Friday, May 11, 2012
NYOTA WA MAN UNITED AOMBA KUINOA SERENGETI BOYS
Quinton Fortune enzi zake akikipiga Man United
Mshambuliaji nyota wa zamani wa Manchester United, Quinton Fortune amefunguka kuwa yuko tayari kuifundisha timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania chini ya miaka 17 kama atapewa nafasi hiyo kwa sababu kiu yake ni kuona soka ya Kusini mwa jangwa la Sahara inakuwa na kufikia kiwango cha Afrika Magharibi na Kaskazini.
Quinton Fortune
Akizungumza na Mwananchi jana jijini Dar es Salaam, Fortune alisema ingawa haifahamu rekodi ya timu ya Taifa ya Tanzania, lakini anaamini kama atapata nafasi ya kuifundisha timu ya vijana itakuwa ni faraja zaidi kwani atakuwa ametimiza kiu yake ya kufundisha soka na kuinua kiwango cha soka la Afrika ya Mashariki.
Fortune ambaye yuko nchini kwa lengo la kuzindua mashindano ya vijana ya Airtel Raising Stars, alisema anaamini wachezaji wa Ukanda huu wa Sahara wana matatizo yanayofanana na ndiyo sababu ya kushindwa kucheza soka katika ligi kubwa duniani kama England.
"Matatizo ya vijana wengi ni elimu ya soka, wana vipaji, lakini lazima upate elimu kwanza ili uweze kufanya vizuri katika soka,"alisema Fortune.
Fortune alisema tatizo lingine ni kushindwa kutafsiri mikataba mbalimbali ya soka, kushindwa kutambua umuhimu na malengo yao katika soka la kimataifa.
Alisema yeye alifanikiwa kucheza Ulaya kwa sababu aliondoka kwao akiwa na miaka 14 na kujiunga na klabu za huko ambazo zilimtunza kufikia hapo.
"Baada ya kumaliza kozi yangu ya ukocha pamoja na kumaliza kazi nilizopewa na klabu yangu ya Manchester United nitarudi Tanzania rasmi kwa ajili ya kufuatilia soka la Tanzania kwa undani zaidi pamoja na kutafuta vipaji na kufuatilia zoezi la Airtel Rasing Stars linavyoendelea pamoja na kuangalia maendeleo yao baada ya hapa,"alisema Fortune.
Mbali na Uzinduzi huo pia Fortune alitembelea Shule ya Msingi ya Maarifa iliyopo Gongolamboto na kucheza soka na wanafunzi wa shule hiyo huku akikabidhi madawati 30 mipira 40 na jezi jozi tatu
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment