Kanali Muammar Gaddafi ameapa kupigana na waasi hadi kifo au ushindi, ripoti zimesema, baada ya waasi kudhibiti makazi yake mjini Tripoli.
Televisheni inayomuunga mkono Kanali Gaddafi, al-Urubah, imesema Kanali Gaddafi ambaye bado hajulikani alipo, ametoa hotuba akisema kuondoka kutoka kwa makazi yake kulikuwa ni ''mpango''.
Makazi hayo ndiyo yaliyokuwa maeneo ya mwisho chini ya udhibiti wa Kanali Gaddafi mjini Tripoli.
Waasi wamekuwa wakisheherekea mafanikio yao katika bustani ya Green Square, mjini Tripoli.
Sanamu ya Gaddafi yaharibiwa.
Waasi wakikanyaga sanamu ya Gaddafi
Picha za televisheni pia zimeonyesha wapiganaji wakivunja sanamu ya kiongozi huyo na kuipiga mateka baada ya kuuteka Bab al-Aziziya siku ya Jumanne. Waasi hao pia walichukua vifaa mbalimbali katika makazi hayo ya Kanali Gaddafi.
Hata hivyo bado mapambano yanaripotiwa katika mji huo, mkiwemo katika maeneo ya Abu Salim na Hadba na karibu na hoteli ya Rixos, ambapo waandishi wa kigeni wanapoishi.
Mwandishi wa BBC Rana Jawad mjini Tripoli amesema kuwa kuna hisia kuwa huu ndio mwisho wa utawala wa Kanali Gaddafi, lakini sherehe kamili hajitaanza hadi pale yeye na jamaa wake watakapo kamatwa.
Akizungumza na redio moja mjini Tripoli, Kanali Gaddafi ameahidi''kifo au ushindi'' katika mapigano dhidi ya majeshi ya NATO na waasi wa Libya, redio ya al-Urubah ilisema.
Kanali Gaddafi aidha amesema makazi yake yameharibiwa na mashambulio 64 ya angalini ya NATO.
Jumanne asubuhi, wapiganaji wa waasi waliokuwa wamejihami vilivyo walimiminika katika mji mkuu kushiriki katika mashambulio ya Bab al-Aziziya.
Baada ya saa tano ya mapigano makali, walivunja lango kuu na kuvamia makazi hayo.
Waasi walionekana wakiharibu masanamu, mkiwemo sanamu ya dhahabu, ya mkono unaovunja ndege ya kivita ya Marekani. Hema ya Kanali Gaddafi ambayo aliitumia kupokea wageni pia iliteketezwa.
Wametoroka kama panya.
''Tumeshinda makabiliano'' Abdul Hakim Belhaj, kamanda wa ngazi ya juu wa waasi mjini Tripoli aliliambia shirika la al-Jazeera.''Wametoroka kama panya''.Haijulikani iwapo kanali Gaddafi na jamaa wake walikuwa katika makazi hayo ya Bab al-Aziziya, lakini inaripotiwa kuwa ina mahandaki ya chini kwa chini, yanayounganisha na maeneo mengine ya mji.
Hali sio wazi katika katika mji wa Sirte, alikozaliwa Kanali Gaddafi, ambayo imekuwa ngome ya maafisa wanaomuunga mkono. Ripoti zinasema wanajeshi waliorudishwa nyuma wanaelekea huko.
No comments:
Post a Comment