Tuesday, November 1, 2011
SHIRIKA LA NDEGE TANZANIA(ATCL) LAFUFUKA SAFARI ZAANZA LEO
Ndege ya shirika la ndege TANZANIA (ATCL)
SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATCL), leo linatarajia kuanza safari zake mikoa ya Tabora na Kigoma.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Paul Chizi, alisema ndege hiyo itakuwa ikienda moja kwa moja kwenye mikoa hiyo na safari hizo zitakuwa za kila siku.
“Matayarisho yote yamekamilika na ndege tunatarajia itaanza safari zake kama kawaida kuanzia kesho (leo) Novemba Mosi... tunaomba Watanzania watoe ushirikiano kwa shirika lao kwa kuchagua kusafiri na ATCL, maana ni usafiri wa moja kwa moja wa uhakika na salama,” alisema Chizi.
Chizi alisema Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), tayari imelipatia shirika cheti cha kuruka kiitwacho Air Operators Certificate (AOC) baada ya kuridhishwa jinsi lilivyotekeleza masharti yake.
Hivi karibuni shirika hilo lilizindua mpango wa biashara (Business Plan) ambao unaeleza jinsi lilivyojizatiti kuhakikisha linamudu ushindani wa usafiri wa anga kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mpango huo ulizinduliwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Athumani Mfutakamba, ambaye alisifu hatua ya shirika hilo kwa mpango huo endelevu, kupata AOC na kulitakia mafanikio mema.
“Nawapongeza kwa kupata cheti cha kuruka, hii ni fursa kubwa kwa Watanzania kuanza kupata huduma za uhakika za shirika lao, naamini mambo yatakwenda vizuri nawatakia mafanikio mema katika mipango yenu mipya,” alisema Dk Mfutakamba.
Serikali katika mwaka wa fedha uliopita ilitenga Sh16.7 bilioni kwa ajili ya kuliwezesha shirika hilo na imeahidi kuendelea kulipa mishahara ya wafanyakazi wa ATCL.
Hata hivyo, katika hali ya kusikitisha wakati shirika linaanza safari zake tena, hakuna hata senti kati ya fedha hizo iliyowekwa kwenye akaunti za ATCL.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment