Friday, July 22, 2011

CHOMBO CHA ATLANTIS CHARUDI DUNIANI

Chombo cha mwisho cha angani cha Marekani leo kilirudi tena duniani, na kutua katika kituo cha vyombo vya angani cha Kennedy, muda mfupi kabla ya jua kuchomoza alfajiri.
Vyombo vya NASA vilitumiwa sana katika kuanzisha kituo cha angani, na vile vile darubini iliyojulikana kama Hubble.
"Chombo hasa kilibadilisha mtizamo wetu wa vile tunavyoiona dunia", alisema kamanda Chris Ferguson, mara tu baada ya chombo hicho kutua.
"Kuna hisia nyingi leo, lakini jambo moja ambalo kamwe halina ubishi ni kwamba Marekani haitaacha kuvinjari", alisema alipokuwa akizungumza na kituo cha kusimamia safari za angani.
Kurudi ardhini kwa Chombo hicho cha kihistoria ni kufuatia amri ya serikali ya Marekani, na hasa kutokana na gharama za juu katika kuvitunza vyombo hivyo vya angani.

Uamuzi huo unamaanisha kwamba nchi hiyo haina tena uwezo wa kuwatuma wataalamu wa anga katika sayari mbalimbali.

Chombo cha Atlantis baadaye kilifahamika kama "the final four", yaani nne za mwisho, na kuashiria nia ya Marekani ya kuialika sekta ya watu binafsi pengine kuvitumia vyombo hivyo kibiashara, na hasa katika kupanga safari za kuwapeleka abiria angani.
Lakini hayo hayatazamiwi kufanyika katika kipindi cha miaka mitatu hadi minne hivi.
Katika kipindi hicho, NASA itawategemea Warusi katika kuwafikishia wataalumu wao hadi kituo cha kimataifa cha angani, kinachojulikana kama International Space Station (ISS).
Licha ya kiza kilichokuwepo katika anga ya kituo cha vyombo vya angani cha Florida, umati mkubwa wa watu ulijitokeza katika kushuhudia chombo hicho cha Atlantis kikirudi duniani.
Watu wengine elfu mbili walikisubiri chombo hicho katika uwanja ambao kilitua, na hata katika kituo cha kukielekeza chombo huko Texas, watu wengi walionekana katika lango la kituo cha safari za anga cha Johnson.

No comments:

Post a Comment