Monday, March 19, 2012

SIMBA S.C NI NOMAAAA YAILIZA MTIBWA 2-1


Siku ya jana ilikuwa mbaya kwa kiungo Patrick Mafisango jana alipiga penalti mara mbili akakosa, lakini bado Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.
Mafisango alikosa penalti hiyo iliyotokana na mshambuliaji Emmanuel Okwi kuchezewa rafu katika eneo la hatari katika dakika ya 59. Alipiga mara ya kwanza akakosa lakini mwamuzi akaamuru irudiwe kwa madai ya kipa kuvuka mstari, hata hivyo alipopiga tena Deogratius Munishi ambaye ni kipa wa zamani wa Simba akadaka tena.
Katika mchezo huo, Simba walipata bao katika dakika ya 18 lililofungwa na Mafisango baada ya kuitumia vizuri krosi ya Okwi. Mtibwa Sugar walirejea kwa kasi katika kipindi cha pili na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 52 kupitia kwa Hussein Javu aliyepiga shuti kali nje kidogo ya eneo la hatari.
Huku timu zote zikionekana kushambuliana kwa zamu, walikuwa ni Simba waliofanikiwa kutikisa nyavu za wapinzani wao baada ya mshambuliaji mrefu, Felix Sunzu kufunga kwa kichwa akipokea mpira wa faulo iliyopigwa na Okwi.
Mtibwa ndiyo waliowahi kulisakama lango la Simba katika dakika ya tatu. Mshambuliaji wa timu hiyo, Javu alibaki yeye na mlinda mlango Juma Kaseja lakini akashindwa kuutumbukiza mpira wavuni.
Beki wa Simba, Mkenya, Derrick Walulya, jana alicheza mechi yake ya kwanza ya ligi tangu asajiliwe na Wekundu wa Msimbazi, Januari, mwaka huu, ingawa alilaumiwa na wachezaji wenzake uwanjani kwa kuonekana kuwa uchochoro, alijitahidi kwa kiasi chake.
Baada ya mchezo huo, Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic, aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri huku akiuponda Uwanja wa Jamhuri kwamba hauna ubora, wakati Kocha wa Mtibwa, Tom Olaba alimshutumu mwamuzi kwa kushindwa kuchezesha vizuri pambano hilo.
Katika michezo mingine iliyopigwa jana, Azam iliifunga Ruvu Shooting kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, wakati Toto African ilifufua matumaini yake ya kubaki ligi kuu kwa kuibamiza Polisi kwa mabao 2-1 katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

MAN UNITED KIBOKO,YAITENGENEZA WOLVES 5-0


Welbeck akishangilia goli

Manchester United imezidi kujichimbia kileleni mwa Ligi Kuu ya England na kuongeza wigo wa pointi nne dhidi ya Manchester City, baada ya kuilaza Wolves mabao 5-0.
Jonny Evans alikuwa wa kwanza kuipatia bao Manchester United, kabla mlinzi wa Wolves Ronald Zubar hajatolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya manjano.
Hali hiyo ilikuwa ni afueni kwa wageni ambapo Antonio Valencia alifunga bao la pili kabla ya Danny Welbeck kutumbukiza wavuni bao la tatu.
Man U 5-0 Wolves

Javier Hernandez baadae alipachika bao la nne kwa kuunganisha vyema mpira wa pembeni uliopigwa na Valencia na muda mfupi baadae Steven Fletcher nusura aipatie Wolves bao la kufutia machozi. Alikuwa Hernandez tena aliyeifungia Manchester United bao la tano.
Wolves sasa wameshinda mchezo mmoja tu kati ya michezo 14 iliyopita ya ligi na wanamuweka meneja wao wa muda Terry Connor katika wakati mgumu wakiwa mkiani mwa msimamo wa Ligi.
Hii ni mechi ya tatu Wolves kupoteza wakiwa chini ya Connor katika mechi nne alizosimamia na wameshafungwa mabao 12 katika mechi tatu na wao bila kutumbukiza mpira wavuni.
Kwa kikosi cha Sir Alex Ferguson ushindi huo umewaongezea hazina ya mabao na kupunguza wigo wa mabao dhidi ya Manchester City na sasa kuwa mabao matatu tu.

FABRICE MUAMBA MAHUTUTI BAADA YA KUANGUKA NA KUZIMIA KWENYE MECHI

Fabrice Muamba kabla ya  kuzirai uwanjani
Fabrice Muamba muda mfupi kabla hajaanguka na kuzirai

Kiungo wa Bolton, Fabrice Muamba, anakabiliwa na saa 24 muhimu sana za maisha yake, meneja wa Bolton Owen Coyle alisema.
Bado anatibiwa katika kitengo cha wagonjwa mahtuti.
Meneja wa Bolton Wanderers, Owen Coyle, alisema anatumai matokeo yatakuwa mema kwa Fabrice Muamba, huku mchezaji huyo anaendelea kuuguzwa.
Coyle alisema hayo nje ya London Chest Hospital, ambako ndiko Fabrice anakotibiwa baada ya kuzirai wakati Bolton Wanderers wanacheza na Tottenham Hotspur kwenye uwanja wa White Hart Lane saa 12 magharibi.
Imejulikana leo kuwa matabibu wasaidizi hawakuweza kuufanya moyo wa kijana huyo wa umri wa miaka 23, kuanza kupiga tena wenyewe kwa karibu saaa mbili, baada ya kubanwa na moyo.
Bolton Wanderers wakicheza na Tottenham Hotspur kwenye robo fainali ya kombe la FA.
Coyle aliwaambia waandishi wa habari: "Tunatumai atapona"
Muamba alizaliwa Zaire (sasa inajulikana Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo) na alifika England akiwa na umri wa miaka 11.
Mchezaji huyo kabla ya kujiunga na Bolton Wanderers alitokea klabu ya Birmingham mwaka 2008 na amecheza mechi 148 katika klabu yake ya sasa.
Mashabiki wa timu zote mbili walikuwa wakiimba jina la Muamba wakati alipokuwa akitolewa uwanjani kwa machela.
Na Muamba alikumbukwa katika mechi zote zilizochezwa Jumapili

Friday, March 16, 2012

MAN U YACHEZESHWA UKUTI NA ATHLETICO BILBAO YACHAPWA KINOMANOMA


Golikipa De Gea akichumpa bila mafanikio na kuruhusu mpira uliopigwa na Llorente kutinga wavuni na kuandika bao la kwanza kwa Athletico Bilbao.

Manchester United jana ilipokea kipondo cha kufa mtu kutoka kwa timu ngumu ya Uhispania Athletico Bilbao cha kamba 2-1.
Katika mchezo huo wa 16 bora ya ligi ya mabingwa sio mwingine bali ni Llorente aliyeanza kutupia kambani kwa shuti kali lililomuacha hoi golikipa wa Man United De Gea akichumpa bila mafanikio na kuipatia Athletico Bilbao bao la kuongoza katika dakika ya 23.
Ngozi iliendelea kusukumwa na kwa mara nyingine tena De Marcos katika dakika ya 65 aliinyong'onyesha Man United na kuwalaza unono mashabiki wa Man U kwa kutupia kambani bao la pili.

Wachezaji wa Man United wakishangilia goli la Rooney.

Goli 2-0 zilidumu mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika na timu zote kwenda vyumba vya kupumzikia huku Man U wakiwa vichwa chini na Athletico Bilbao wakiingia vyumbani vifua mbele.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Bilbao wakionekana kuridhika na goli mbili na kuanza kulinda,soka lilipigwa kiasi cha mashabiki wa Man United kuanza kuachia viti na kutafuta milango ya kutokea..hamad mungu sio Athumani,alikuwa ni mchezaji kipande cha mtu Wayne Rooney katika dakika ya 80 alipofanikiwa japo kutikisa nyavu na kuipatia Man United bao la kufutia machozi na kuwarudishia uhai mashabiki wa Man United waliokuwa wakipumulia mipira kwa dakika zote 80.
Man United 2-1 Athletico Bilbao

Thursday, March 15, 2012

MAMA AJERUHI MWANAWE KWA MPIRA

Video hii inaonesha tukio lililotokea huko majuu ambapo mtoto alikuwa akicheza mpira katika bustani ya nyumbani kwao, mama kwa upendo akaona akajiunge na mwanae katika kucheza lile kabumbu.
Wakati mama na mwana wakirukaruka huku na kule wakisukuma lile kabumbu kwa muda fulani kama kawaida kitu chochote hasa michezo ukiufurahia sana mzuka unapanda si kitoto,balaa lililotokea baada ya mama na mwana kupandwa na mzuka wa soka ni mama kujikuta akifumua shuti la kwelikweli kuelekea kwa mwanawe na kwa bahati nzuri au mbaya mama alifumua shuti lililokwenda moja kwa moja kwenye uso wa mwanawe kama unavyoona wachezaji wanapofumua mashuti na kutinga wavuni basi ndivyo ilivyokuwa.
Mtoto ilibidi aangue kilio baada ya shuti kutua sawasawa katika paji la uso wake, mama alipatwa na kazi ya ziada kumnyamazisha mtoto na hatimae mtoto alinyamaza na kama ilivyo kawaida kwa watoto hawana kinyongo muda uleule akatabasamu na akaanza tena kucheza mpira huku akimuita mama yake, safari hii mama alikuwa kama kafungwa mawe miguuni alishindwa kabisa kupiga mpira.

Tuesday, March 13, 2012

ARSENAL "GUNNERS" WAIRARUA NEWCASTLE BILA HURUMA


Robin Van Persie "R.V.P" akitupia kambani goli la kusawazisha dhidi ya Newcastle


Thomas Vermaelen na Sagna wakishangilia goli la pili na la ushindi

Thomas Vermaelen alifunga bao la ushindi katika dakika ya 95 dhidi ya Newcastle, na kupunguza tofauti ya pointi kati yake na Tottenham kuwa ni pointi moja tu.
Tottenham imo katika nafasi ya tatu, na Arsenal inashikilia nafasi ya nne.
Hatem Ben Arfa aliwawezesha Newcastle kupata bao la kwanza katika mechi hiyo ya Jumatatu jioni kwa bao la chini kwa chini, lakini furaha yao ilizimwa hata kabla ya dakika moja kumalizika.
Theo Walcott alimsukumia mpira Robin van Persie, na ambaye alifunga bao lake la 33 msimu huu.
Mvutano ulizuka uwanjani baada ya kipenga cha mwisho, kufuatia bao la Vermaelen ambalo liliingia wavuni huku mechi ikielekea kumalizika, na mechi hiyo ikiwa ni ya nne ambayo Arsenal, baada ya kuachwa nyuma, iliweza kujitahidi na kupata ushindi.
Ulikuwa ni ushindi wa kusisimua kwa mashabiki wa Arsenal, timu ambayo imecheza vizuri sana hivi karibuni, hasa ikifikiriwa kwamba majirani Spurs walikuwa na tofauti ya pointi 12 kati yao na Arsenal, kabla ya mechi sita zilizopita.
Arsenal 2-1 Newcastle United 

Monday, March 12, 2012

Swansea yaipopoa Man City Kileleni, Man United yakalia usukani


Wayne Rooney akitupia kambani goli la kwanza la United dhidi ya WBA.

Manchester United imefanikiwa kukalia kiti cha Ligi ya Kuu ya England kwa mabao mawili yaliyopachikwa na Wayne Rooney na kuilaza West Brom.
United imepata nafasi hiyo ya kukalia kiti cha uongozi baada ya Manchester City kuteleza kwa kulazwa bao 1-0 na Swansea.
Rooney aliifungia Manchester United bao la kwanza kabla ya mapumziko, alipounganisha mpira uliopigwa na Javier Hernandez ambao ulimpita mlinda mlango Ben Foster.
Mshambuliaji huyo wa Manchester United alifunga tena bao la pili kwa mkwaju wa penalti, wakati mlinzi wa West Brom Jonas Olsson alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya njano.
Man united 2-1 West Bromwich Albion

Wakiwa wamesaliwa na michezo 10 kabla ya msimu wa ligi kumalizika, Manchester United sasa wanapewa nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wake baada ya Manchester City kuteleza.
Matumaini ya Manchester City kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya Kandanda ya England yaliingia dosari baada ya bao la kichwa dakika za mwisho la Luke Moore lilipoipatia Swansea ushindi wa bao 1-0.

Young na Rooney wakishangilia Goli

wansea City kwa ushindi huo sasa imeacha wazi mbio za kuwania ubingwa ligi ya England baada ya ushindi huo katika uwanja wao wa Liberty.
Kikosi cha Roberto Mancini kiliponea chupuchupu kufungwa dakika za mwanzo za mchezo wakati Joe Hart alipookoa mkwaju wa penalti wa Scott Sinclair baada ya Hart kumuangusha Wayne Routledge ndani ya sanduku la hatari.
Swansea ilipata bao lake hilo moja baada ya Moore kuunganisha kwa kichwa mpira wa pembeni wa Routledge zikiwa zimesalia dakika saba kabla mchezo kumalizika.
City hawakucheza vizuri ingawa Micah Richards dakika za mwisho alifunga bao ambalo lilikataliwa kwa vile alikuwa ameotea.
Manchester City sasa wanashikilia nafasi ya pili wakiwa na pointi 66 na Manchester United wamekusanya pointi 67.