Friday, August 3, 2012

YAKWANGU BAADA YA KAULI YA Dk MWAKYEMBE KUZUIA "UCHIMBAJI DAWA"


Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe.

Waziri wa uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe kupitia bunge amepiga marufuku mabasi ya abiria yaendayo mikoani kusimama njiani ili kutoa fursa ya abiria kujisaidia(Kuchimba Dawa).Na kuahidi kuwachukulia hatua wenye mabasi watakaosimamisha mabasi njiani na abiria kwenda kujisaidia.
Binafsi nina haya ya kujiuliza, Swala la mtu kwenda haja ni la hiari au sio la hiari?
Pia anaposema kuwachukulia hatua wenye mabasi, shida ya kwenda haja ndogo ni ya wenye mabasi au ni ya abiria?
Na je amechukua hatua gani za makusudi kuwasaidia wasafiri jinsi ya kujisaidia wawapo safarini baada ya kupiga kupiga marufuku mabasi ya abiria kusimama njiani?


Nijuavyo mimi swala la mtu kwenda haja sio la kupanga ila ni swala la kibiolojia. Mtu huhitaji kwenda haja ndogo baada ya matumizi ya Vyakula na vinywaji na baada ya mwili kufanya kazi na kuchukua virutubisho muhimu huhitaji kutoa vile visivyohitajika mwilini. Na pindi mwili unapohitaji kutoa masalia ya chakula na vinywaji yasiyohitajika mwilini ni kitendo kisichokuwa cha hiari, ambacho kwa lugha ya kitaalamu hujulikana kama "Involuntary action".


Unaweza kumshauri mtu asitumie vinywaji au apunguze matumizi ya chakula awapo safarini, lakini ikumbukwe kuwa hali ya hewa,mshtuko na aina ya vyakula huweza kusababisha mabadiliko ya ghafla katika mwili wa binadamu na kusababisha mtu kuhitaji kutoa haja. Mara nyingi hutegemea na maumbile ya mtu na matumizi ya vyakula ama vinywaji,wakati mwingine vyakula au vinywaji mtu awapo safarini ndio huwa chanzo kikubwa cha kuleta mabadiliko ya ghafla katika mwili wa binadamu na kusababisha aidha kwenda haja ya kawaida au haja itokanayo na ugonjwa kutokana na chakula au kinywaji alichotumia mtu.


Sababu kubwa aliyoitoa Mh Mwakyembe ni kuwa kitendo cha mabasi ya abiria kusimama njiani na watu kujisaidia ni udhalilishaji kwa kile alichosema kwamba abiria wa rika tofauti huchanganyika wakati wa kujisaidia"kuchimba dawa". Binafsi pia naona huo ni udhalilishaji lakini sio busara kupiga marufuku mabasi ya abiria kusimama na watu kwenda kujisaidia kwasababu kitendo cha kujisaidia sio cha hiari ni cha kibiolojia.
Nafikiri ingekuwa busara kama Mh Mwakyembe kupitia bunge wangejadili ni jinsi gani ya kuwasaidia abiria wanaohitaji kujisaidia wawapo safarini ili kuwaepusha na udhalilishaji, Kitu ambacho kingefanyika Ni kuangalia jinsi gani utaratibu wa kujisaidia njiani"kuchimba dawa' ungeratibiwa ili kuondoa muingiliano wa rika na jinsia pindi mabasi yanaposimama njiani na abiria kujisaidia.
Hili lingewezekana kwa kuwashirikisha madereva na makondakta wa mabasi ya abiria, Kwa pamoja wakajadili utaratibu wa abiria kujisaidia njiani uwe wa namna gani ili kuondoa udhalilishaji uliozungumziwa.
Ingekuwa ni busara zaidi kupitia bunge wangepitisha Sheria ya kila basi la abiria la kwenda mikoani ni lazima liwe na choo,sheria au utaratibu huu ungeondoa madhila yote yanayotokea pindi abiria wanapojisaidia njiani.

No comments:

Post a Comment