Monday, May 7, 2012

SIMBA YAIRARUA YANGA 5-0, OKWI AINYANYASA BEKI YA YANGA,LOYD NCHUNGA ATOKA ATIMUA MBIO BAADA YA BAO LA TANO, MASHABIKI 3 WAZIMIA UWANJANI


Kioo cha matangazo cha uwanja mkuu wa Taifa kilivyokuwa kikisomeka katika dakika za majeruhi

Lloyd Nchunga jana alishindwa kuvumilia na kuamua kukimbia uwanjani baada ya timu yake kutandikwa bao la nne, wakati Yanga ilipopokea kipigo cha Paka mwizi cha mabao 5-0 kutoka kwa wapinzani wao, Simba.
Mwenyekiti huyo ambaye hivi karibuni alijikuta katika wakati mgumu, baada ya wazee wa klabu yake kutaka kuichukua timu mikononi mwake, alishuhudia mvua ya mabao kutoka kwa mabingwa, Simba, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar na kuzidi kuwa katika hali ngumu zaidi.
Katika mchezo huo, Simba walianza kupata bao dakika ya kwanza tu ya mchezo kupitia kwa Emmanuel Okwi aliyeunganisha vizuri pasi ya Felix Sunzu baada ya Nurdin Bakari kupoteza mpira karibu na lango la Yanga.

Nimewanyongaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa


Mchezaji aliyei-cost Yanga kuliko mchezaji mwingine yeyote Shadrack Nsajigwa


wa Yanga Papic jukwaani akiAliyekuwa kocha mkuu shuhudia timu hiyo ikinyanyaswa na Simba

Baada ya bao hilo, Yanga walifanya mashambulizi kadhaa katika dakika ya tisa na 11 huku shuti moja lililopigwa na Athuman Idd ‘Chuji’ likigonga mwamba na kurejea dimbani kabla Hamis Kiiza kupiga tena na safari hii mlinda mlango Juma Kaseja akiucheza mpira na baadaye kuokolewa na mabeki wake.

Okwi akishangilia baada ya kuitengeneza Yanga goli la kwanza

Kipindi cha kwanza kiliisha kwa Simba kuendelea kuongoza kwa bao 1-0 lakini kipindi cha pili ndicho kilichopeleka simanzi kubwa Jangwani baada ya kushuhudia kipa Said Mohammed aliyechukua nafasi ya Yaw Berko, akiokota mipira minne langoni mwake.
Aibu ya Yanga ilianzia dakika ya 53, baada ya Felix Sunzu, kupiga penalti kwa ufundi akiandika bao la pili. Penalti hiyo ilitokana na Okwi kuchezewa faulo katika eneo la hatari.
Dakika ya 62, Okwi alifanya tena kazi ya ziada, alipomtoka beki mkongwe, Shadrack Nsajigwa na kufunga bao safi lililowaacha wachezaji wa Yanga wakiwa wameshika viuno kwa huzuni.

Huku Jangwani wakiendelea kujiuliza, Simba walipata penalti nyingine katika dakika ya 66 baada ya Okwi kufanyiwa faulo tena ndani ya eneo la hatari na kipa, Mohammed. Juma Kaseja ndiye aliyepiga penalti hiyo na kuiandikia Simba bao la nne.


Nahodha wa Simba Juma Kaseja Juma akikabidhiwa kombe la ligi kuu ya Tanzania bara

Wachezaji wa Simba wakishangilia na kombe lao

Katika hali ya kushangaza, Simba walipata penalti ya tatu dakika ya 71 iliyotokana na beki, Athuman Idd ‘Chuji’ kumfanyia faulo Okwi ndani ya eneo la hatari. Patrick Mafisango alipiga penalti hiyo na kufikisha bao lake la 11 kwenye Ligi Kuu ya Bara msimu huu.
Katika tukio la kusikitisha, mashabiki wawili wa Yanga walizimia na kubebwa na watu wa Msalaba Mwekundu, baada ya Mafisango kufunga bao la tano huku Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Fred Felix Minziro, akigoma kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu mchezo huo.
Naye Kocha Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic, amesema baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa, kwa sasa wanachokiangalia ni kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Yanga ilifanikiwa kuichapa Simba bao 1-0.

Katika matokeo mengine, licha ya Villa Squad kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mlandizi, Pwani, ilijikuta ikishuka daraja na kuungana na Polisi Dodoma pamoja na Moro United.

Umati uliohudhuria kichapo cha Yanga

Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, JKT Oljoro ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi, wakati huko Mkwakwani, Tanga, Toto ilipata kipigo kama hicho kutoka kwa Coastal Union na kunusurika kushuka daraja kutokana na kuwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa licha ya kuwa na pointi 26 sawa na Villa.
Mtibwa Sugar iliendeleza ubabe wake kwa kuifunga Moro United bao 1-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Azam ikiishinda Kagera mabao 2-1, Chamazi, Dar na African Lyon ikiibamiza JKT Ruvu mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro

No comments:

Post a Comment