Tuesday, March 6, 2012

LIGI YA MABINGWA ULAYA ARSENAL KUPENYA KWENYE TUNDU LA SINDANO LEO?


AC Milan na Barcelona zina dalili kubwa ya kusonga mbele katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki hii, huku Zenit St Petersburg na Olympique Lyon zikiwa mashakani na zitajaribu kutetea ushindi mwembamba zilizopata katika mechi za awali.
AC Milan ambayo bado inasaka ubingwa wa Serie A, Kombe la Italia na Ligi ya Mabingwa Ulaya, inakwenda kuitembelea Arsenal katika Uwanja wa Emirates leo Jumanne ikiwa na akiba ya mabao 4-0 iliyoyafunga katika mechi ya kwanza ya hatua ya 16 bora.
Nao mabingwa watetezi, Barcelona, walishinda mabao 3-1 dhidi ya Bayer Leverkusen na hawana wasiwasi mkubwa kwa kuwa watawakaribisha wapinzani wao katika uwanja wa nyumbani.  

Kikosi cha AC Milan

Kikosi cha Arsenal

Huenda kukawa na stori tofauti leo Jumanne kwa kuwa Zenit ilishinda mabao 3-2 dhidi ya Benfica na huenda kibao kikageuka.
Vile vile Olympique Lyon ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 katika mechi ya kwanza dhidi ya APOEL Nicosia, na kibaya ni kwamba safari hii itakuwa ugenini.
Kama APOEL itaingia robo fainali itakuwa ni timu ya kwanza ya Cyprus kufikia hatua hiyo na kama ikisonga mbele itazipiku klabu za Ufaransa ambazo zimejikuta zikianguka katika hatua hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu minne.
AC Milan na Zenit ni klabu ambazo zitasaka nafasi muhimu wiki hii huku zikiwa zinaongoza ligi.
Katika hatua nyingine, Arsene Wenger ana wasiwasi kama wanaweza kubadilisha mambo yaliyotokea katika Uwanja wa San Siro.

“Hatuishi katika dunia ya ndoto, ukiangalia kwa makini utaona ni kama tumeshatolewa,” alisema kocha huyo.
Kama AC Milan itafunga bao katika Uwanja wa Emirates maana yake ni kwamba Arsenal itatakiwa kufunga mabao sita ili kusonga mbele.

Habari mbaya kwa Arsenal ni kuwa AC Milan imekuwa ikifunga angalau bao moja katika kila mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Katika hatua nyingine, kama Leverkusen ikitolewa itatoa wasiwasi kwa mashabiki wa Ujerumani ambao wanaweza kukosa wawakilishi katika hatua ya robo fainali kwa kuwa Bayern Munich ambayo nayo ipo katika hatua ya 16 bora ilifungwa na FC Basel bao 1-0 katika mechi ya awali.
Wasiwasi mkubwa upo kwa Leverkusen, ambayo itacheza na Barcelona kesho Jumatano kwa kuwa wapinzani wao ni balaa.
Kikosi cha Pep Guardiola hakijafungwa na vikosi vya Ujerumani katika mechi 16 walizokutana karibuni.
Benfica ilikuwa ikienda vizuri, ghafla ilianza kufanya vibaya baada ya kufungwa mabao 3-2 na St Petersburg wiki tatu zilizopita.

No comments:

Post a Comment