Monday, May 21, 2012

CHELSEA YATWAA NDOO YA LIGI YA MABINGWA WA ULAYA


Wachezaji wa Chelsea wakiwa na mwali wa ligi ya mabingwa ulaya

Meneja wa mda wa Chelsea Roberto di Matteo alipoingia mkutano wa wandishi wa habari kwa mazungumzo ya baada ya mechi saa saba na robo usiku wa manane, akijivunia rekodi kubwa kwa meneja yeyote wa muda kuwahi kushinda, machungu ya Chelsea daima kukosa Kombe la Ligi ya mabingwa tayari yalikua yamefutwa kwa dawa nyepesi kutamka, Ushindi.
Didier Drogba alipojipanga, bila pupa,wasiwasi wala hofu na kuupiga mpira ule kumpita golikipa wa Bayern, Manuel Neuer, mwenye sifa ya kuzuia mikwaju ya penati na kuthibitisha ushindi wa 4-3 kupitia matuta, miaka mingi ya kosa kosa iliwatoka wachezaji wote,wafanyakazi na viongozi wa Chelsea.

Manager Roberto Di Matteo of Chelsea speaks to the media during a press conference at Chelsea Training Ground on May 15, 2012 in Cobham, England.
Kocha wa Muda wa Chelsea Robert Di Matteo aliyeipa ubingwa wa barani ulaya Chelsea na kuweka rekodi ya kocha wa muda mwenye mafanikio zaidi
Hili lilifuatiwa na Drogba kuvua shati lake na kulipeperusha juu ya kichwa chake kuonyesha furaha ya ushindi baada ya kukimbia kuzunguka uwanja mzima, huku Fernando Torres na David Luiz wakipanda juu ya besera la goli kuonyesha furaha yao. Wakati huo Mmiliki wa klabu hio Abramovich mwenyewe akiruka na kupiga makofi huku akiimba ikidhihirisha sura isiyoonekana kwa kawaida kwa mtu msiri asiyeonyesha hisia zake.


Drogba akishangilia baada ya kutupia kambani penati ya mwisho iliyoipa ubingwa Chelsea

Ikiwa mkwaju huo ulikua wa mwisho kwa mchezaji huyu kutoka Ivory Coast kama mchezaji wa Chelsea, pamoja na bao lake la kusawazisha lile la Thomas Mueller, basi Drogba ataondoka kwa kuweka rekodi yake binafsi.


Drogba akimiliki mpira katika fainali hiyo

Drogba mwenyewe hakuweza kuelezea bayana juu ya majaliwa yake baada ya kukabidhiwa zawadi ya mchezaji bora wa mechi hio ya fainali ya Ligi ya mabingwa barani Ulaya. Punde mkataba wake unafikia mwisho na bado hakuna matumaini ya kama ataongezewa mda.

Hatma ya Meneja wa mda Di Matteo bado haijabainika na mwenyewe alishindwa kusema ni nini alidokezewa na Abramovich walipokumbatiana kwenye ngazi kabla ya sherehe za kukabidhiwa Kombe kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 107 ya klabu hio.
Haikua kazi rahisi kwa Chelsea uwanjani mpira ulipochezwa katika sehemu ya uwanja ya Chelsea lakini hadi mwisho lakini waliepuka uwezekano mkubwa wa kufungwa zaidi ya mabao manne ila kutimiza ndoto ya Abramovich.



Mara pekee kwa klabu hii kushamiri katika mashindano ya Ulaya, ulikua mwaka 1971 kabla ya hata Liverpool kushinda nje ya England, Chelsea ilipoichapa Real Madrid na kujishindia Kombe la Mshindi la mwaka huo wa 1971.

Drogba, aliongoza na kua kinara, na hivyo kuandika jina lake kwa vitendo katika historia. Kipa Petr Cech amepitia kipindi kigumu wakati wa kampeni ya Ligi ya mabingwa wa Ulaya lakini mjini Munich alionyesha ukomavu kwa kuzuia mkwaju wa Arjen Robben katika kipindi cha ziada na wakati wa matuta alizuia mkwaju wa Ivica Olic.
Mwamko wa Chelsea ulianza pale alipotimuliwa Andre Villas Boas kufuatia kipigo cha 3-1 na Napoli na mrithi wake Di Matteo akageuka kua chachu ya ufanisi kwa kusababisha ushindi wa Kombe la FA na mechi kadhaa za Ligi kuu ya Premiership.


Matokeo ya Napoli yakageuka kuipendelea Chelsea na baada ya hapo kuichabanga Benfica kujishindia fursa ya kukutana na Barcelona ambayo waliweza kuishinda kwa hatua zote mbili,nyumbani na ugenini licha ya kusukumwa kwa dakika nyingi.


Sifa kubwa anastahili Roberto Di Matteo aliyechimba ndani ya bongo za wachezaji aliyewafahamu na kuamini kua wana uwezo wa kushiriki na kucheza soka kwa kiwango cha juu na kushinda.

Bila shaka wadadisi watakosoa mbinu zilizotumiwa dhidi ya Barcelona na huko Munich lakini jibu la Di Matteo ni moja tu angalia rekodi ya mwaka 2012, Mabingwa wa Ulaya ni Chelsea.

Uwanja wa Allianz Arena ambapo kipute cha fainali ya ligi ya mabingwa kilipigwa na Chelsea
kuibuka kidedea


MIPIGO YA PENATI

Friday, May 18, 2012

JEZI NAMBA 30 KUTOTUMIKA TENA SIMBA KATIKA KUMUENZI MAREHEMU PATRICK MUTESA MAFISANGO


Patrick Mutesa Mafisango akiwa na jezi namba 30

Habari za kuthibitika kutoka ndani ya klabu ya Simba ya Dar es salaam ambao ni mabingwa wa soka Tanzania bara 2012-2013 zinasema jezi namba 30 iliyokuwa ikitumiwa na kiungo mkabaji marehemu Patrick Mutes Mafisango imepigwa "STOP" kutumika au kuvaliwa na mchezaji mwingine katika hali ya kumuenzi mchezaji huyo wa kimataifa kutoka Rwanda.


Wachezaji wa Simba Uhuru Selemani na Yondani wakiwa katika majonzi hospitali ya muhimbili

Uhuru Suleiman ameshindwa kujizuia akimwaga chozi katika hospitali ya Taifa Muhimbili

Patrick Mutesa Mafisango alifariki siku ya alhamisi alfajiri saa 10:25 akitokea Muziki kuelekea nyumbani kwake keko. Ajali hiyo ilitokea maeneo ya Tazara jijini Dar es salaam kwa kile kilichosemekana marehemu alikuwa katika jitihada za kuokoa maisha ya muendesha pikipiki ndipo alipojaribu kumkwepa kwa kuwa gari ilikuwa katika mwendo kasi iliacha njia na kuingia mtaroni na kupinduka na kusababisha kifo cha mchezaji huyo papo hapo na wenzake aliokuwa nao kwenye gari kujeruhiwa.


Mashabiki wa Simba na wapenzi wa Mafisango wakiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili

Hii ndiyo gari aliyopata nayo ajali Patrick Mutesa Mafisango

Kifo cha Mafisango kimeacha majonzi sio tu kwa Mashabiki na wachezaji wa Simba bali watanzania wote wapenda michezo na Wanyarwanda wote ambapo walikuwa wakimtegemea kwenda kujiunga na timu yao ya Taifa kupeperusha bendera ya Rwanda katika mashindano ya kutafuta nafasi ya kucheza kombe la dunia.


Boniface Pawasa mchezaji wa zamani wa Simba ameshindwa kabisa kujizuia akitokwa na machozi mbele yake ni Uhuru Suleiman

Wasanii wa kundi la Wanaume kushoto Chege na wenzake wakiwa msibani nyumbani kwa Mafisango

Haruna Moshi "Boban" akiwa katika lindi la majonzi akimlilia Mafisango

Kitu cha kusikitisha na kuhuzunisha zaidi ni kwamba Patrick Mutesa Mafisango baada ya kuitwa kujiunga na kikosi cha timu ya soka ya Taifa ya Rwanda na kocha Micho, aliomba asogezewe siku kwani alikuwa ndio ametoka kushiriki mashindano ya kombe la shirikisho akiwa na timu yake ya Simba ya Dar es salaam. Alipokubaliwa Patrick Mutesa Mafisango alikuwa amepanga kuondoka Tanzania leo 18/5/2012 kwenda kujiunga na timu yake ya Taifa ya Amavubi lakini kwa masikitiko siku hiyohiyo aliyoipanga kwenda Rwanda kujiunga na Timu yake sasa anakwenda akiwa hana uhai tena...inasikitisha sana!! MUNGU AILAZE ROHO YA PATRICK MUTESA MAFISANGO MAHALA PEMA PEPONO..AMIN!

Thursday, May 17, 2012

DEDICATION TO ALL PATRICK MAFISANGO,RWANDESE & SIMBA SPORTS CLUB SUPPORTERS-CANDLE IN THE WIND (ELTON JOHN)

LIVERPOOL WAMTIMUA KENNY DAGLISH

Kocha aliyetimuliwa Liverpool Kenny Daglish

Kocha Mkuu wa Liverpool Kenny Dalglish ametimuliwa kuifundisha klabu hiyo.

Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo inasema uamuzi huo umefikiwa baada ya tathmini ya kina iliyofanywa.

"Baada ya kutathmini kwa makini klabu imefikia uamuzi na kuona mabadiliko ni ya muhimu" Imesema taarifa hiyo

"Matokeo ya ligi kuu ya Premia yametusikitisha na katika kulinda maendeleo yaliyopatikana ni lazima kufanya mabadiliko"


Dalglish kuondoka kwake kwenye klabu ''kumefanywa kwa utu na heshima kubwa''.

Kocha Mkuu wa Wigan Roberto Martinez na Kocha wa zamani wa Liverpool Rafael Benitez wanatajwa kuwa huenda wakachukua nafasi ya Dalglish.

Dalglish anaelezwa kutokuwa na matokeo mazuri katika ligi kuu ya England.

Kuondoka kwake kumekuja baada ya mazungumzo na wamiliki wa Klabu hiyo John Henry na Tom Werner mjini Boston,Marekani siku ya Jumatatu.

Zaidi ya Liverpool kufika fainali ya FA na kuchukua Kombe la Carling, timu hiyo imemaliza ligi kuu ya England ikiwa nafasi ya nane huku ikipoteza michezo mingi.


BREAKING NEWS...PATRICK "MUTESA" MAFISANGO AFARIKI DUNIA


Kiungo wa zamani wa Simba s.c Marehemu Patrick Mafisango"Mutesa"


Kiungo mashuhuri wa Simba sports club Patrick Mafisango amefariki ghafla katika ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Tazara amabapo ni kituo cha gari moshi linalounganisha nchi ya Tanzania na Zambia,wilaya ya Temeke jijini Dar es salaam.

Chanzo cha ajali hiyo ni kitendo cha Marehemu Mafisango akiwa katika gari yake na mdogo wake alipojaribu kumkwepa muendesha pikipiki na katika harakati za kuokoa maisha ya muendesha pikipiki huyo hatimae gari la Mafisango liliacha njia na kuingia kwenye mtaro na kupinduka na kusababisha kifo cha mchezaji huyo wa Simba, katika ajali hiyo pia mdogo wake Mafisango alijeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitalini.

"Kifo cha Patrick mafisango kimetusikitisha sana hasa kipindi hiki ambachio alikuwa katika kiwango cha juu sana ametuachia pengo wanasimba" Alisema mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage alipohojiwa na kituo kimoja cha radiop nchini Tanzania.

Patrick Mafisango enzi za uhai wake akilisakata kabumbu

Mafisango akiwa amebebwa juujuu na wachezaji wenzake wakishangilia ushindi enzi za uhai wake

Mafisango kulia enzi za uhai wake akishangilia goli pamoja na mwenzake Emmanuel Okwi

Mafisango wa tatu kushoto waliosimama akiwa na kikosi cha Simba enzi za uhai wake

Mafisango akiwa amejipumzisha baada ya mazoezi na timu yake ya Simba

Mafisango katika swaga za kitaa enzi za uhai wake