Friday, September 23, 2011

Bob Bradley amrithi Shehata timu ya taifa ya Misri

Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Marekani, Bob Bradley, Alhamisi ametangazwa kuwa sasa ni kocha mpya wa timu ya taifa ya Firauni ya Misri.
Mkataba wa Bradley utaendelea hadi fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil, kufanyika mwaka 2014.
Bob Bradley
Anachukua ukocha kutoka kwa Hassan Shehata aliyejiuzulu baada ya mfululizo wa matokeo ya kutoridhisha
Atakuwa akipokea mshahara wa dola za Marekani 40,000 kwa mwezi.
Kulikuwa na fununu kwamba Bradley alitazamiwa kuiongoza timu ya Misri ya Firauni, na aliweza kupata mkataba huo baada ya mashauri na chama cha soka cha Misri mjini Cairo.
Anatazamiwa kuitisha mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumamosi, ili kuelezea mipango yake, katika kuinyanyua timu hiyo ambayo imekuwa ikifanya vibaya hivi majuzi.
Misri imetwaa ushindi katika awamu tatu za fainali ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, lakini wakati huu imeshindwa kufuzu kushirikishwa katika fainali zijazo kufanyika katika mataifa ya Equatorial Guinea na Gabon mwaka 2012.
"Wachezaji wa Misri ni wazuri mno," alielezea mara tu baada ya kufika Cairo.
"Nchini Marekani tulijitahidi kuwaimarisha wachezaji katika nyanja zote; kiufundi, kimaarifa, miili yao pia, na nadhani ni muhimu kufanya hivyo."
Hisia za mashabiki na vyombo vya habari hazijajitokeza waziwazi kufuatia Bradley kutangazwa kama kocha mpya nchini Misri.
Bradley awali alitazamiwa kuwasili Misri siku ya Jumanne, lakini akacheleweshwa kutokana na matatizo katika kupata ndege.
Chama cha soka cha Misri (EFA), kilikuwa kimefikiria pia kumpa kazi hiyo kocha wa zamani wa Ghana, Milovan Rajevac, lakini hatimaye kikaamua kumwajiri Bradley.
Bradley anachukua wadhifa ulioachwa wazi na Hassan Shehata, ambaye aliamua kujiuzulu kutokana na mfululizo wa matokeo mabaya katika mechi za awali za kufuzu kushirikishwa katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2012.
Timu ya Firauni, licha ya kwamba hawana tena nafasi ya kufuzu kwa mashindano hayo, watakuwa ni wenyeji wa timu ya Niger, katika mechi yao ya mwisho ya kufuzu mwezi Oktoba.

No comments:

Post a Comment