Thursday, June 21, 2012
RUNGU LA UEFA LAIANGUKIA ENGLAND KUFUATIA VURUGU ZA MASHABIKI EURO 2012
Mashabiki wa soka wa Uingereza wakilipuka kwa mayowe ya ushindi
Chama cha soka cha England, FA, kimelimwa faini ya Euro 5,000 (sawa na pauni 4000), kutokana na utovu wa nidhamu wa mashabiki wake ambao Ijumaa iliyopita walijaribu kuuvamia uwanja baada ya England kuichabanga Sweden.
Faini hiyo ni kufuatia mashabiki kujaribu kuingia uwanjani baada ya England kuiangushia kipigo Sweden cha 3-2 katika mechi ya kundi D mjini Kiev.
Chama cha FA kimeamua hakitakata rufaa kuhusiana na faini hiyo, na kwa kuwa UEFA haijaitoza FA pesa nyingi, inaashiria kwamba shirikisho hilo la soka ya Ulaya linalichukua tukio hilo kama jambo dogo.
"Tunakubali hatua iliyochukuliwa, na tunalifikiria tukio hili kama jambo ambalo limetatuliwa," taarifa ya FA ilielezea.
Baada ya magoli ya England yaliyotiwa wavuni na Theo Walcott na Danny Welbeck, mashabiki kati ya 20 hadi 30 walivikaribia vizuizi uwanjani, na kutaka kuingia ndani ya uwanja wa Olympic, lakini walifanikiwa kuifikia sehemu ya riadha tu.
Chama cha FA, kikijitetea, kiliweza kutoa ushahidi thabiti wa video mbele ya UEFA na kuonyesha kwamba “uvamizi” huo ulikuwa ni jambo ambalo lilitokea ghafula, na wala mashabiki hao hawakuwa wamepanga kutekeleza kitendo hicho.
Tukio hilo lilichukuliwa kama jambo dogo, na hata afisa wa UEFA katika mechi hiyo hakulitaja katika ripoti yake kuhusiana na mechi.
Chama cha FA pia kimethibitisha kwamba hakuna mashabiki wa England waliokamatwa aidha nchini Poland au Ukraine katika mashindano ya mwaka huu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment