Monday, September 26, 2011
SIMBA JUU KWA JUU YATAFUNA MIWA YA MTIBWA, KAGERA SUGAR YATOA DOZI KWA POLISI
Uhuru Selemani akichanja mbuga
MSHAMBULIAJI Emmanuel Okwi alitia kambani bao pekee na kuipaisha Simba kileleni mwa Ligi Kuu katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, pia Kagera Sugar imepata ushindi wake wa kwanza msimu huu baada ya kuilaza Polisi Dodoma mabao 2-0.
Simba ambao walishuka kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare mara mbili Kanda ya Ziwa iliwachukua dakika 35 kabla ya mashabiki wake kufurahi baada ya Okwi kupokea vizuri pasi ya Uhuru Seleman na kufunga bao hilo kwa shuti kali ambalo limeiwezesha Simba kufikisha pointi 18.
Pamoja na ushindi huo wa bao 1-0 ilioupata Simba, beki wa timu hiyo Victor Costa alikosa mkwaju wa penalti katika dakika ya 90 baada ya mkwaju wake kupanguliwa na kipa wa Mtibwa Sugar, Deogratius Munishi"Dida"
Mabingwa wa mwaka 2000, Mtibwa Sugar walianza mechi kwa kishindo kupitia Masoud Ally aliyepokea pasi ya Thomas Maurice na kupiga shuti kali la umbali wa mita 25, lililopanguliwa na kipa wa Simba, Juma Kaseja.
Simba walijibu mapigo katika dakika ya nane kupitia kwa Uhuru Seleman aliyetokea winga ya kushoto na kutoa pasi kwa Emmanuel Okwi aliyepiga shuti lililopaa juu.
Mtibwa waliendelea kupeleka mashambulizi katika lango la Simba, ambapo walipata faulo ambayo ilipigwa na Masou Ally katika dakika ya11 na mpira uligonga mwamba na mabeki wa Simba waliokoa mpira huo na kuwa kona.
Pia Simba na wenyewe waliendelea kulishambulia lango la Mtibwa ila katika dakika ya 13 Okwi alishindwa kutumia vizuri pasi ya Jerry Santo kufunga bao.
Mechi hiyo pia ilisimama kwa dakika kadhaa baada ya kiungo Zuberi Katwila wa Mtibwa kugongana na Victor Costa wakati wakiwania mpira wa juu na wote wawili walitolewa nje kwa ajili matatibu, lakini walitibiwa na kurudi kuendelea na mchezo.
Lakini hali ya Katwila ilionekana siyo nzuri kwani alikuwa akichechea na aliomba kutoka hivyo kocha wa Mtibwa Sugar, Tom Olaba alilazimika kumtoa Katwila katika dakika ya 22 na kumwingiza Awadhi Juma.
Chipukizi Shomari Kapombe wa Simba katika mechi hiyo alikosa bao dakika ya 28 baada ya shuti lake kumgonga beki wa Mtibwa na kuwa kona ambayo haikuleta madhara.
Kapombe pia alitengeneza pasi nzuri kwa Uhuru aliyemchungulia Okwi ambaye aliutumia vizuri udhaifu wa nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Salum Sued aliyeoneka kushindwa kwenda na kasi ya mchezo kufunga bao la Simba katika dakika ya 35.
Mtibwa walirudi kwa kasi katika kipindi cha pili, ambapo katika dakika ya 47, nusura wasawazishe baada ya krosi ya kiungo Shabaan Nditi kutua kichwani mwa Maurice ambaye alipiga nje.
Katika dakika ya 90, Simba walipata penalti baada ya Haruna Moshi kuangushwa kwenye eneo la hatari na mwamuzi David Paulo kutoka Mtwara kuamuru adhabu hiyo.
Beki wa Simba, Costa alishindwa kutoa zawadi ya bao kwa mtoto wake watatu wa kiume aliyezaliwa juzi baada ya mkwaju wake wa penalti kupanguliwa na kipa wa Mtibwa Sugar, Munishi katika dakika ya 90.
Kocha Olaba wa Mtibwa katika mechi hiyo alimtoa Ally Mohamed na kumwingiza Hussen Javu wakati, Moses Basena wa Simba aliwatoa Uhuru Selemani ,Amri Kiemba na Gervais Kago na kuwaingiza Ulimboka Mwakingwe, Shija Mkina na Haruna Moshi.
Akizungumza baada ya mechi hiyo kumalizika kocha wa Mtibwa, Olaba alisema wachezaji wake hawakucheza vizuri katika kipindi cha kwanza, lakini walibadilika dakika 45 za mwisho.
"Viungo walikosa maelewano katika kipindi cha kwanza, lakini tuliporudi mapumziko walibadilika na kufanya vile tulivyotaka."
KAGERA: Wenyeji Kagera Sugar baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Oljoro katikati ya wiki walibadilika jana na kuichakaza Polisi Dodoma mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Washambuliaji Hussein Sued na Said Dilunga walitia kambani mabao mawili katika kipindi cha kwanza na kurudisha imani ya wanakagera kwa timu yao ambayo imepata ushindi huo kwa mara ya kwanza.
Sued alifunga bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti dakika ya kumi baada ya Dilunga kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki wa Polisi, Frank Sindato na mwamuzi Amon Paul kutoka mkoani Mara kuamuru penalti.
Wakati maafande hao waliokuwa chini ya kocha msaidizi wakijiuliza nini kinatokea Sued alipitisha krosi nzuri iliyomkuta Dilunga aliyesukuma mpira wavuni na kuwainua mashabiki wa Kagera Sugar waliojitokeza kwenye uwanja huo.
Kagera Sugar iliwapumzisha Malegesi Mwanga, Sunday Frank, Sued na kumwingiza Khamis Ally na Temmy Felix, Ibrahim Mamba, Katika mechi hiyo Polisi iliwapumzisha Raygan Mbuta na Delta Nyamancheja na nafasi zao kuchukuliwa na Ibrahim Masawe na Haruna Hassan.
Pia katika mchezo huo wenyeji walioneka kucheza kwa kujiamini na kuelewana tofauti na ilivyokuwa walipocheza dhidi ya Oljoro.
Ligi hiyo inaendelea leo kwa Azam wanaoshika nafasi ya pili kuwavaa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi, wakati Chamazi, JKT Ruvu watakuwa na kibarua kizito mbele ya Villa Squad huku jijini Mwanza Toto African watakuwa wenyeji wa Oljoro JKT kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Katika hatua nyingine Shirikisho la soka Tanzania limetangaza viingilio vya mchezo kati ya Yanga na Coastal Union kuwa ni sh 3,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa VIP C ni sh 7,000, VIP B ni sh 10,000 na VIP A itakuwa sh. 15,000.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment