Monday, November 14, 2011

Bunge Sports kushiriki mashindano ya mabunge ya Afrika mashariki Bujumbura

TIMU ya soka ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeingia kambini mjini Dodoma kujiandaa na michuano ya wabunge wa mabunge ya Afrika Mashariki, michuano itakayofanyika, Bujumbura, Burundi kuanzia Novemba 20.

Kocha wa timu hiyo, Kassim Majaliwa alisema kuwa kikosi chake kitaondoka Dodoma Novemba 19 kikiwa na wachezaji 25.Aliwataja wachezaji watakaoandamana na timu hiyo kuwa ni Amos Makala, William Ngeleja, Kighoma Malima, Sadifa Juma, Masauni Masauni, Erasto Zambi, Juma Nkamia na Steven Ngonyani.

Wachezaji wengine wanaounda timu hiyo ni; Haeshi Khalfan, Muiguru Mchemba, Ali Kingwangwala, Abdul Mteketa, Ngwali Juma, Victor Kawawa, Fakhi Haji Fakhi, Mahamoud Mgimwa, Chris Kimnyonyele na Job Lusinde.

Majaliwa ambaye ni Naibu Waziri wa Tamisemi aliwataja wengine kuwa ni Mambi Mumbala, Mark Kilumbi, Kassim Fundi na Michael Kadebe wakati daktari ni Kassim Ramadhani na Cesilia Sanya.

Mashindano hayo yatashirikisha nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Tanzania na wenyeji Burundi. Mwaka jana yalifanyika Arusha na Tanzania ilitwaa ubingwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Prof. Maji Marefu alisema maandalizi yanakwenda vizuri na timu yake iko vizuri kutetea ubingwa.

Stars yaifunga Chad 2-1

Mbinu ya kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Jan Poulsen ya kushambulia mwanzo mwisho katika mechi dhidi ya Chad, ilizaa matunda jana baada ya kuibuka na ushindi wa kwanza ugenini wa mabao 2-1 mechi ya kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi fainali za Kombe la Dunia, shukrani kwa Nurdin Bakari aliyefunga bao la ushindi kwenye mechi hiyo.
Nurdin aliyeingia toka benchi, alifunga bao hilo katika dakika ya 85 akimaliza pasi nzuri ya Thomas Ulimwengu na kuwanyamazisha mashabiki wa Chad waliojazana kwenye Uwanja wa Idriss Mahamat.Huu ni ushindi wa kwanza ugenini wa kocha Poulsen tangu aanze kuifundisha Stars akichukua nafasi ya kocha Marcio Maximo.
Matokeo haya ni mazuri kwa Stars na angalau yametuliza kiu ya mashabiki wa soka nchini ambao kwa muda mrefu wamekuwa wanyonge kila timu yao inapocheza.Ili iweze kuingia hatua ya makundi, sambamba na Morocco, Ivory Coast na Gambia, Stars itahitaji sare tu katika mechi ya marudiano itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wiki ijayo.
Mara baada ya mchezo kumalizika, Poulsen alisema kikosi chake kilicheza vizuri, na anashukuru mfumo wake wa kushambulia mfululizo ulizaa matunda.
Stars iliyotua mjini N'djamena siku moja kabla ya pambano, walioonekana kuwa na hamu ya kupata ushindi wa ugenini, walianza mchezo kwa kasi, na ndani ya dakika ya kwanza tayari walikuwa wameshafika langoni mwa wapinzani wao.
Falsafa ya kocha wa Stars Jan Poulsen ya kushambulia mwanzo mwisho, ilionekana kuwa kasi tangu mwanzo, baada wachezaji wake kugongeana vizuri pasi bila wenyeji kugusa mpira na kulazimisha kona dakika ya kwanza lakini bila kuzaa matunda.
Taifa Stars ambayo kwa mara ya kwanza jana ilishuhudia Shomari Kapombe akianza kwenye kikosi cha kwanza Poulsen, iliandika bao la kuongoza dakika ya 12 kupitia kwa Mrisho Ngassa.Ngassa alifunga bao hilo tamu baada ya kutumia akili nyingi na maarifa kuvunja mtego wa kuotea na kumfunga kipa wa Chad Brie Mbaya, ikiwa ni pasi ya Nizar Halfan.
Baada ya bao hilo, wenyeji Chad walicharuka na iliwachukua dakika tatu baadaye kufunga bao la kusawazisha likiwekwa kimiani na mshambuliaji Labo Mahamat.Bao hilo lilianza kwa mpira wa adhabu ndogo kufuatia winga wa pembeni wa Stars, Mrisho Ngassa kumchezaji faulo staa wa Chad Ndousel Ezekiel.
Karim Yaya alipiga adhabu hiyo na kumkuta mfungaji aliyeunganisha wavuni. Ngassa alionyeshwa kadi ya njano kwa kosa hilo.Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, huku Stars wakitawala nusu ya kwanza ya kipindi cha kwanza kupitia kuelewana vizuri kwa viungo wanaocheza soka la kulipwa, Abdi na Nizar.
Hata hivyo, wenyeji Chad waliokuwa wakiongozwa na nyota wao Mahamat na Ezekiel, walicharuka nusu ya mwisho ya kipindi hicho baada ya kuusoma mchezo wa Stars.Kikosi cha Stars kilikuwa, Kaseja, Kapombe, Idrisa, Morris, Nyosso, Henry, Nditi, Ngassa, Abdi, Samatta na Nizar.

Esperance yatwaa ubingwa wa Afrika



BEKI Harrison Afful aliifungia bao la ushindi, Esperance ya Tunisia katika mechi ya fainali ambayo Wydad Casablanca waliokuw 10 uwanjani walilala kwa bao 1-0 katika mchezo wa pili wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Afful alifumania nyavu katika dakika ya 21, aliingia ndani ya eneo la hatari na kuachia mkwaju uliopmpita kipa wa Wydad, Yassine Bouno—aliyesimama langoni kuchukua nafasi ya mkongwe Nadir Lamyaghri aliyeumia mazoezini.

Esperance iliyotwaa ubingwa mara ya mwisho 1994, wakati Wamorocco wa Wydad walitwaa ubingwa mwaka ’92.Timu hizop mbili kutoka Kaskazini mwa Afrika zilitoka suluhu katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye mji wa Casablanca wiki moja iliyopita.

Wydad ilipunguzwa kasi baada ya mchezaji wake, Mourad Lemsen kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Yannick N’Djeng.Esperance iliyopigwa 6-1 na TP Mazembe ya DR Congo katika fainali ya mwaka jana. Esperance pia iliingia fainali mwaka 1999 na kufungwa na Raja Casablanca Morocco kwa penalti na mwaka uliofuata ilifungwa na Hearts of Oak.

Lakini safari hii ikicheza mbele ya mashabiki 50,000 waliojazana Stade 7 November mjini Rades walikuwa na kila sababu ya kushinda.Baada ya bao, Afful alitengeneza mipira mingi ikiwemo wa dakika ya 28 alipomtolea pande Oussama Darragi, akiwa ndani ya eneo la hatari, alipaisha mpira huo.

Wydad ilishindwa kusawazisha nafasi ya wazi katika dakika ya 32 wakati Fabrice Ondama lakini shuti lake liliokolewa na kipa wa Esperance, Moez Ben Cherifa.

Friday, November 11, 2011

Reggie Love"Obama's little Brother" kuacha kazi na kuondoka Ikulu ya Marekani "WHITE HOUSE"


Obama na Reggie wakicheza mpira wa kikapu.

Huenda hakuna msaidizi wa ikulu ya Marekani aliye karibu zaidi na Rais Obama zaidi ya Reggie Love, Love mwenye umri wa miaka 30 ni mchezaji wa zamani wa mpira wa miguu na kikapu ambaye amekuwa msaidizi wa Rais Obama tangu kipindi alipokuwa seneta.

Akiwa msaidizi binafsi wa Obama Love amekuwa nae karibu zaidi bila hata kuacha umbali wa futi kadhaa pindi anaposaini Aotographs na anapoweka "swaga" kwa ajili ya kupiga picha.

Amekuwa karibu zaidi na Obama na mara nyingi wamekuwa wakicheza Mpira pamoja na Obama amekaririwa akisema Reggie Love ni mdogo wake na mtu wake wa karibu ambavyo hajawahi kutokea,na sasa anaondoka.



Muda wa mazoezi..Obama akiwa katika jogging,Reggie hayuko mbali

Reggie akiwaonesha jambo maafisa wa Ikulu pamoja na Rais Obama


Nipe Gwala...Obama akimpa tano Reggie

Obama ndani ya Gari na "mdogo wake" Reggie



Obama akiteta jambo na Reggie

Obama akifunga kwa staili ya Lay up

Obama na Reggie wakikatiza mitaa kuelekea mazoezini

Reggie kipindi anacheza mpira wa Kikapu na timu ya Duke

Love akipiga chabo kwanza kabla ya Obama kutoka


Obama na Reggie ndani ya ndege ya rais




Ikulu ya Marekani haijatoa taarifa zaidi ya kuondoka kwa Reggie Love lakini watu wa karibu wamesema Reggie anataka ajikite zaidi katika kumalizia Masters yake katika chuo kikuu cha Pennsylvania (University of Pennsylvania's Wharton Business School).

Mkali wa Kwenye udongo vs mkali wa kwenye nyasi


Uwanja huu sio wakugushi, mastaa Roger Federer na Rafael Nadal walipepetana katika maonesho ya mwaka 2007 katika jiji la Mallorca huko Spain. Ukiwa umetengenezwa kwa udongo nusu uwanja na nusu uwanja nyasi nia na madhumuni kumpata bingwa wa viwanja vya aina zote, ambapo Nadal aliibuka na ushindi wa seti tatu dhidi ya Federer.

Uwanja wa Tennis wa ajabu zaidi Duniani.


Huu ni uwanja ambao utawekwa kwenye kumbukumbu zaidi kwa kuwakutanisha Andre Agassi na Roger Federer zaidi ya walipokutana Wimbledon,U.S open au katika viwanja vingine. Uwanja huu upo futi 700 juu ya pwani ya Jumeirah katika hotel ya nyota saba ya Burj Al Arab nchini Dubai. Mpambano huo ulifanyika february 2005.

Taifa Stars uso kwa uso na Chad leo 11-11-11.

Timu ya taifa ya Tanzania,TAIFA Stars leo itacheza staili ya kushambulia mwanzo-mwisho dhidi ya wenyeji wao timu ya taifa ya Chad katika pambano muhimu la awali kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia. Mechi inapigwa kwenye Uwanja wa Idriss Mahamat Ouya jijini N’Djamena.

Mbwana Samatta anatarajiwa kuongoza mashambulizi ya Stars dhidi ya Chad leo
 
Kocha wa Stars, Jan Poulsen amekumbushia falsafa yake ya kucheza kwa kushambulia, ambapo atawatumia viungo wawili na kujaza washambuliaji mbele Abdi Kassim, Nizar Khalfan, Mrisho Ngassa na Mbwana Samata.

Stars waliwasili jijini N’dJamena saa saba usiku juzi kwa ndege ya shirika la ndege la Kenya itaingia uwanjani ugenini kusaka matokeo bora katika pambano hilo la awali kabla ya kurudiana na wenyeji wao katika uwanja wa taifa Jumanne jioni.

Katika kujiandaa na  pambano la leo, jana Stars walifanya mazoezi yao jioni katika uwanja wa Idriss Mahamat Ouya huku wakimkosa mlinzi wa kulia wa timu hiyo, Erasto Nyoni ambaye alianza kusumbuliwa na malaria tangu alipotua jijini N’Djamena.

Kwa mujibu wa Poulsen, kiungo chipukizi, Shomari Kapombe anatazamiwa kuziba nafasi ya Nyoni huku winga mahiri Mrisho Ngassa akitazamiwa kuanza pambano hilo baada ya kukosekana katika vikosi vya kwanza vya kocha Poulsen katika mechi za karibuni.
Kurudi kikosini kwa Ngassa kunatokana na kujitoa kwa mshambuliaji Danny Mrwanda ambaye amekuwa akianza katika mechi za karibuni kama mshambuliaji anayesaidia mashambulizi kuanzia upande wa kushoto.
Poulsen ameimbia Mwananchi, haifahamu timu ya Chad lakini akaahidi kubadili fomesheni ya Stars dakika kadhaa baada ya kuanza kwa pambano hilo kutokana na jinsi atakavyowasoma wapinzani wake.
“Siijui vizuri Chad. Nitawaangalia katika dakika 20 za mwanzo na kama kuna uwezekano wa kubadili fomesheni basi nitafanya hivyo. Lakini kama ilivyo kawaida yangu, asilimia 95 ya mchezo wa timu yangu unategemea zaidi na jinsi tunavyocheza wenyewe kuliko ambavyo mpinzani wetu anacheza.” alisema Poulsen.
Hata hivyo, Poulsen alisema atafurahi zaidi kucheza soka la kushambulia kwa ajili ya kupata matokeo mazuri badala ya kucheza soka la kujihami ambalo haliisaidii timu.
Naye kocha wa Chad ambaye kikosi chake kilifanya mazoezi ya mwisho katika uwanja wa Idriss Mahamat Ouya, Mohamed Omary alisema dakika tisini ndio zitaaamua mshindi wa leo na si vinginevyo.
“Sichezi mpira nje ya uwanja. Nacheza ndani ya uwanja. Dakika tisini ndio zitaamua matokeo ya mechi ya kesho (leo).” Alisema Omary
Endapo Stars itapata matokeo mazuri katika mechi zake mbili dhidi ya Chad ambazo zinachezwa ndani ya siku nne, itapata nafasi ya kucheza kundi la kufuzu kwenda kombe la dunia ikipangwa pamoja na Gambia, Ivory Coast na Morocco
Mwamuzi wa pambano la leo ni Ogunkolade Bunmi wa Nigeria akisaidiwa na Abidoye Tunde na Baba Abel ambao wote pia ni Wanigeria.
 
Kwa mujibu wa Poulsen kikosi kamili cha Stars leo ni Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Juma Nyoso, Idrisa Rajab, Shaabani Nditi, Henry Joseph,
Abdi Kassim, Nizar Khalfan, Mrisho Ngassa na Mbwana Samata