Wednesday, August 3, 2011

29, OKTOBA 2011 NI SIMBA NA YANGA

29-OKTOBA-2011

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetangaza rasmi ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2011/2012 huku mechi ya Simba na Yanga ikitarajiwa kupigwa Oktoba 29 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Ratiba hiyo ilitangazwa jana na Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura ambaye alisema ligi hiyo itaanza Agosti 20, mwaka huu lakini Simba na Yanga zitaingia uwanjani Agosti 21.

Alisema kuwa mchezo wa kwanza wa ligi kwa Simba utakuwa dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, huku Yanga ikianza kwa kuvaana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga itakuwa Oktoba 29 kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam ambapo Yanga ndiyo itakuwa mwenyeji katika mchezo huo wa kwanza.


“Mchezo mwingine wa Simba na Yanga utakuwa Aprili Mosi mwakani, uwanja ambao mchezo huu utapigwa utajulikana baadaye kwa kuwa Uwanja wa Uhuru utakuwa tayari umekamilika, hivyo inawezekana mechi hiyo ikachezwa kwenye uwanja huo,” alisema Wambura.

Ratiba hiyo inaonyesha kuwa, mzunguko wa kwanza utamalizika Novemba 5, huku ligi hiyo ikitarajiwa kufikia tamati Aprili Mosi mwakani na hivyo Simba na Yanga zitakutana kwenye mchezo wa mwisho kabisa wa ligi.
Michezo ya ufunguzi katika ligi hiyo itakuwa ni kati ya Villa Squad na Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na Coastal dhidi ya Mtibwa kwenye Dimba la Mkwakwani, Tanga.

Katika michezo mingine, Kagera Sugar itavaana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Kaitaba, Polisi Dodoma itaanza na African Lyon kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma na Azam itapepetana na Moro United kwenye Dimba la Chamanzi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Kuna habari kuwa, timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes imealikwa nchini Botswana kushiriki michuano ya vijana ya Shirikisho la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa) itakayofanyika kuanzia Desemba Mosi hadi 10, mwaka huu.Huku ikibainishwa kuwa gharama zote ni za cosafa.

No comments:

Post a Comment