England walimaliza nafasi ya nne.
Katibu wa klabu ya Arsenal David Miles amesema Gunners wamefurahi kuepuka safari ndefu hadi Urusi kumenyana na Rubin Kazan.
"Itakuwa kibarua kigumu. Lakini hatutawadharau Udinese kabisa. Upangaji ulivyokwenda unatupa nafasi kwa mechi ya kwanza nyumbani na tuna matumaini tutautumia vyema," alisema Miles.
Udinese, walimaliza msimu wa ligi iliyopita ya Italia - Serie A kwa kushika nafasi ya nne. Msimu huu timu hiyo ilimuuza winga wake hatari Alexis Sanchez kwa klabu ya Barcelona, pia kiungo wa kutumainiwa Gokhan Inler kwa klabu ya Napoli.
Meneja mkuu wa Udinese Franco Collavini amesema: "Tunafanya kazi kubwa kukamilisha usajili wa klabu yetu itakapofika tarehe 31 mwezi wa Agosti.
"Tutahakikisha tunafanya kila liwezekanalo kuiandaa timu yetu kwa njia bora zaidi. Tunaiheshimu Arsenal. Ni moja ya vilabu muhimu Ulaya."
Wakati Aersenal walipotolewa katika Ligi ya Ubingwa wa Ulaya mwezi Machi dhidi ya Barcelona, mpachika mabao hodari wa timu hiyo Robin van Persie alioneshwa kadi ya manjano kwa kupiga mpira langoni baada ya mwamuzi Massimo Busacca kupuliza filimbi ya kuashiria ameotea.
Kutolewa huko kwa Van Persie ina maana hatacheza mchezo wa kwanza dhidi ya Udinese, wakati kiungo Samir Nasri pia alifungiwa na Uefa baada ya kutoa maneno makali kwa mwamuzi huyo Busacca.
Mechi ya kwanza ya Arsenal dhdi ya Udinese itakuwa katikati ya mechi yao ya kwanza ya kufungua msimu wa Ligi Kuu ya Soka ya England dhidi ya Newcastle na pia mechi yao na Liverpool katika uwanja wa Emirates, Jumamosi ya terehe 20 mwezi wa Agosti.
Mechi ya pili nchini Italia itakuwa tarehe 23 Agosti, Arsenal ikiwa njiani kwenda uwanja wa Old Trafford kuikabili Manchester United.
Timu 10 zitakazofanikiwa zitaingia katika makundi kukabiliana na timu zilizofuzu moja kwa moja, ambapo makundi yatapangwa mjini Monaco tarehe 25 Agosti.
Timu za kufuzu hatua ya makundi zimepangwa ifuatavyo:
Wisla Krakow v Apoel Nicosia
Maccabi Haifa v Genk
Dinamo Zagreb v Malmo FF
FC Copenhagen v Plzen
BATE v SK Sturm Graz
Odense BK v Villarreal
FC Twente v Benfica
Arsenal v Udinese
Bayern Munich v FC Zurich
Lyon v Rubin Kazan
Mechi za kwanza zitachezwa kati ya tarehe 16/17 na marudio ni tarehe 23/24 Agosti

CHELSEA YARIDHIA USAJILI WA LUKAKU

Chelsea imeafiki makubaliano ya kumsajili mshambuliaji kijana kutoka klabu ya Anderlecht Romelu Lukaku.

Romelu Lukaku

Lukaku mwenye umri wa miaka 18 atajiunga na klabu hiyo ya Chelsea inayojinoa kwa Ligi Kuu ya England, ikisubiria majibu ya afya yake na makubaliano ya mahitaji yake binafsi.
Klabu ya Anderlecht ilitangaza kumuu za Lukaku kupitia mtandao wao, lakini haikubainisha kiwango cha ada. Chelsea inaarifiwa mwezi dau lao la paundi milioni 18 lilikataliwa na klabu ta Anderlecht.
"Ni mchezaji kijana mwenye mtazamo wa mbali," alisema meneja wa Chelsea Andre Villas-Boas baada ya klabu ya Chelsea kushinda mechi yake dhidi ya Rangers siku ya Jumamosi.
"Kilichobakia hivi sasa ni kujitayarisha labda kumpata mchezaji huyu mwenye kipaji cha kupachika mabao."
Lukaku ni mchezaji maarufu nchini Ubelgiji msimu wa 2009/2010 alipkuwa na umri wa miaka 16 alikuwa mfungaji bora wa ligi ya nchi hiyo.
Wakati Chelsea wakikamilisha taratibu za kumnasa Lukaku, winga wao Yury Zhirkov, ameondoka katika klabu hiyo na kujiunga na klabu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi.
Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusiana na uhamisho wa Zhirkov lakini taarifa kutoka Urusi zimesema uhamisho wake utakuwa wa paundi milioni 13.2.
Zhirkov mwenye umri wa miaka 27 aliyejiunga na Chelsea akitokea klabu ya CSKA Moscow miaka miwili iliyopita, amesaini mkataba wa miaka minne na klabu ya Anzhi.
Mchezaji huyo ambaye alijiunga na Chelsea kwa kitita cha paundi milioni 18 na kucheza mechi 49 kwa klabu hiyo, alitambulishwa kwa mashabiki wa klabu hiyo ya Anzhi ilipokuwa ikicheza mechi ya ligi dhidi ya Tom Tomsk siku ya Jumamosi.

MAN UNITED YAIRARUA MAN CITY NGAO YA HISANI

Bao la Nani dakika ya 94 ya mchezo, liliiwezesha Manchester United kurejea katika mchezo kwa mtindo wa aina yake, ambapo hadi mapumziko walikuwa nyuma kwa mabao 2-0 na kufanikiwa kuwalaza mahasimu wao wakubwa wa mji mmoja Manchester City mabao 3-2 na kunyakua Ngao ya Hisani.

Wachezaji wa Man United wakishangilia ushindi

Huku kila mtu akiwa anajua mpambano huo utachezwa dakika 30 za nyongeza na hata ikibidi mshindi kupatikana kwa mikwaju ya penalti, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ureno, aliivuruga ngome ya Manchester City na kutimua mbio kasi sana na kumzidi mlinzi Kompany baada ya kusogezewa pande kutoka kwa Wayne Rooney, akamzunguka mlinda mlango wa City Joe Hart na kuujaza mpira wavuni pasi na wasiwasi. Lilikuwa bao zuri la tatu na la ushindi kwa Manchester United.
City waliongoza kwa mabao 2-0 hadi wakati wa mapumziko baada ya mlinda mlango mwanagenzi wa United, Mhispania David De Gea kuonekana akibabaika na kushindwa kuucheza mpira wa juu wa krosi, hali iliyomfanya Joleon Lescott kupachika bao kwa kichwa na pia bao la pili la mkwaju wa mbali uliopigwa na Edin Dzeko.
Lakini United, wakiwa wanajua mechi zao mbili za mwisho katika uwanja wa Wembley walipoteza, kufungwa na Barcelona katika fainali ya Ubingwa wa Ulaya, pia kulazwa na Manchester City katika nusu fainali ya kombe la FA, walibadilika na kujipanga vizuri na kuweza kuwanyima raha majirani wao na hatimaye wakarejesha mabao mawili haraka haraka.
Chris Smalling alikuwa wa kwanza kupunguza deni la mabao, baada ya kuunganisha mkwaju wa adhabu ndogo uliochongwa na Ashley Young kabla Nani kusawazisha kabla ya kuandika bao la tatu dakika ya mwisho ya mchezo.
Kwa uhaki vijana wa Sir Alex Ferguson walipoteana wakati Manchester City walipofunga mabao yao ya haraka, huku winga wao mpya Young akionekana kuzoea mazingira mapya.
Manchester City, kwa upande mwengine walikuwa wakitumia vyema kila idara uwanjani na walichokusudia katika kipindi cha kwanza ni kumfanya mwamuzi Phil Dowd awe na kibarua kigumu, huku mlinzi Micah Richards akiwa miongoni mwa wachezaji wanne waliooneshwa kadi ya manjano kwa kumchezea vibaya Young.

MACHAFUKO LONDON YAENDELEA

Kwa siku ya tatu mfululizo, machafuko na uporaji wa mali umeendelea katika maeneo kadhaa viungani mwa jiji la London. Majengo yameteketezwa moto maeneo ya Peckham na Hackney mashariki mwa London.

Jengo likiteketea kwa moto jijini london katika ghasia zinazoendelea.
Vijana waliovalia mavazi yaliyofunika nyuso zao wamevamia maduka na kupora bidhaa, huku polisi wakikumbwa na wakati mgumu kuthibiti ghasia.

Mji wa pili nchini Uingereza Birmingham umekumbwa na machafuko ambapo polisi wamewakamata washukiwa kadhaa.

Hali ya sasa imemlazimu Waziri Mkuu David Cameron kukatiza likizo yake nchini Italia na amekuwa na kikao cha dharura usiku kucha na waziri wake mambo ya ndani Teresa May,naibu wawaziri Mkuu Nick Clegg na Mkuu wa idara ya jeshi la Polisi.


Machafuko ya sasa yalianza Jumamosi usiku baada ya wakaazi wa Tottenham kuandamana kupinga kupigwa risasi na kuuawa kwa kijana mmoja.