Thursday, March 15, 2012

MAMA AJERUHI MWANAWE KWA MPIRA

Video hii inaonesha tukio lililotokea huko majuu ambapo mtoto alikuwa akicheza mpira katika bustani ya nyumbani kwao, mama kwa upendo akaona akajiunge na mwanae katika kucheza lile kabumbu.
Wakati mama na mwana wakirukaruka huku na kule wakisukuma lile kabumbu kwa muda fulani kama kawaida kitu chochote hasa michezo ukiufurahia sana mzuka unapanda si kitoto,balaa lililotokea baada ya mama na mwana kupandwa na mzuka wa soka ni mama kujikuta akifumua shuti la kwelikweli kuelekea kwa mwanawe na kwa bahati nzuri au mbaya mama alifumua shuti lililokwenda moja kwa moja kwenye uso wa mwanawe kama unavyoona wachezaji wanapofumua mashuti na kutinga wavuni basi ndivyo ilivyokuwa.
Mtoto ilibidi aangue kilio baada ya shuti kutua sawasawa katika paji la uso wake, mama alipatwa na kazi ya ziada kumnyamazisha mtoto na hatimae mtoto alinyamaza na kama ilivyo kawaida kwa watoto hawana kinyongo muda uleule akatabasamu na akaanza tena kucheza mpira huku akimuita mama yake, safari hii mama alikuwa kama kafungwa mawe miguuni alishindwa kabisa kupiga mpira.

Tuesday, March 13, 2012

ARSENAL "GUNNERS" WAIRARUA NEWCASTLE BILA HURUMA


Robin Van Persie "R.V.P" akitupia kambani goli la kusawazisha dhidi ya Newcastle


Thomas Vermaelen na Sagna wakishangilia goli la pili na la ushindi

Thomas Vermaelen alifunga bao la ushindi katika dakika ya 95 dhidi ya Newcastle, na kupunguza tofauti ya pointi kati yake na Tottenham kuwa ni pointi moja tu.
Tottenham imo katika nafasi ya tatu, na Arsenal inashikilia nafasi ya nne.
Hatem Ben Arfa aliwawezesha Newcastle kupata bao la kwanza katika mechi hiyo ya Jumatatu jioni kwa bao la chini kwa chini, lakini furaha yao ilizimwa hata kabla ya dakika moja kumalizika.
Theo Walcott alimsukumia mpira Robin van Persie, na ambaye alifunga bao lake la 33 msimu huu.
Mvutano ulizuka uwanjani baada ya kipenga cha mwisho, kufuatia bao la Vermaelen ambalo liliingia wavuni huku mechi ikielekea kumalizika, na mechi hiyo ikiwa ni ya nne ambayo Arsenal, baada ya kuachwa nyuma, iliweza kujitahidi na kupata ushindi.
Ulikuwa ni ushindi wa kusisimua kwa mashabiki wa Arsenal, timu ambayo imecheza vizuri sana hivi karibuni, hasa ikifikiriwa kwamba majirani Spurs walikuwa na tofauti ya pointi 12 kati yao na Arsenal, kabla ya mechi sita zilizopita.
Arsenal 2-1 Newcastle United 

Monday, March 12, 2012

Swansea yaipopoa Man City Kileleni, Man United yakalia usukani


Wayne Rooney akitupia kambani goli la kwanza la United dhidi ya WBA.

Manchester United imefanikiwa kukalia kiti cha Ligi ya Kuu ya England kwa mabao mawili yaliyopachikwa na Wayne Rooney na kuilaza West Brom.
United imepata nafasi hiyo ya kukalia kiti cha uongozi baada ya Manchester City kuteleza kwa kulazwa bao 1-0 na Swansea.
Rooney aliifungia Manchester United bao la kwanza kabla ya mapumziko, alipounganisha mpira uliopigwa na Javier Hernandez ambao ulimpita mlinda mlango Ben Foster.
Mshambuliaji huyo wa Manchester United alifunga tena bao la pili kwa mkwaju wa penalti, wakati mlinzi wa West Brom Jonas Olsson alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya njano.
Man united 2-1 West Bromwich Albion

Wakiwa wamesaliwa na michezo 10 kabla ya msimu wa ligi kumalizika, Manchester United sasa wanapewa nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wake baada ya Manchester City kuteleza.
Matumaini ya Manchester City kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya Kandanda ya England yaliingia dosari baada ya bao la kichwa dakika za mwisho la Luke Moore lilipoipatia Swansea ushindi wa bao 1-0.

Young na Rooney wakishangilia Goli

wansea City kwa ushindi huo sasa imeacha wazi mbio za kuwania ubingwa ligi ya England baada ya ushindi huo katika uwanja wao wa Liberty.
Kikosi cha Roberto Mancini kiliponea chupuchupu kufungwa dakika za mwanzo za mchezo wakati Joe Hart alipookoa mkwaju wa penalti wa Scott Sinclair baada ya Hart kumuangusha Wayne Routledge ndani ya sanduku la hatari.
Swansea ilipata bao lake hilo moja baada ya Moore kuunganisha kwa kichwa mpira wa pembeni wa Routledge zikiwa zimesalia dakika saba kabla mchezo kumalizika.
City hawakucheza vizuri ingawa Micah Richards dakika za mwisho alifunga bao ambalo lilikataliwa kwa vile alikuwa ameotea.
Manchester City sasa wanashikilia nafasi ya pili wakiwa na pointi 66 na Manchester United wamekusanya pointi 67.

Chelsea yazinduka usingizini,Liverpool yapokea kichapo kutoksa kwa Sunderland


Didier Drogba akiwa katika harakati za kufunga na kufanikiwa kuipatia goli Chelsea


Drogba akishangilia goli dhidi ya Stoke City nyuma ni Sturridge na Juan Mata
Chelsea 1-0 Stoke City

Didier Drogba umaliziaji wake maridadi umeihakikishia ushindi ingawa mwembamba Chelsea dhidi ya Stoke City iliyokuwa ikicheza pungufu ya mchezaji mmoja katika pambano la kwanza la Roberto di Matteo kusimamia akiwa meneja wa muda Chelsea katika Ligi Kuu ya England.
Stoke walicheza karibu mchezo wote wakiwa na wachezaji 10 baada ya Ricardo Fuller kuoneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumtimba pajani Branislav Ivanovic.
Chelsea mipira yao iligonga mwamba mara mbili lakini iliwabidi wawe waangalifu kuikabili Stoke City iliyokuwa ikijihami vizuri.
Lakini Drogba hatimaye akamaliza kazi baada ya kumzunguka mlinda mlango Asmir Begovic baada ya kupokea pasi ya Juan Mata na kupachika bao lake la 100 tangu aanze kucheza Ligi Kuu ya England.
Hali ya kusua-sua kwa Liverpool kwenye ligi imeendelea tena baada ya kuchapwa na timu iliyoonesha ari ya kusaka ushindi ya Sunderland.
Baada ya kosakosa za kipindi cha kwanza, Sunderland walifanikiwa kuongoza kwa kupachika bao baada ya mkwaju wa Fraizer Campbell kuzuiwa na mlinda mlango Pepe Reina kabla ya Nicklas Bendtner kuuwahi na kuutumbukiza wavuni.
Liverpool waliwaingiza Steven Gerrard na Andy Carroll lakini mabadiliko hayo hayakuzaa matunda kwa upande wa wao.

Niclas Bendtner akishangilia goli alilofunga dhidi ya Liverpool

Sunderland 1-0 Liverpool

Sunderland walijihami vyema kulinda bao lao moja dhidi ya Liverpool ambao nusura wangesawazisha.
Junior Hoilett akifunga mabao mawili ameisaidia timu yake ya Blackburn kupanda juu kutoka eneo la hatari la kuteremka daraja na kuicha Wolves wakicheza uwanja wa nyumbani wakiendelea kusuasua eneo la kuteremka daraja wakiwa nafasi moja tu kutoka mkiani.
Mashabiki wa Wolves walifanya maandamano kabla ya mchezo dhidi ya Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu yao ya Wolves Jez Moxey kwa kumteua Terry Connor kushikilia nafasi ya umeneja na hatimaye wakashuhudia timi yao ikiporomoka kwa kuonesha kiwango cha chini.
Hoilett alifunga bao lake la kwanza baada ya kumiliki mpira wa kimo cha mbuni na kuachia mkwaju kutoka upande wa kona na kuingia moja kwa moja wavuni.
Na baadae mshambuliaji huyo akafanikiwa kufunga bao lake la pili kwa mkwaju wa yadi 25 mara tu baada ya kuanza kipindi cha pili.
Kufungwa huko kumeicha Wolves nafasi ya 19, nafasi moja tu kutoka mkiani wakiwa wamepata ushindi wa mchezo mmoja tu katika mechi 14 za Ligi zilizopita.
Bao la kwanza la Andreas Weimann la Ligi Kuu ya England liliipatia ushindi Aston Villa dhidi ya Fulham waliokuwa wakicheza kwa kiwango cha juu na hatimaye wakamaliza kwa huzuni katika uwanja wa Villa Park.
Villa walimiliki mchezo katika kipindi cha kwanza huku Gabriel Agbonlahor nusura angepachika bao.
Marc Albrighton alipiga mkwaju uliogonga mwamba katika dakika za mwanzo za kipindi cha pili na baadae Damien Duff wa Fulham mkwaju wake nao ukagongwa mwamba. Hadi mwisho Aston Villa 1 Fulham 0.
Meneja wa QPR Mark Hughes aliachwa asifahamu la kufanya baada ya kushuhudia timu yake ikinyimwa ushindi baada ya bao la dakika za mwisho la Ivan Klasnic kuipatia ushindi wa mabao 2-1 Bolton.
QPR ilitakiwa kuwa mbele kwa bao moja kipindi cha kwanza lakini mpira wa kichwa aliochonga Clint Hill haukuhesabiwa bao licha ya mpira kuonekana umevuka mstari.
Bolton iliongoza kwa bao la kwanza lililofungwa kwa kichwa na Darren Pratley kabla Djibril Cisse kusawazisha kwa mkwaju wa karibu, ingawa baadae picha za televisheni zilizokuwa zikirudiwa zilionesha alikuwa ameotea.
Lakini bao la dakika za mwisho la Klasnic aliyepokea pasi murua kutoka kwa Ryo Miyaichi na kufanikiwa kumpita mlinda mlango Paddy Kenny, liliitoa Bolton kutoka eneo hatari la kuteremka daraja.

Friday, March 9, 2012

WENGER AOPOA "JEMBE" KUTOKA F.C COLOGNE

Lukas Podolski
Kifaa kipya kitakachotua Arsenal Lukas Podolski

Klabu ya Arsenal imeafikiana na mshambuliaji wa Ujerumani Lukas Podolski kutoka klabu ya Cologne, BBC Michezo imefahamu.
Kwa mujibu wa taarifa Arsenal italipa pauni za Uingereza £10.9m kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 kwa mkataba wa miaka minne akilipwa pauni £100,000 kila wiki.

Thursday, March 8, 2012

HAPPY WOMENS DAY

MBWANA SAMATTA YUKO JUU ATIKISA NYAVU HUKO MBUJI-MAYI


Mbwana Samatta mfungaji wa goli pekee na la ushindi la TP Mazembe dhidi ya S.M Sanga Balende

MBWANA Samatta ameendelea kudhihirisha kuwa ni moto wa kuotea mbali katika kuzifumania nyavu, baada ya kuifungia timu TP Mazembe bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya timu ya S.M Sanga Balende.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (Super League) ilichezwa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Kumbuji- Mayi, kilomita 1000 kutoka jiji la Lubumbashi.

Mbwana alifunga bao hilo dakika 48, kutokana na krosi ya Kilitcho Kasusula aliyeingia kipindi cha pili dakika ya 46 kuchukua nafasi ya Ngandu Kasongo.
Muda huo ndiyo aliingia Mtanzania mwingine, Thomas Ulimwengu kuchukua nafasi ya Yannick Tusilu.
Baada ya mchezo huo, rais wa klabu hiyo, Moise Katumbi aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo mgumu.
Haya ni mafanikio mengine kwa Samatta akiwa na TP Mazembe na ndiye anaongoza kwa ubora kwenye timu hiyo tangu msimu mpya wa ligi uanze.

Hivi karibuni, Kocha wa timu ya Taifa (Taifa Stars, Jan Poulsen alimtema nyota huyo chipukizi kwenye kikosi cha Stars kwa maelezo kwamba hajitumi anapoitwa kuchezea timu hiyo.