Roberto De Matteo
Roberto Di Matteo amefutwa kazi na klabu ya Chelsea, baada ya
kuwa meneja kwa kipindi cha miezi minane.
Di Matteo aliiwezesha Chelsea kuwa mshindi wa klabu bingwa barani Ulaya, na
vile vile kupata Kombe la FA msimu uliopita, na mwezi Juni, alitia saini mkataba
wa miaka miwli.
Lakini kufuatia Chelsea kuzabwa magoli 3-0 na Juventus usiku wa Jumanne,
inaelekea timu hiyo itakuwa na kibarua kigumu sana cha kufanikiwa kuendelea
katika michuano ya klabu bingwa, na kwa hiyo wasimamizi wa klabu wameonelea ni
vyema kumtimua kutoka Stamford Bridge.
Kulingana na taarifa katika mtandao wa Chelsea, "klabu kitatoa taarifa kamili
hivi karibuni kuhusiana na meneja wa timu".
Roman Abramovich, tajiri anayemiliki klabu ya Chelsea, sasa atakuwa
anamtafuta meneja wa tisa, tangu kumiliki klabu mwaka 2003, na kwa muda mrefu,
inaaminika amekuwa akizitamani sana huduma za aliyekuwa meneja wa Barcelona ya
Uhispania, Pep Guardiola.
Lakini vile vile amewasiliana na aliyekuwa kocha wa Liverpool ya Uingereza,
Rafael Benitez, na kuna uwezekano huenda akashikilia hatamu kwa muda mfupi.
Abramovich, raia wa Urusi, tayari alikuwa amewasiliana na Benitez hata kabla
ya Chelsea kushindwa nchini Italia.