Monday, October 31, 2011
MB DOGG AFUNGUA STUDIO
MB DOGG
Mwanamuziki wa muziki wa bongo fleva aliyetamba vilivyo katika mwa miaka ya 2000 Mb Dogg alitamba na vibao kama Mapenzi Kitu Gani, Si Uliniambia, Latifa, Naona Raha na nyinginezo. Hivi ni baadhi ya vibao ambavyo viliweza kumweka juu msanii huyu Afrika Mashariki.
Ni wazi kuwa wasanii wote wanaoimba hivi sasa ni chimbuko la Mb Dogg japokuwa hili wengi hawalifahamu, au kutokana na kutojua chimbuko la muziki huu wa kuimba ambao nao ni miongoni mwa muziki wa bongo fleva.
Awali wasanii wengi wa Tanzania walikuwa wakiimba hiphop zaidi na kurap kuliko kuimba muziki ulioonekana hauna soko.
Mb Dogg ambaye hufanya misafara ya kibiashara mara kwa mara huko Pretoria nchini Afrika Kusini ameweka bayana mpango wake alionao hivi sasa katika kuuendelea muziki wa kizazi kipya, ikiwa ni pamoja na kufungua studio ya kisasa.
Yafuatayo ni mahojiano ya mwanamuziki huyo alipofika katika ofisi za gazeti moja la habari hapa nchini la Mwananchi, msanii huyu aliweka bayana maisha yake kwa sasa, muziki, matukio mbalimbali na nini anatarajia kufanya baada ya kukaa kimya kwa miaka mitatu sasa.
Swali: Mbona umekaa muda mrefu pasipo kutoa wimbo wowote?
Jibu: Niliamua kupumzika, tangu nilipotoa kibao cha Natamani na baadaye Sagablasha niliamua kukaa kimya kwa muda nifanye mambo mengine kwanza, maisha sio muziki peke yake, ukiamua kufanya mambo mengine unaendelea pia.
Swali: Mashabiki wamjue vipi Mb Dogg wa sasa?
Jibu: Si kama wa zamani, hivi sasa anaitwa mwalimu wa wasanii, najivunia kwani ni kundi kubwa la wasanii waliopo juu hivi sasa, wamepita katika mgongo wangu ule ule ambao niliuanzisha mimi, namaanisha muziki wa kuimba.
Swali: Inakuwaje kuhusu Tip Top Connection unadhani baada ya kuondoka huko ndio sababu ya wewe kushuka kimuziki?
Jibu: Sijashuka kimuziki, ila niliamua kukaa kimya kwa muda nifanye mambo mengine kwanza, kuondoka Tip Top si sababu kuu ya mimi kushuka kuna sababu nyingine nyingi tu ambazo zinamfanya msanii kukata tamaa.
Swali: Nini sababu nyingine zilizokukatisha tamaa?
Jibu: Msanii unaweza kufanya kazi na wakubwa wako wasiithamini nguvu yako na hivyo unakata tamaa, ni mambo mengi sana yaliyotokea ambayo kiukweli nilishayaongea sana na sipendi kuyarudia kwani, Tip Top Connection hivi sasa ni watu wangu wa karibu ila sitaweza kufanya nao kazi na sitarajii.
Swali: Unadhani sababu ya wewe kutoka katika kundi inaweza kuwa sababu nyingine ya kukosa muda wa hewani katika redio za FM?
Jibu: Swali gumu sana hilo, na halijibiki ingawa nadhani inaweza kuwa sababu ya mimi kukata tamaa japokuwa sina uhakika na hilo kwamba ndio sababu ya kazi zangu kutochezwa.
Swali: Nini unafanya kwa sasa ili kuuendeleza muziki huu wa kizazi kipya?
Jibu: Safari yangu ya mwisho nikitokea Afrika Kusini ilikuwa ni kwenda kuchukua vifaa vya kuikamilisha studio yangu ya kisasa iliyopo maeneo ya Ubungo Makuburi itayoitwa Makopa Record, itakayorekodi audio na video. Imeshakamilika na muda wowote itaanza kazi, nimefanya hivi ikiwa ni mchango wangu wa kuendeleza muziki huu. Hata hivyo ninaendelea na muziki na nimeshafanya kazi kadhaa nikiwa na P Funk Majani pamoja na Man Walter na ninataraji kuziachia hivi karibuni.
Swali: Wiki hii vyombo vya habari vimeripoti kuwa ulipigwa risasi nchini Afrika Kusini je kuna ukweli wowote?
Jibu: Ninashangaa kisa hicho hakinihusu kabisa, yaani mama yangu alipatwa na presha baada ya kusikia habari hizo kwani alikua mbali na mimi kwa wakati huo, nimesikitika kwani ni vema wangenitafuta mimi mwenyewe ili wahakikishe taarifa hizo kuliko kuzianika hadharani pasipo utafiti wowote.
Swali: Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, inasemekana kuwa ulikuwepo eneo la tukio na ni wapi makazi yako kwa sasa kati ya Tanzania na Afrika Kusini?
Jibu: Nilikuwepo eneo la tukio, lakini sijahusika watu hao walikuja kumtafuta mtu wao na kumpiga risasi, ni Mtanzania ambaye amefariki siku chache zilizopita. Ila tukio hilo lilitokea Septemba 28, nikiwa Afrika Kusini. Kwa sasa makazi yangu ni Tanzania lakini hufika mara kwa mara nchini huko kibiashara zaidi.
Swali: Suala la kutangazwa kuwa umemiminiwa risasi nchini humo unadhani limekuathiri kwa namna moja ama nyingine.
Jibu: Limeniathiri tena kwa kiasi kikubwa, kwani hivi sasa wengi wanadhani ninajihusisha na vitendo vya kiharifu ndio maana nimepatwa na maswahibu hayo, kitu ambacho si kweli.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment