Tuesday, August 2, 2011

WILSHERE KUIKOSA MECHI YA ENGLAND DHIDI YA UHOLANZI, THIERRY HENRY AKATALIWA KUICHEZEA ARSENAL.

Jack Wilshere inaonekana atakosa mechi ya kirafiki kati ya England na Uholanzi tarehe 10 mwezi wa Agosti, baada ya kuumia kifundo cha mguu wakati Arsenal ilipocheza mchezo wa kujipima nguvu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.

Jack Wilshere
Meneja wa Arsena, Arsene Wenger alilazimika kumtoa kiungo huyo kama tahadhari siku ya Jumapili walipocheza na New York Red Bulls kuwania Kombe la Emirates.
Wenger alisema hakuumia sana ila kifundo cha mguu wake kilivimba.
"Iwapo hataweza kucheza wiki ijayo, basi hataweza kucheza mechi dhidi ya Benfica, kwa hiyo kwa vyovyote hataichezea England," alisema Wenger.
Timu ya utabibu ya Gunners imetabiri hataweza kucheza kwa muda wa wiki moja, lakini Wenger amesema bado kuna nafasi anaweza kupona haraka na kucheza siku ya Jumamosi katika mechi ya mwisho ya maandalizi ya Ligi dhidi ya Benfica.
"Wameniambia huenda wiki ijayo atakuwa sawaswa," alisema. "Lakini kwa kawaida yeye huwa anapona haraka, ni kijana mkakamavu, kwa hiyo ninatumaini atapona haraka tofauti na madaktari walivyotabiri."
Meneja wa England Fabio Capello tayari atawakosa Steven Gerrard na Theo Walcott kwa ajili ya mchezo huo wa kimataifa kwenye uwanja wa Wembley.
Wakati huo huo mshambuliaji wa New York, Thierry Henry alikataliwa kuichezea Arsenal dakika tano za mwisho katika mechi hiyo ya Jumapili.
Alikubaliana na Wenger kwamba atabadilisha timu dakika tano kabla ya kumalizika mchezo huo wa kirafiki.
Lakini mwamuzi Kevin Friend alikataa kuruhusu hilo kwani kanuni za Fifa zinaeleza kwamba mchezaji haweza kuchezea timu zote mbili katika mchezo mmoja.

No comments:

Post a Comment