Uhuru Selemani wa Simba akifanya vitu vyake
JKT Oljoro jana walishindwa kwenda sambamba na kasi ya Simba waliocheza pungufu sehemu kubwa ya mchezo na kukubali kipigo cha mabao 2-0, shukrani kwa mabao ya kipindi cha pili ya mshambualiaji, Emmanuel Okwi yaliyoihakikishia Wekundu hao wa Msimbazi pointi zote tatu.
Katika mechi hiyo iliyochangamshwa na ushindani mkubwa toka timu zote mbili kwenye Uwanja wa Taifa, ilishuhudia kiungo wa Simba Haruna Moshi 'Boban' akionyeshwa kadi nyekundu isiyo na onyo baada ya kumrushia teke la makusudi mchezaji wa Oljoro, Omary Mtaki dakika ya 42.
Mwamuzi Isiaka Shirikisho wa Tanga, ambaye alionekana kushindwa kwenda sawa na kasi ya mchezo, pia aliwalima kadi za njano Omary Khasim wa JKT kwa kumchezea vibaya Haruna Moshi, kisha Kelvin Yondani na Jonas Gerald wa Simba kwa kuwachezea vibaya Kalege Mgunda na Nyambele.
Ushindi huo umeifanya Simba kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo kwa kufikisha pointi 34, tatu mbele ya mahasimu wao Yanga watakaoshuka dimbani mwishoni mwa wiki hii.
Katika mechi hiyo ambayo Simba walitumia zaidi viungo kufanya mashambulizi, JKT Oljoro waliofungwa 2-0 mzunguko wa kwanza, itabidi wajilaumu kwa kushindwa kutumia ya fursa ya wapinzani wao kucheza pungufu kupata ushindi.
Kocha wa Oljoro, Ally Kidy mara baada ya mchezo alikiri kuzidiwa na Simba, lakini akawalaumu wachezaji wake kushindwa kutumia vizuri nafasi nyingi za kufunga walizopata na pia kutumia mwanya wa Simba kucheza pungufu.
Simba walitawala dakika 20 za mwanzo wa mchezo na kukosa mabao kadhaa, huku Oljoro wakirejea mchezo dakika 10 za mwisho za kipindi hicho baada ya awali kufunikwa sehemu ya kiungo.
Mabadiliko yaliyofanywa na Simba kumtoa Gervais Kago na kuingia mshambualiaji wa kimataifa kutoka Uganda, Okwi katika kipindi cha pili ndiyo yaliyoipa ushindi timu hiyo.
Okwi, ambaye pengo la kutokuwapo kwake katika mchezo wa kwanza lilionekana wazi, alitumia dakika 15 tangu aingie uwanjani kuipeleka Simba mbele kwa bao zuri akimalizia pasi ya Uhuru Selemani.
Dakika nne baada ya bao hilo, Oljoro walikuja juu na kufanya shambulizi la nguvu ambalo nusura lizae bao la kusawazisha kufuatia piga nikupige kabla ya mabeki wa Simba kuokoa hatari.
Mchezaji Bakari Kigodeko wa Oljoro hatasahau nafasi ya wazi kufunga akiwa amebaki na nyavu na kisha kupiga mpira nje katika dakika ya 71.
Walikuwa Simba waliotawala mchezo bila kuonekana kama walikuwa pungufu uwanjani na kujipatia bao la pili dakika saba kabla ya filimbi ya mwisho baada ya Okwi kuinasa pasi ya Mafisango na kufunga bao hilo.
Kocha wa Simba Cirkovic Milovan aliwapongeza wachezaji wake kwa kuonyesha mchezo mzuri na kushinda mchezo huo pamoja na kwamba walicheza pungufu. "Matokeo mazuri kwetu, ni ishara ya kuwa tayari kwa ajili ya mechi dhidi ya Kiyovu ya Rwanda," alisema.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyopigwa Mbagala, nje kidogo ya jiji kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi kati ya African Lyon iliichapa Polisi Dodoma mabao 2-0.Mechi hiyo ilishuhudia timu zote zikishambuliana kwa zamu kipindi cha kwanza, huku Lyon wakionekana kufika zaidi langoni mwa wapinzani wao.
Wakicheza kwa kushambuliana, Semy Kessy aliifungia Lyon bao la kwanza dakika ya 30 kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Polisi, Gerald Mwingira baada ya awali kuwalamba chenga mabeki wa timu hiyo.Lyon walijihakikishia pointi tatu ushindi kwa kufunga bao la pili kupitia Sunday Juma baada ya kushirikiana vizuri na Samuel Ngasa katika dakika ya 76.
No comments:
Post a Comment