Mmoja wa abiria aliyeokolewa katika ajali ya meli ya Mv Spice Islender, Shaame Faki Ally akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, mjini Unguja baada ya kunusurika kufa katika ajali hiyo iliyotokea katika eneo ya Nungwi, Zanzibar. Shaame amefiwa na ndugu zake 32 waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo. Picha na Jacson Odoyo
MAHARUSI watarajiwa, waliokuwa wakienda kufunga ndoa katika Kisiwa cha Pemba mjini Zanzibar, ni miongoni mwa watu ambao wanasadikiwa kuwa miili yao imenasa katika meli hiyo.Mpaka sasa miili ya watu 240 waliofariki katika ajali hiyo ya meli ya Spice Islender iliyotokea katika eneo la Nungwi, Unguja mwishoni mwa wiki iliyopita, wamepatikana na kuzikwa.Imeelezwa kuwa watarajiwa hao walikuwa wameongozana na watu 36 wa familia moja walitokea Vingunguti, Dar es Salaam kuelekea Pemba kuhudhuria sherehe ya maharusi hao.
Meli hiyo inakadiriwa kuwa ilikuwa na abiria wapatao 1,000 ingawa taarifa za mmiliki zinaonyesha kuwa ilikuwa na abiria 605 kwa mujibu wa tiketi zilizokatwa huku abiria waliookolewa wakiwa 601 na maiti zilizopatikana zikiwa 240.
Akizungumza jana katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Unguja mmoja wa manusura wa ajali hiyo, Shaame Faki Ally alisema walikuwa watu 36 kutoka familia moja.
Ally alisema safari yao ilianzia Dar es Salaam kuelekea Pemba kwenye harusi ya mdogo wao aliyemtaja kwa jina la Hadia Hassan na bwana harusi akimtaja kwa jina moja la Haji.
“Tulikuwa watu 36 wakubwa kwa watoto lakini walionusurika ni wanne tu, 32 wote wamefariki dunia katika ajali hiyo na kati ya watu waliofariki miili iliyoonekana ni saba waliobaki hawajaonekana mpaka sasa,” alisema Ally na kuongeza:
“Ingawa mimi ni mzima lakini mpaka hivi sasa sijui pakuanzia wala pa kutokea baada ya kutoka hospitali kwa sababu familia nzima imeteketea katika ajali hiyo.”
Ally ambaye ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho kuokelewa katika ajali hiyo alidai kuwa meli hiyo ilikuwa na watu wengi waliokuwa wametokea Dar es Salaam kuelekea Pemba.
“Meli ilikuwa imejaa na kumbuka wakati tunatoka Dar es Salaam tulikuwa watu wasiopungua 1,200 pamoja na mizigo na tulipofika Unguja ikapakia watu wengi hivyo kwa ujumla tulikuwa watu wasiopungua 2,000 ndani ya meli,” alidai.
Akizungumzia safari ya kutokea Unguja kuelekea Pemba kabla ya meli kuanza kuzama, Ally alisema: “Mimi nilikosa siti hivyo nikawa na kazi ya kuzunguka huku na kule na wakati mwingine nikishuka chini kwa ajali ya kuwanunulia maharusi vyakula na kila nilipokuwa nikipita niliwakanyaga watu au kuwaruka kutokana na umati mkubwa uliokuwa ndani ya meli.”
Alisema ilipofika majira ya saa sita usiku meli ikaanza kujaa maji, ghafla akawaona wafanyakazi wa meli pamoja na mabaharia wakizunguka na ndoo kwa ajili ya kuyachota, ndipo alipokimbia chini walipokuwa wenzake na kuwaeleza hali halisi.
Alisema kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya, alianza kuwaona mabaharia wakichukua majaketi na kuvaa kisha wakaanza kujitupa majini mmojammoja na wengine wakamfuata nahodha wa meli hiyo na kumtoa alipokuwa kisha wakamvisha jakati na kuondoka naye.
Alisema kuwa baada ya kuona tukio hilo, alianza kuwajulisha ndugu na jamaa kwa njia ya simu kuhusu tukio hilo.
Tulikusanyika wote tukasali
“Kwa kweli nilipoona hivyo nikajua sasa tumekwisha. Nikarudi tena chini nikakuta maji yameshajaa ndani ya meli ndipo tukakusanyika wanandugu wote tuliokuwa ndani ya meli pamoja na maharusi wetu tukaswali swala ya mwisho na kuambizana kuwa kila mtu ajiokoe mwenyewe na Mungu akipenda tutakutana popote pale iwe duniani ama peponi,” alisema Ally.
“Niliwakusanya watoto wote baada ya kuona wazazi wao wamechanganyikiwa na ukizingatia kwamba hawana uzoefu na masuala ya maji nikawapa godoro na kuwaambia kwamba walishikilie kwani ndilo itakalowaokoa.”
“Baada ya kuwapa watoto godoro, nikarudi kuwatafuta ndugu wengine lakini sikufanikiwa kuwaona tena ndipo nilipoamua kurudi juu kutafuta jaketi nikapata moja nikalivaa kisha nikarudi nilipowaacha watoto na kuungana nao. Wakati huo maji yalikuwa yameshajaa ndani ya meli."
“Kidogo nikaokota mbao ambayo baadaye ilinisaidia kuvunjia moja ya dirisha la meli hiyo kwani wakati huo hata mlango ulikuwa hauonekani nikawapitisha watoto pamoja na mimi mwenyewe nikapita.”
“Nilipofika nje ya meli, nikakuta watu wengi wanaelea na majaketi yao wengine wakiwa wameshafariki dunia, kwa sababu yale majaketi kama hujui kuogelea hayawezi kukusaidia, isipokuwa ukifa huwezi kuzama badala yake utakuwa ukielea juu ya maji. Kadri muda ulivyozidi niliona watoto wakizidiwa na kuishiwa nguvu na mwishoni wote wakafariki dunia mbele yangu.”
Muda wote akisimulia, Ally alikuwa akibubujikwa machozi... “Baada ya kuona ndugu zangu wote wameteketea, ndipo nilipoanza kujiokoa mwenyewe na ilipofika saa 5:00 asubuhi, nikaona helikopta ikipita nikaanza kupeperusha shati langu kila wakati mpaka waliponiona na kuja kuniokoa.”
“Walipofika wakashusha kamba nikajitahidi kujivisha kwa shida kwani wakati huo wote hakuna hata kiungo changu kimoja kilichokuwa kinafanya kazi mwili ulianza kuchanika kwa sababu ya chumvi na baridi kali.”
Miongoni mwa walionusika alikuwamo mtoto wa miaka sita akiwa na dada yake mwenye umri wa miaka 12. Mama mdogo wa mtoto huyo, Mariam Hemedi alisema Said anaendelea vizuri na dada yake amesharuhusiwa kutoka hospitali.
Pinda aongoza mawaziri kutoa pole
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alikutana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na kumpa pole kutokana na ajali hiyo.
Pinda akiwa amefuatana na baadhi ya mawaziri, akiwamo William Lukuvi na Mary Nagu alimpa pole Dk Shein pamoja na wananchi wote kutokana na tukio hilo na kuwataka wananchi kuendelea kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu cha msiba.
Nayo Kamati ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoshughulikia Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ikiongozwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa ilifika Zanzibar na kumpa mkono wa pole Dk Shein.
Lowassa akiwa na wajumbe wa kamati hiyo alimweleza Dk Shein kuwa wameupokea kwa masikitiko makubwa msiba huo na ndiyo wakaona kuwa kuna umuhimu wa kufika Unguja kutoa mkono wa pole kwa Rais pamoja na wananchi wote.
Dk Shein alisisitiza na kurejea kauli yake aliyoitoa kwa wananchi juzi baada ya tukio hilo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imeamua kuunda tume ya uchaguzi ili kujua chanzo cha tukio hilo na baada ya hapo taarifa rasmi itatolewa kwa wananchi pamoja na kufuatia taratibu za kisheria.
Alisema waliopatikana hadi jana mchana walikuwa 816, kati yao waliokuwa hai ni 619 na waliofariki dunia ni 197. Miongoni mwa waliofariki dunia, 39 walizikwa na Serikali na 158 walitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu na jamaa zao.
Dk Shein alisema juhudi kubwa zimefanywa na Kamati ya Maafa na kutoa shukurani kwa viongozi wote wa SMZ na Jamhuri ya Muungano ambao wameshiriki kikamilifu katika msiba huo akiwamo Rais Jakaya Kikwete.
Wajumbe wa Baraza la Wakilishi wamefanya kikao cha dharura kujadili maafa hayo na kutuma salamu maalumu kwa Rais huku wakisisitiza kuchukuliwa hatua kwa wale wote waliohusika na uzembe katika tukio hilo.
Mbowe ataka meli zisafiri mchana tu
Kiongozi wa Upinzani bungeni na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema Tanzania haina haja ya kuruhusu vyombo vya usafiri kufanya kazi hiyo usiku kwani haina uwezo wa kuwaokoa watu pindi ikitokea ajali.
Mbowe alisema hayo huko Nungwi alipokwenda kuviona na kuvipongeza vikosi ambavyo vilitumika kwa ajili ya uokoaji wa watu katika ajali hiyo.
“Usafiri wa usiku ufutwe mara moja kwa sababu hatuna uwezo wa kuwaokoa pakitokea ajali.”
Alitaka Serikali iwawajibishe wale wote waliohusika na uzembe wa aina yeyote ile katika ajali hiyo ikiwa ni pamoja na viongozi wa bandari.
“Hili na jambo la aibu kwa Tanzania miaka 15 iliyopita tulikwenda Afrika ya Kusini na kuomba Jeshi la uokozi na mwaka huu tena! Kwa nini hutuundi letu,” alisema Mbowe.
Mbowe alikabidhi Sh5milioni kwa ajili ya watu walioathirika na ajali hiyo.
Sheikh Mkuu atuma rambirambi
Sheikh Mkuu wa Tanzania, Issa Shaban Bin Simba ametuma salamu za rambirambi akisema Bakwata limepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya ajali hiyo mbaya ya meli.
"Kwa niaba ya Baraza na Waislamu wote kwa ujumla, namwomba Allah (S.W) awape moyo wa subira na uvumilivu, wafiwa na wewe Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, katika kipindi hiki kigumu. Aidha, nawaombea kwa Mwenyezi Mungu (S.W) majeruhi wote wapone haraka Inshallah,” ilisema taarifa yake iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana.
Wazamiaji wa 'Sauzi' watua
Wazamiaji 12 kutoka nchini Afrika ya Kusini, wamewasili Zanzibar usiku wa kuamkia jana kuungana na wazamiaji wengine wa vyombo vya ulinzi na usalama kuhakiki kama bado kuna miili iliyokwama kwenye meli hiyo.
Kamanda wa kikosi maalumu cha Afrika Kusini, Wiyn Combrein alisema tayari wameshafika katika meli ya Spice Islanders kujaribu kuiopoa meli hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Bandarini ya Malindi, alisema watakuwapo hapa kufanya kazi hiyo kwa muda wa wiki moja hadi mbili.
Alisema wameshapeleka vifaa vyao kwa kutumia meli ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), tayari kwa kuanza kazi hiyo leo asubuhi. Combrein alisema kupitia watalamu waliochunguza, meli hiyo iko chini umbali wa mita 400 hadi 517.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Aboud Mohammed alisema kuwa wazamiaji hao wamewasili wakiwa na zana za kisasa za uzamiaji na kwamba kazi ya kwanza itakayofanywa na timu hiyo ni kuhakikisha kuwa wanaifikia meli hiyo iliyozama umbali wa karibu nusu kilometa kwenye mkondo mkubwa wa maji na majabali.
Bado Serikali na wananchi wanaamini kuwa kuna miili ya watu waliokwama katika vyumba vya meli hiyo tangu ilipozama usiku wa Jumamosi, Septemba 10 mwaka huu ikiwa na idadi ya watu isiyojulikana.
Makundi ya wananchi wamekuwa wakitaja idadi ya ndugu na jamaa waliosafiri na Meli hiyo na ambao hawajapatikana wakiwa hai au miili yao kiasi cha kutia shaka kuwa huenda bado wamenasa ndani ya vyumba vya meli hiyo.
UN, balozi zatuma rambirambiKatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amemtumia salamu za rambirambi Rais Jakaya Kikwete kutokana na ajali hiyo.
Taarifa ya Katibu huyo iliyosambazwa jana na Ubalozi wa Tanzania ulioko New York, Marekani kwa vyombo vya habari, imeeleza kuwa Ban Ki Moon amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali hiyo.
"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali hiyo na ninawapa pole wananchi wa Tanzania," imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Amezitaka familia zilizoathirika katika tukio hilo kuwa na subira na kuendelea na kumtegemea Mungu katika kipindi hiki kigumu... “Nawatakia kila la kheri na nafuu ya haraka majeruhi wote walionusurika katika ajali hiyo," amesema.
Wakati huo huo Ubalozi wa Tanzania, Abudhabi na Consulate ya Tanzania, Dubai UAE wametuma rambirambi kutokana na ajali hiyo.
Taarifa ya Balozi Mohamed Maharage Juma kwa niaba ya wafanyakazi wenzake iliyotumwa kwa Dk Shein, SMZ na wananchi wote wa Zanzibar imesema imeshtushwa na msiba huo mzito uliotokea.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Japan, Salome Sijaona kwa niaba ya wafanyakazi wa ubalozi ametuma salamu za rambirambi kwa Dk Shein na kusema wanawapa pole wale wote waliopoteza ndugu zao katika ajali hiyo na kuwaombea kupona haraka kwa wale walionusurika.
No comments:
Post a Comment