Ushindi wa magoli 4-0 dhidi ya Africa Lyon wiki iliyopita, ulikuwa wa kwanza mkubwa msimu huu kwa Wekundu hao wa Msimbazi.
Basena anaamini kuwa kasi ya kufunga walioonyesha washambuliaji wake baada ya kuwapa maelekezo, leo itapata mwendelezo kama ilivyokuwa kwenye mechi dhidi ya Lyon.
Kocha wa Ruvu Shooting, Charles Mkwasa naye amejipanga kuhakikisha timu yake inaitibulia Simba kwa kupanga jeshi la uhakika likiongozwa na wapachika mabao wake wake, Abdalah Juma, Revocatus Maliwa na Yusuph Mgwao kwa lengo ya kusaka mabao ya mapema.
Kwa upande wao Simba itaendelea kuwategemea washambuliaji wake Gervais Kago, Felix Sunzu na Emmanuel Okwi watakaolishwa mipira na viungo Uhuru Selemani na Haruna Moshi 'Boban'.
Timu hizo zitashuka dimbani zikiwa zinatofautiana kwa pointi 10, kwani Simba inayoongoza ligi imejikusanyia pointi 21 mpaka sasa ikiwa imecheza michezo tisa wakati Ruvu Shooting inakamata nafasi ya saba ikiwa imejikusanyia pointi 11 huku ikiwa imeteremka dimbani mara tisa.
Simba ambayo ilirejea kwa kishindo katika uongozi wa ligi, ni dhahiri italazimika kufanya kazi ya ziada ili iweze kuibuka na ushindi hasa ukizingatia itaikabili Ruvu Shooting inayotumia mfumo wa soka la kasi na nguvu.
Akizungumzia pambano hilo, Basena alisema,"Kwanza kabisa tunatarajia kupata upinzani mkubwa ukizingatia sisi ndio tunaongoza ligi."
"Zaidi ya hapo nimewaambia wachezaji wangu wasahau matokeo ya ushindi wa mabao manne tuliyoyapata katika mechi yetu ya mwisho, wajue wana kazi ya kufanya ili tuendelee kushikilia nafasi tuliyopo, kwa mantiki hiyo nina imani tutashinda,"alisema Basena.
Naye Mkwasa alisema kuwa hawatarajii kupoteza mechi hiyo kwa mara nyingine na kuongeza kuwa vipigo walivyovipata msimu uliopita vinatosha na sasa ni zamu yao kutoa kipigo.
"Nimewaambia vijana wangu kwa nini kila siku watufunge?, ina maana hatujui mapungufu yetu au ni uzembe tu!, Simba ni timu nzuri sawa, lakini na sisi ni lazima tuonyeshe ni bora zaidi yao, vinginevyo itakuwa aibu,"alisema Mkwasa ambaye pia ni kocha wa timu ya soka ya wanawake, Twiga Stars.
Katika hatua nyingine Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo huo kuwa ni Sh 10,000 kwa jukwaa la viti maalumu (VIP) na Sh 5,000 kwa jukwaa la mzunguko.
BAADHI YA MECHI ZAWAHISHWA KUPISHA MECHI YA STARS NA CHADTaifa Stars inatarajia kuingia kambini Novemba 3 mwaka huu kujiandaa kwa mechi ya kwanza ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Chad itakayofanyika Novemba 11 mwaka huu jijini N’Djamena.
Ili kutoa fursa kwa wachezaji watakaoitwa Stars kuripoti kambini ndani ya muda uliopangwa, mechi za mwisho kumaliza mzunguko wa kwanza Ligi Kuu ya Vodacom zimefanyiwa marekebisho. Mechi hizo sasa zitachezwa Novemba 2 mwaka huu badala ya tarehe ya awali ya Novemba 5 mwaka huu.
Mechi hizo ni Oljoro vs Villa Squad (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid), Moro United vs Simba (Uwanja wa Taifa), Polisi Dodoma vs Yanga (Uwanja wa Jamhuri), Toto Africans v Azam (Uwanja wa CCM Kirumba), Kagera Sugar vs Coastal Union (Uwanja wa Kaitaba), Mtibwa Sugar vs African Lyon (Uwanja wa Manungu) na Ruvu Shooting vs JKT Ruvu (Uwanja wa Mlandizi).
No comments:
Post a Comment