Thursday, December 8, 2011

KILIMANJARO STARS KUTINGA FAINALI YA CECAFA LEO?












Kilimanjaro stars

LEO ni siku ya 363 tangu Uganda Cranes na Kilimanjaro Stars ya Tanzania Bara zilipokwaana katika nusu fainali mwaka jana ya Michuano ya Tusker Chalenji na leo timu hizo zinarudiana katika hatua hiyo.

Timu hizo zilimaliza dakika 120 zikiwa suluhu na katika mikwaju ya penalti, Bara ilishinda penalti 5-4.

Leo hii, timu hizo zinakutana kwenye Uwanja wa Taifa kuwania kucheza fainali. Ni wazi Uganda hawatotaka kurudia makosa ya mwaka jana wakati Bara inataka kuendeleza rekodi yake ya ushindi kama ilivyokuwa mwaka jana.

Kivutio kikubwa katika mchezo wa leo ni beki wa Kilimanjaro Stars, Juma Nyosso atakayesimama na mshambuliaji wa The Cranes, Emmanuel Okwi.

Itakumbukwa mwaka jana, wawili hao walivyokuwa wakichezeana ubabe na leo wanakutana tena. Nyosso na Okwi wanaitumikia klabu ya Simba.

Bara iliingia hatua hiyo baada ya kuilaza Malawi bao 1-0 wakati Uganda iliifungisha virago Zimbabwe kwa kuilaza idadi hiyo.

Mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani, utatanguliwa na mechi nyingine ya nusu fainali kati ya Rwanda na Sudan ambazo pia zinawania tiketi ya fainali ya michuano hiyo. Fainali imepangwa kufanyika keshokutwa.

Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Charles Boniface Mkwasa alisema kuwa vijana wake wote wapo kamili kwa mechi hiyo dhidi ya Uganda ambayo ni mabingwa mara 11 wa mashindano hayo ya Chalenji tangu yalipoanzishwa mwaka 1973.

Alisema amefanyia kazi kasoro kadhaa kwa kushirikiana na msaidizi wake Jamhuri Kihwelu na ana matumaini makubwa wa kufanya vizuri kwenye mchezo huo.

"Tumejipanga vizuri kuhakikisha tunaibuka na ushindi katika mchezo wa kesho (leo) dhidi ya Uganda ambayo imeonyesha uwezo mkubwa katika mashindano haya tangu yalipoanza kutimua vumbi.

"Baada ya ushindi wa jana (juzi) dhidi ya Malawi kwa hakika vijana wapo katika morali ya hali ya juu ukilinganisha na mechi nyingine zilizotangulia.

Katika hatua nyingine, Mkwasa amewataka Watanzania wote kushikamana na kuinunga mkono timu hiyo ili kuwatia nguvu za kupigana wachezaji wa Kilimnjaro Stars ili kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo.

Naye kocha wa Uganda, Bobby Williamson alisema kuwa leo timu yake itashuka uwanjani kwa kazi moja tu ya kuhakikisha inaibuka na ushindi katika mchezo huo licha ya kudai kuwa itakabiliwa na upinza mkubwa kutoka wa Kilimanjaro Stars.

Alisema Kilimanjaro Stars ilianza mashindano hayo vibaya lakini kadri mashindano hayo yanavyo zidi kusonga mbele inabadilika na kufanya vizuri hivyo mchezo huo wa leo hautakuwa mwepesi kwake huku akidai kuwa baadhi ya wachezaji wa timu hizo wanafahamiana.

Naye Calvin Kiwia anaripoti kuwa nahodha wa Uganda, Andrew Mwesiga amesema watahakikisha wanakuwa makini na winga wa Kili Stars, Mrisho Ngassa kuhakikisha haleti madhara.

Beki huyo mkongwe aliyekuwa akishuhudia pambano la robo fainali baina ya Kili Stars na Malawi alisema anamuona Ngassa kuwa ndiye mchezaji pekee hatari wa kuchungwa.

"Ni mchezaji mzuri, ana mbio na uwezo wakupiga chenga, hatuna budi kuweka tahadhari kubwa juu yake kuhakikisha haleti madhara kwetu," alisema Mwesiga.
"Tanzania 'Kili Stars' wanamtumia sana kutengeneza mashambulizi yake, nafikiri ndiye mchezaji ambaye tunaweza tukamwekea ulinzi zaidi," alisisitiza.

Alisema anaamini wakifanikiwa kufanya hivyo na kumdhibiti watakuwa wamejitengenezea nafasi nzuri ya kushinda pambano hilo na kutua fainali.
"Nafikiri 'Ngassa' ndio roho ya timu ya Tanzania anajituma vizuri na kucheza kwa ushirikiano na wenziye," alisema.
Ngassa hajaifungia Kili Stars bao lakini ametoa mchango mkubwa kwenye kikosi hicho, akitoa pasi ya mwisho kwa Nurdin Bakari aliyeifungia Tanzania bao la ushindi dhidi ya Malawi na penalti iliyofungwa na Mwinyi Kazimoto mchezo wa makundi na Zimbabwe