Bingwa zamani wa ndondi za uzito wa juu duniani Joe Frazier amefariki baada ya kuugua saratani ya ini.
Kulingana na familia yake, Frazier - anayejulikana pia kwa jina la Smokin' Joe - aligunduliwa anaugua saratani wiki kadha zilizopita na alikuwa anapokea matibabu.
Frazier mwenye umri wa miaka 67 alishikilia mkanda wa ubingwa wa dunia miaka kati ya 1970 na 1973.Alikuwa ndiye mtu wa kwanza kumchapa Muhammad Ali mwaka 1971. Baadae akachapwa na Ali katika mapambano mawili yaliyofuatia.
Meneja wake Leslie Wolf amesema Frazier aligunduliwa na maradhi ya saratani ya ini mwezi uliopita na alikuwa anatibiwa katika nyumba maalum inayotunza wagonjwa mahututi huko Philadelphia.
Hapo jumamosi, Bw Wolf alisema hali yake haikuwa nzuri lakini madaktari wak walikuwa wanafanya kila juhudi kumsaidia.
Frazier alishinda taji la ubingwa wa dunia kwa uzito wa juu mwaka 1970 baada ya kumtwanga Jimmy Ellis mjini New York.
Aliendelea kushikilia taji hilo hadi mwaka 1973, ambapo alipigwa na George Foreman.
Lakini mwanamasumbwi huyo huenda anafahamika zaidi kwa mapambano makubwa na Ali, likiwemo lile la kukata na shoka la Phillipines lililopewa jina la Thriller in Manila mwaka 1975.
No comments:
Post a Comment