Stars itacheza na Algeria 'Desert Warriors' Septemba 3 ikiwa ni mechi ya mchujo ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani Guinea ya Ikweta na Gabon huku kocha wa timu hiyo, Jan Poulsen akitarajiwa kuweka wazi kikosi chake Agosti 25.
Ofisa habari wa Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo, Jamali Zuberi aliiambia Mwananchi jana kuwa serikali imeamua kukubaliana na ombi la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutumia uwanja huo kwa kuwa ni suala la kitaifa.
"Mechi za Stars lazima zichezwe Taifa, pia Yanga na Simba wakikutana kwenye ligi kama wataomba kutumia uwanja huo tutawaruhusu kwa kuwa kuna maslahi, lakini mechi zao na timu nyingine kwenye ligi watumie viwanja vingine," alisema Zuberi.
Simba na Yanga kwenye Ligi zinakutana mapema mwezi Oktoba, mara ya mwisho zilikutana wiki iliyopita kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii na Yanga kulala mabao 2-0.
Zuberi alisema serikali imeamua kufunga uwanja huo kwa sasa kutokana na gharama za uendeshaji kuwa kubwa na uwanja huo hauwezi kumudu mikiki mikiki ya Ligi kwa kipindi chote kwani kwa kuruhusu hivyo utaharibika.
Serikali ilitangaza kuufunga uwanja huo mara baada ya mechi ya Simba na Yanga kutokana na uharibifu mkubwa uliotokea huku viti vingi vikiwa vimeharibiwa vibaya ikiwa ni pamoja na sehemu za vyoo.
No comments:
Post a Comment