Wednesday, November 9, 2011

Taifa Stars kuelekea Chad leo,serikali yaipatia milioni 10


Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, inaondoka leo kuelekea nchini Chad, huku serikali ikitoa kiasi cha sh10 milioni kama hamasa ya ushindi katika mechi ya kuwania kufuzu kucheza hatua ya makundi tayari kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil.
Awali safari ya Stars ilikuwa ifanyike jana, lakini ilikwama kutokana na kuchelewa kupatikana kwa viza kuingia nchini Chad, na sasa itapaa mchana huu kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi fedha hizo juzi usiku kwenye hoteli ya New Africa, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema fedha hizo ni motisha kwa wachezaji ili waweze kufanya vizuri.
"Naamini wengi mnafahamu timu yetu ina mtihani mkubwa wa kucheza na Chad Ijumaa wiki hii, na marudiano Novemba 15. Nimeona na mimi nitoe motisha kwa wachezaji ili wafanye vizuri," alisema Pinda.
"Naomba makampuni, taasisi, watu binafsi, na mashirika mbalimbali waisapoti timu yetu kwa hali na mali kwa wale wote wanaitakia heri Tannzania.
"Nimempa jukumu Waziri mwenye dhamana ya michezo Emmanuel Nchimbi kuhakikisha michango yote inapita kwake na inawafikia walengwa," alisisitiza.
Kocha wa Stars Jan Poulsen alisema wanakwenda kupambana kiume kwenye mchezo huo na kuwataka Watanzania kuwaunga mkono.

"Tumefanya maandalizi mazuri, sijaona mapungufu. Kwenye ushindani kuna kushinda, kushindwa au kwenda sare. Tumejiandaa kushinda mechi hii," alisema Poulsen.Naye Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodgar Tenga alimshukuru Waziri mkuu kwa kutoa mchango huo na kuahidi kuwapa wachezaji fedha hizo ikiwa ni motisha kwao.
Wakati huo huo, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bonifas Wambura, amesema jana kuwa msafara wa Stars utakuwa na watu 40 na utaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo Eliud Mvella.
Pia wamo wajumbe wawili wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na baadhi ya mashabiki wa soka.
Msafara huo unatarajia kuwasili mjini N’Djamena, mji mkuu wa Chad leo saa 1.15 usiku saa za huko, sawa na saa 3.15 kwa muda wa nyumbani.

No comments:

Post a Comment