Wapinzani wa jadi katika soka la Tanzania, timu za Simba na Yanga leo zitaingia katika vita nyingine pale zitakaposhuka dimbani kukabiliana katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mpambano huo unaoashiria ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu itakayoanza Jumamosi hii, unatarajiwa kuwa na upinzani mkali huku ukiwa unafanyika takribani siku 36 tu tangu timu hizo zilipokutana katika mechi ya fainali ya michuano ya Kombe la Kombe la Kagame katika mechi iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa na Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Ugumu wa mpambano huo unatokana na ukweli kwamba Simba itataka kulipiza kisasi baada ya kufungwa kwa penalti katika mechi ya msimu uliopita ya Ngao ya Jamii wakati Yanga ikitarajia kulinda heshima yake baada ya kufuta uteja wa kufungwa na mpinzani wake kwa takribani miaka nane mfululizo.
Maandalizi.
Timu zote zinaonekana kujiandaa kikamilifu kutokana na kucheza mechi kadhaa za kirafiki za kujipima nguvu na timu za ndani na nje ya nchi.
Wakati Yanga ilisafiri hadi nchini Sudan kucheza na mabingwa wa nchi hiyo timu ya El Hilal, Simba ilijichimbia visiwani Zanzibar kwa takribani wiki mbili, ambapo ilicheza na timu za Polisi Zanzibar na timu ya taifa ya vijana Zanzibar,Karume Boys kabla ya kuhamishia kambi jijini Arusha, ambapo ilialika timu za Victors ya Uganda na AFC Leopards ya Kenya na kucheza nazo mechi za kirafiki.
Makocha:
Kocha wa Yanga, Mganda Sam Timbe amesema ataendeleza rekodi yake kwa kuibuka na ushindi katika mchezo wa leo, ambapo pia aliahidi kuibuka na ushindi kila wakati timu hizo zitakapokutana ili awape raha mashabiki wa klabu yake.
Naye Moses Basena ambaye pia ni raia wa Uganda amewataka mashabiki wa klabu hiyo kutokuwa na wasiwasi akisema amefunga njia zote ambazo wapinzani wanaweza kuchoropoka ili kuepuka kipigo.
Vikosi:
Baadhi ya sura zilizokuwapo wakati wa michuano ya Kagame hazitarajiwi kuonekana dimbani leo kwa upande wa Simba, sura hizo ni pamoja na mshambuliaji Mussa Mgosi aliyeuzwa katika timu ya DC Motema Pembe ya DR Congo, Mohammed Idd Banka aliyesitishiwa mkataba pamoja pia Mwinyi Kazimoto na Ulimboka Mwakingwe ambao ni majeruhi wakati Yanga inatarajiwa kumkosa kiungo mkabaji Nurdin Bakari.
Wachezaji wanaotarajia kuanza kwa upande wa kikosi cha Simba ni pamoja na kipa Juma Kaseja, Said Nassoro' Chollo', Amir Maftah, Obadia Mangusa, Juma Nyosso, Jerry Santo, Uhuru Suleiman, Patrick Mafisango, Felix Sunzu, Haruna Moshi 'Boban' na Emmanuel Okwi.
Wakati kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuwa; Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua,Nadir Haroub 'Cannavaro',Chacha Marwa, Juma Seif kijiko, Godfrey Taita, Haruna Niyonzima, Kenneth Asamoah, Jerry Tegete na Kigi Makasi.
Waamuzi
Idd Mbaga, Israel Mjuni, Hamis Chang'waru.
Ulinzi:
Mkurugenzi wa Kampuni ya mafuta ya Big Bon waliyonunua mechi hiyo, Ahmed Baashwani mbali ya kusema watatumiachombo maalumu kuwabaini watu watakaoghushi tiketi, pia alisema vyombo vya usalama vitakuwa imara kudhibiti vurugu huku akiwataka mashabiki kukaa katika majukwaa kulingana na maelekezo ya tiketi zao.
No comments:
Post a Comment