Thursday, August 16, 2012

CHADEMA KUZINDUA TAWI HOUSTON MAREKANI Agosti 25,2012


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewatangazia wananchi wote kuwa Siku ya Jumamosi Aug 25 kutakuwa na ufunguzi rasmi wa tawi la chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA Jijini Houston, Texas Nchini Marekani
Wageni rasmi wa ufunguzi wa tawi hilo ni Mhe. Freeman Mbowe na Mhe. Jodeph Mbilinyi a.k.a Mr II/Sugu
Sherehe za ufunguzi wa tawi hilo zitaanza mida ya saa 5:PM (Jioni).

MASIKINI FABRICE MUAMBA, MPIRA NDIO BASI TENA


Fabrice Muamba

Mchezaji mahiri wa Timu ya Bolton Wanderers inayoshiriki ligi kuu ya Barclays Nchini Uingereza Fabrice muamba amestaafu rasmi soka baada ya kupokea ushauri wa mwisho kutoka kwa jopo la madaktari bingwa wa moyo na klabu ya Bolton ilitangaza rasmi Muamba kutocheza tena soka kufuatia matatizo ya kiafya.

Muamba akiongea kwa huzuni alisema amekuwa na ndoto za kurudi uwanjani na kukipiga katika klabu yake ya Bolton siku zote alizokuwa katika matibabu.
"Tangu kipindi nilipopata mshtuko wa moyo na kutolewa hospitalini, Nilikuwa na matumaini makubwa ya kuendelea na mchezo wangu wa soka na kuichezea Bolton Wonderers kwa mara nyingine" Alisema Muamba kwa huzuni kubwa.

Wiki iliyopita Muamba alisafiri mpaka Ubelgiji kwenda kufanyiwa oparesheni ndogo ya moyo na madaktari kumshauri kwasasa asahau kukipiga kutokana na hali ya afya yake.
Haya ndio maneno ya Fabrice Muamba wakati akitangaza kustaafu soka kutokana na matatizo ya kiafya.

“I have remained utterly positive in the belief I could one day resume my playing career.

“But the news was obviously not what I had hoped it would be and I am now announcing my retirement.
“Football has been my life. I count myself very lucky to have been able to play at the highest level.
“While the news is devastating, I have much to be thankful for.
“I thank God that I am alive and I pay tribute once again to the members of the medical team who never gave up on me.
“I would also like to thank everyone who has supported me throughout my career, and the Bolton fans.
“I am blessed to have the support of my family and friends at this time.”


Soma zaidi hapa: http://www.thesun.co.uk/sol/homepage/news/4488759/Fabrice-Muamba-retires-Bolton-ace-quits-over-heart-fears.html#ixzz23gqM1Uop Ikumbukwe Muamba al manusra apoteze maisha baada ya kuzimia kwa dakika 78 alipozirai wakati wa mechi kombe la FA kati ya Bolton na Tottenham katika dimba la White Hart Lane Machi 17,2012. Nae Mchumba wa Muamba, Shauna Muamba alikuwa na haya ya kusema “Thanks for all the support. We’re blessed to have our family and we’re looking forward to whatever the future holds.”
Soma zaidi hapa: http://www.thesun.co.uk/sol/homepage/news/4488759/Fabrice-Muamba-retires-Bolton-ace-quits-over-heart-fears.html#ixzz23grXAMIL



Daaah jembeee, pole sana yote maisha cha muhimu ni kumshukuru mungu kuwa upo hai mpaka leo baada ya kuzimia kwa masaa 78.

Picha za siku Muamba alipozima ghafla uwanjani







Fabrice Muamba katika uzi wa Bolton kabla ya kupatwa na matatizo ya kiafya(moyo).

STARS NGUVU SAWA NA BOTSWANA


Erasto Nyoni mfungaji wa goli la kwanza la Stars katika mazoezi kabla ya kuivaa Botswana

Taifa Stars imetoka sare ya mabao 3-3 na wenyeji Botswana (Zebras) katika moja kati ya mechi kadhaa za kirafiki za kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) zilizochezwa leo (Agosti 15 mwaka huu) usiku.
Hadi mapumziko kwenye mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Molepolole ulioko Kilometa 40 nje ya Jiji la Gaborone, timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2. Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 17 lililofungwa kwa penalti na beki Erasto Nyoni.
Mwamuzi Lekgotia Johannes Stars alitoa adhabu hiyo baada ya beki Oscar Obuile Ncenga wa Zebras kumuangusha ndani ya eneo la hatari mshambuliaji Mrisho Ngasa aliyekuwa akimkabili kipa Mompoloki Sephekolo.

Bao hilo halikudumu muda mrefu, kwani Zebras walisawazisha dakika ya 26 baada ya shuti kali lililopigwa naLemponye Tshireletso nje ya eneo la hatari kumshinda nahodha wa Taifa Stars, Juma Kaseja. Dakika tano baadaye kiungo mshambuliaji Mwinyi Kazimoto aliifungia Stars bao la pili kwa shuti la mbali.

Tshireletso aliisawazishia tena Zebras dakika ya 37. Mfungaji alifunga bao hilo kwa kichwa akiunganisha mpira wa krosi kutoka wingi ya kushoto uliopigwa na Tebogo Sembowa ambaye kabla alimtoka beki Aggrey Morris.
Kipindi cha pili kilianza kwa Kocha Kim Poulsen wa Stars kuwatoa Frank Domayo na Salum Abubakar na nafasi zao kuchukuliwa na Shabani Nditi na Athuman Idd. Safari hii Zebras ndiyo walioanza kufunga dakika ya 69 ambapo kiungo Michael Mogaladi aliifungia bao la tatu kwa kichwa akiunganisha krosi fupi iliyotokana na mpira wa kurusha.
Dakika 13 za mwisho Stars walicheza pungufu baada ya beki Erasto Nyoni kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na kumchezea rafu mshambuliaji Lovemore Murirwa.
Mrisho Ngasa ambaye alikuwa nyota kwenye mchezo huo aliisawazishia Stars dakika ya 84 baada ya kugongeana one-two na mshambuliaji Simon Msuva aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Haruna Moshi.

“Licha ya timu kucheza vizuri, tatizo kubwa lilikuwa kwenye safu ya ulinzi ambapo mabeki waliruhusu mipira mingi ya krosi na kuwaacha washambuliaji wa Botswana wakifunga bila bughudha. Mabeki hawatakiwi kuruhusu mipira ya krosi, wakiruhusu ni lazima wahakikishe wanawadhibiti washambuliaji wa timu pinzani.
“Kwa upande wa washambuliaji, Said Bahanuzi alikuwa akicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa akiwa na Stars tangu nilipomjumuisha kwenye timu kwa mara ya kwanza. Kuna makosa madogo madogo ambayo niliyatarajia, hivyo nitamrekebisha polepole,” alisema Kocha Poulsen mara baada ya mechi hiyo.

Stars; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Frank Domayo/Shabani Nditi,
Mrisho Ngasa, Salum Abubakar/Athuman Idd, Said Bahanuzi/Simon Msuva, Haruna Moshi/Ramadhan Singano na Mwinyi Kazimoto.
Zebras; Mompoloki Sephekolo, Tshepo Motlhabankwe/Tshepo Maikano, Edwin Olerile, Oscar Obuile Ncenganye, Mompati Thuma, Patrick Motsepe/Jackie Mothatego, Lemponye Tshireletso, Michael Mogaladi, Tebogo Sembowa, Ntesang Simanyana na Galabgwe Moyana/Lovemore Murirwa.

Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inarejea nyumbani kesho (Agosti 16 mwaka huu) ambapo itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 1.20 usiku kwa ndege ya Kenya Airways.
(Afisa habari TFF)

MGHANA WA SIMBA KUIKOSA LIGI KUU, YAWANIA JEMBE LINGINE KUTOKA MALI

KLABU ya Simba imesema mchezaji Aboul Karimu kutoka Mali atafanya majaribio na klabu hiyo hivi karibu na kama atafanya vyema hivyo atapewa nafasi ya kuitumikia klabu hiyo ya msimbazi.

Akizungumza na gazeti hili jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema Simba imekuwa na mazungumzo na wakala wa kimataifa Valer St.Clair kuhusu majaribio ya mchezaji huyo raia wa Mali.

“Endapo atafanikiwa kwenye majaribio anaweza kuwa mchezaji wa mwisho kusajiliwa kwenye dirisha la usajili na hivyo kupata nafasi ya kuitumikia timu ya Simba kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania bara na ligi Mabingwa Afrika,” alisema Kamwaga.
Mchezaji huyo anatarajiwa kutua nchini mwishoni mwa wiki hii na kuanza majaribio wakati dirisha la usajili likiwa linafikia tamati Septemba 10.

Vile vile klabu ya Simba jana ilichukua fursa ya kuwatambulisha wachezaji wake wapya wa kimataifa, MKenya Pascal Ochieng na Mghana Daniel Akuffor.

Kamwaga alisema beki wa kati Pascal Ochieng atachukua majukumu hayo kwenye Ligi Kuu ambayo iko karibuni kuanza wakati Daniel Akuffor atakuwa akiichezea wekundu wa msimbazi kwenye ligi ya mabingwa ya Afrika.

Kamwaga pia alisema Simba imeweka wazi kwamba mkataba wa Mchezaji mpya Daniel Akuffor utamalizika Mei mwakani.

Alisema,“mkataba wetu na Akuffor mwisho mwezi wa tano na hivyo kwenye makubaliano yetu hatacheza Ligi Kuu ila ataiwakilisha Simba kwenye ligi ya mabingwa ya Afrika.”

Simba itashiriki kwenye ligi ya mabingwa Afrika itakayoanza mwaka huu baada ya kutwaa kombe la ligi kuu ya Tanzania bara wakati huo huo timu ya Azam iliyomaliza katika nafasi ya pili itashiriki kwenye kombe la Shirikisho Afrika.

Wednesday, August 15, 2012

TAIFA STARS Vs BOTSWANA


Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania,Kili Taifa Stars wakiwasili katika uwanja wa ndege wa Sir Seretse Khama jijini Gaborone,Botswana. Timu ya Taifa ya Tanzania leo hii itajitupa katika dimba la Taifa la Molepolole mjini Gaborone kupepetana na Timu ya Taifa ya Botswana "The Zebras" ikiwa ni mchezo wa kirafiki wa kimataifa.

Tuesday, August 14, 2012

HANS POPE AIFUNGUKIA YANGA, MZAZI WA TWITE AHOFIA USALAMA WA MWANAE

Sakata la usajili wa Mbuyu Twite aliyejiunga Yanga, huku Simba nayo ikiingia naye mkataba, umeendelea kuwa 'kivutio', ambapo sasa Wekundu hao wa Msimbazi wameibuka na madai mapya.
Mwenyekiti wa Kamati ya usajili klabu ya Simba, Zacharia Hans Pope ameilaumu Yanga kwa kuuingiza mchezo wa soka kwenye machafuko.

Pope amesema kitendo cha wenzao kuwazunguka na kumshawishi Twite kurejesha fedha walizompa ili asajili Simba, kinaweza kuleta uhasama usio na ulazima."Tumepata taarifa kuwa baba mzazi wa Mbuyu (Twite) amemkataza mwanaye kuja kuichezea Yanga kwa hofu maisha yake."
"Mzee Twite anataka Simba na Yanga zikutane kufanya mazungumzo kwa lengo la kuweka mambo sawa kisha ndipo amruhusu kuja Tanzania," alisema Pope.
"Unadhani kwa kitendo walichofanya Yanga, mashabiki wa Simba watafurahi? Baba yake mzazi (Twite) amechukizwa na hali hiyo, anahofia usalama wa kijana wake," alisema Pope.
"Vita ya soka haina tofauti na ile ya siasa au dini. Kwa hiyo baba mzazi wa Mbuyu ameomba Yanga na Simba kumaliza suala hili mwanaye aweze kucheza soka kama ilivyo kazi yake."

Katika kusisitiza ukweli wa madai yao, Pope alisema tayari uongozi wa Yanga umeomba kukutana nao ili kuzunguza na kumaliza suala hilo.
"Ukweli ni kamba, hatuna tatizo na Yanga. Nafikiri siyo mara yao ya kwanza wala mwisho kutufanyia mchezo huu mchafu. Ni kawaida yao."

"Wameomba [Yanga] tukutane ili kumaliza utata wa suala hili, vinginevyo Twite hatakuja siyo kujiunga na Yanga au Simba, bali haji kabisa."
Aliongeza: "Tulianza mazungumzo na Bahanuzi (Said)wakatuzunguka na kumsainisha, ikawa hivyo tena kwa Kavumbagu (Didier) na sasa wametuma viongozi Kenya kutaka kumsainisha Pascal Ochien ambaye yupo na timu Arusha."

"Nafikiri Yanga kama wanataka kulipa kisasi cha mabao matano tuliyowafunga, wacheze mpira na siyo kutuzunguka na kusajili wachezaji wetu."
"Hata sisi tunaweza mchezo huo mchafu---ni kweli tunaweza kuwafanyia, lakini hatuoni sababu ya kufanya hivyo," alisema zaidi Pope.

Alipoulizwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Yanga, aliyefanikisha usajili wa Twite, Abdallah Bin Kleb, alikana kuwapo na makubaliano ya kukutana na Simba kuzungumza suala la mchezaji huyo.
Bin Kleb aliibeza kauli ya Pope na kusema inalenga kuwaziba mdomo mashabiki wa Simba ili wasahau kuzungumza suala la usajili wa Twite.

"Hakuna makubaliano ya sisi [Yanga] kukutana na Simba ili kuzungumza suala la Twite. Kwanza kwa nini tufanye hivyo wakati mchezaji tumemsajili kwa kufuata taratibu," alihoji Bin Kleb.
"Kama Simba wana matatizo na mchezaji ni wao, sisi hatuna matatizo na Twite wala mzazi wake, sasa iweje leo ashindwe kuja kujiunga na timu aliyopenda kuichezea?," alisema.

Alisema, Twite anatarajia kuja nchini wiki ijayo akitoka Kongo alikokwenda kuwasalimia wazazi wake ambao hakuonana nao muda mrefu.
Wakati huohuo, mshambuliaji mpya wa Simba George Ochan kutoka Kenya tayari ameshajiunga na wenzake, Arusha, huku Sihaune Abdulaziz kutoka Ghana akitarajia kutua leo.

MALIASILI KIMENUKA,MKURUGENZI WANYAMAPORI ATIMULIWA


Waziri wa Maliasili na Utalii Khamis Kagasheki

Mkurugenzi wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Obeid Mbangwa na wenzake wawili, wametimuliwa kazi kwa kashfa ya kutorosha wanyama hai 136 wa aina 14 tofauti kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), usiku wa Novemba 26, 2010.


Mkurugenzi wa Wanyamapori alietimuliwa kazi Obeid Mbangwa

Hatua hiyo imefikiwa baada ya tume mbili zilizoundwa kuchunguza suala hilo bila kuhusisha wizara yenyewe, kumaliza kazi yake na kukabidhi ripoti kwa Waziri.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki alisema jana mjini Dodoma kuwa mbali na watuhumiwa hao, mtumishi mwingine wa wizara hiyo amevuliwa madaraka, wawili wamepewa onyo kali la maandishi na wawili uchunguzi dhidi yao unaendelea.

Mbangwa wakati wa kashfa hiyo ya kusafirisha wanyama hai wanaokadiriwa kuwa na thamani ya Sh170 milioni kwa ndege ya kijeshi ya Qatar, alikuwa Mkurugenzi Msaidizi Matumizi ya Wanyamapori.
Wengine waliotimuliwa kazi ni Simon Gwera na Frank Mremi waliokuwa Maofisa Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha mkoani Arusha.

Mkurugenzi Msaidizi, Uendelezaji Wanyamapori, Boneventura Midala amevuliwa madaraka kutokana na kutochukua hatua kikamilifu za ulinzi ambazo zingeweza kuzuia kutokea kwa utoroshaji wa wanyama. Wakati wa tukio hilo alikuwa Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Kuzuia Ujangili.

Katika hatua hizo, maofisa wanyamapori daraja la pili, wawili waliotekeleza maelekezo ya wakuu wao wa kazi yaliyo kinyume cha sheria wamepewa onyo kali la maandishi.

Kagasheki aliwataja maofisa hao kuwa ni Ofisa Leseni ya Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha Arusha, Martha Msemo na Ofisa Leseni Ofisi ya Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha Dar es Salaam, Anthonia Anthony.

Rungu la wizara hiyo pia limemwangukia Mkuu wa Kituo cha Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha Arusha, Silvanus Ukudo aliyepewa onyo kali la maandishi kwa kushindwa kufuatilia kupata maelekezo ya Mkurugenzi wa Wanyamapori kuhusu mtumishi wake aliyekiuka sheria katika utoaji wa vibali.

Ukudo pia ameonywa kwa kushindwa kupeleka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, taarifa kuhusu mtumishi huyo ili achukuliwe hatua za kinidhamu.
Kagasheki alisema uchunguzi unaendelea dhidi ya watumishi wengine wawili, Ofisa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Mohamed Madehele na Ofisa wa Kituo cha Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha Arusha, Mariam Nyallu.

Alisema kwa upande wa wafanyabiashara waliohusika katika kashfa hiyo, kesi inaendelea mahakamani na kwa upande wa Qatar, Serikali alisema: “Tumefanya kila jitihada. Tumewasiliana kupitia Makao Makuu ya Cites, Geneva, Uswisi, lakini Qatar pamoja na kukubali kupokea maombi yetu kutoka Cites, imekaa kimya.”

Kuhusu hatua zaidi dhidi ya watuhumiwa hao, Waziri Kagasheki alisema: “Kwa kuwa imebainika walihusika na vibali vilivyosababisha hao wafanyabiashara wakamatwe, suala hilo halijaishia hapo.”
Waziri huyo alisema atajitahidi kadri ya uwezo wake kusimamia wizara hiyo ili kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa... “Sheria zipo nzuri, udhaifu mkubwa ni kwa watendaji wetu,” alisema.
Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo Mbangwa alisema hajui chochote.

Alisema hadi jana alikuwa hana taarifa za kufukuzwa kazi hivyo hawezi kusema chochote hasa bila ushahidi.

Unasema wamenifukuza kazi, ndiyo wametangaza hivyo? Mimi sina taarifa hizo na hivyo siwezi kuelezea chochote,” aling'aka Mbangwa.