Bunge la Bajeti ya Serikali ya 2015/16 linaanza leo
mjini Dodoma kwa mwendo wa mchakamchaka kutokana na kuongezwa saa mbili
kila siku ili limalizike Juni 27.
Saa za mjadala katika vikao zimeongezwa ili kuziba
pengo la siku 12 zinazopungua na kutoa fursa kwa wabunge kuchangia
bajeti za wizara na Bajeti Kuu ya Serikali ndani ya siku 44
ikilinganishwa na siku 56 zilizotumika kupitisha bajeti ya mwaka 2014/15
na miaka ya nyuma.
Kutokana na hali hiyo, wachambuzi wa bajeti,
wachumi na wanasiasa wamesema hawatarajii kuona jipya isipokuwa mipasho
inayolenga Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Serikali imepanga kukusanya na kutumia Sh22.4
trilioni katika mwaka wa fedha 2015/16 ikiwa ni nyongeza ya Sh2.6
trilioni ikilinganishwa na Bajeti ya mwaka 2014/15 ambayo ilikuwa Sh19.8
trilioni.
Kwa miaka iliyopita, baadhi ya wizara zenye
majukumu mengi zilikuwa zinatengewa siku mbili au tatu, lakini safari
hii hali itakuwa tofauti kwa kuwa zitajadiliwa kwa siku moja tu au mbili
kulingana na mjadala utakavyokuwa na mapumziko yatakuwa Jumapili pekee.
Mkurugenzi wa Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano
wa Kimataifa wa Bunge, Jossey Mwakasyuka alisema badala ya Bunge kuanza
saa 3.00 asubuhi hadi saa 7.00 mchana na baadaye saa 11 jioni hadi saa
1.45 usiku; sasa litaanza 3.00 asubuhi hadi saa 8.00 mchana na kuendelea
saa 10.00 jioni hadi saa 2.00 usiku.
“Ili kuendana na muda, tumeongeza saa kadhaa ili
kumaliza shughuli zote zilizopangwa. Siku za Jumamosi zitahesabika kama
siku za kazi kama kawaida.” alisema.
Alisema Bunge hilo litamalizika Juni 27 lakini
akaongeza: “Tumeacha siku tatu za dharura, kuanzia Juni 28 hadi 30 ili
kama kuna jambo lolote la muhimu litajitokeza Bunge linaweza kuendelea
kwa muda huo wa siku tatu.”
Alisema kutokana na mabadiliko ya uwasilishaji, ni
lazima bajeti iwe imesomwa kabla ya kuanza utekelezaji wa bajeti ya
mwaka unaofuata Julai Mosi.
“Inawezekana tukapata kiongozi wa kulihutubia
Bunge au katika upitishaji wa bajeti za wizara akidi isitimie na
kulazimika shughuli husika kuendelea siku inayofuata. Zamani Bunge la
Bajeti lilikuwa likianza Juni hadi Agosti, lakini kwa mabadiliko haya
sasa lazima limalizike Juni,” alisema.
Alisema bajeti zote za wizara hadi kufikia Juni 10
zitakuwa zimeshasomwa, Juni 11 itasomwa Bajeti Kuu ya Serikali na
kuanza kujadiliwa.
Alisema ratiba hiyo pia inaweza kuvurugika utakapoanza mfungo wa Ramadhani.
No comments:
Post a Comment