Maandamano na migomo ni haki za msingi kwa mwananchi yeyote yule ili mradi maandamano hayo au mgomo huo ufuate kanuni na taratibu na vyote hivyo vifanyike pasipo kukiuka au kuvunja sheria na kanuni za nchi. Sasa basi bila kujali kuwa maandamano au mgomo umefuata taratibu au la, nijuavyo mimi maandamano au migomo huwa ni katika kutafuta haki ambayo kwa namna moja au nyingine imenyimwa au imenyang'anywa iwe kwa bahati mbaya au kwa makusudi na ili ipatikane lazima kuwe na shinikizo la amani yaani maandamano au mgomo.
Hali imekuwa mbaya sana pindi migomo au maandamano yanapotokea iwe kwa kufuata taratibu au kwa kutifuata taratibu,waandamanaji huwa hawana nia ya kudhuru zaidi ya kutaka kusikilizwa, lakini cha kushangaza jeshi letu la polisi limeonesha udhaifu kwani mara kwa mara hupenda kutumia silaha za moto katika kukabiliana na waandamanaji kitu ambacho si sahihi kwasababu waandamanaji huwa hawana silaha sasa iweje polisi watumie silaha kukabiliana nao? Hili linanipa wasiwasi kwamba jeshi letu la polisi limekosa ubunifu na halina ujuzi wowote wa kukabiliana na waandamanaji na wanaona suluhisho ni kurusha silaha za moto ambazop matokeo yake zimekuwa zikiua na kujeruhi wananchi ambao kwa namna moja au nyingine huwa hawana makosa.
Wakati mwingine huwa inanipa hisia mbaya na kufikiria kuwa hawa askari wetu pindi zinapotokea purukushani basi wao huona hapo ndio pa kuonesha utaalamu wao wa kufyatua risasi kwa hali halisi askari anaweza akaanza kazi mpaka akastaafu bila kufyatua risasi zaidi ya kwenye mafunzo.
Ushauri wangu kwa jeshi letu ambalo ndilo lenye dhamana ya kusimamia usalama wetu na mali zetu wajipange upya katika kukabiliana na migomo au maandamano pasipo kudhuru wananchi kwani hili linaleta chuki kati ya jeshi la polisi na wananchi, siamini kuwa hakuna njia nyingine ya kukabiliana na waandamanaji,swali la kujiuliza je waandamanaji wangekuwa wanaandamana na silaha za moto hali ingekuwaje?
No comments:
Post a Comment