Kocha aliyefariki dunia Manuel Preciado
Kocha mpya aliyeteuliwa juzi Manuel Preciado amefariki saa 24 baada ya kutangazwa kama Kocha wa klabu ya Uhispania, Villarreal.
Kocha huyo ambaye hapo zamani alikua kocha wa Sporting Gijon alifariki kutokana na mshtuko wa moyo akiwa na umri wa miaka 54.
Kifo chake kimetokea saa 24 baada ya kukubali mkataba wa kuiongoza klabu ya
Villareal iliyoshuka daraja, ambapo mkataba wake ulikua wa kuanza msimu wa mwaka
2012 hadi 2013.
Kocha Preciado enzi za uhai wake viwanjani
Preciado aliefungashiwa virago na Sporting Gijon mnamo mwezi Januari licha ya kuiwezesha klabu hio kupanda daraja mara mbili kuingia Ligi kuu ya Uhispania, La Liga.
Mnamo mwezi Aprili mwaka 2011, klabu yake ya Sporting Gijon iliikwamisha klabu maarufu ya Real Madrid kwa kuvunja rekodi yake ya miaka tisa bila kupoteza kwenye uwanja wa nyumbani safari hii ikiwa chini ya Jose Mourinho.
Wakati akisakata soka Preciado alicheza kama beki na alianza kukipiga katika klabu ya Racing Santander na pia kushiriki mechi za vilabu kama Linares, Mallorca, Alaves, Ourense na Gimnastica.
Baada ya kustaafu kama mchezaji mwaka 1992, akaanza shughuli za ukufunzi akianzia klabu ya Gimnastica na pia kuinoa Racing B, Racing Santander, Levante na Murcia kabla ya kujiunga na Sporting Gijon mwaka 2006.
Baadaye aliiwezesha klabu hio kupanda daraja hadi Ligi kuu ya Uhispania katika msimu wake wa pili na kukaa na klabu hio kwa kipindi cha miaka sita.
No comments:
Post a Comment