Tuesday, April 24, 2012

EVERTON YAIBANA MBAVU MAN UNITED


Nani akipigilia msumari huku kipa wa Everton akichumpachumpa bila mafanikio

Matumaini ya Manchester United kunyakua taji la ubingwa wa Ligi ya Kandanda ya England yalitiwa doa wakati Everton ilipopigana kiume wakiwa nyuma ya mabao 4-2 na kumaliza mchezo kwa sare ya mabao 4-4 katika mpambano wa kusisimua hasa dakika za mwisho kwenye uwanja wa Old Trafford.
Wayne Rooney aliisawazishia Manchester United baada ya kuunganisha kwa kichwa pasi kutoka kwa Nani baada ya bao la kuongoza la Everton lililofungwa kwa na Nikica Jelavi.


Rooney akitupia kambani katika mechi hiyo

Danny Welbeck na Nani waliipatia Manchester United mabao mawili kabla Marouane Fellaini kufunga bao moja jingine kwa Everton.

Rooney alionekana kuipatia ushindi Man United alipopachika bao la nne na muda mfupi baadae Everton wakacharuka na kupachika mabao mawili katika muda wa dakika tatu kupitia kwa Jelavic na Steven Pienaar.


Fellaini akipiga kichwa mbele ya Ferdinand na kuipatia bao la kusawazisha Everton

Katika dakika za mwisho, Patrice Evra alipiga mpira wa kichwa uliogonga mlingoti wa lango la Everton akiwa karibu kabisa na baadae mlinda mlango wa Everton Tim Howard aliokoa kwa ustadi mkubwa mkwaju wa Rio Ferdinand na kuinyima ushindi Manchester United.

Manchester United hata hivyo bado wanaongoza Ligi Kuu ya England wakiwa na pointi 83.

Dah hawa watoto vipi wametumwa?

MAWAKILI SITA WANAMTETEA LULU ,YUMO MSHINDI WA TUZO YA MWANAMKE JASIRI YA MARTIN LUTHER KING


LULU
Msanii  wa filamu za Bongo movies, Elizabeth Michael Kimemeta maarufu kama Lulu, jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu huku akibubujikwa machozi kiasi cha kumfanya Hakimu Ritha Tarimo ambembeleze ili kumnyamazisha. Lulu anashtakiwa mahakamani hapo kwa kutuhuma za kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba na alifikishwa jana kwa mara ya pili akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari Magereza na Polisi.

Lulu alifikishwa mahakamani hapo saa 3:06 asubuhi akiwa katika basi dogo la Magereza pamoja na mahabusu wengine wanawake ambalo lilikuwa likisindikizwa na magari mengine mawili na alikuwa chini ya ulinzi wa askari sita wa kike wa Magereza na askari mmoja wa kike wa Polisi wakishirikiana na askari wa kiume wa Magereza zaidi ya sita.















Lulu (mwenye kiremba) akisindikizwa na askari kuingia mahakamani huku machozi yakimmwagika

Mara baada kuingia katika chumba cha Mahakama, Lulu ambaye alikuwa amevalia dira jekundu alianza kulia kwa uchungu hali ambayo ilimlazimu Hakimu Tarimo pamoja na baadhi ya askari kumnyamazisha.
Kutokana na kujaa kwa watu mahakamani hapo, askari wa Kikosi Maalumu cha Magereza walilazimika kuufunga mlango wa Mahakama hiyo ili kesi hiyo isikilizwe.

Baada ya kesi hiyo kutajwa, Wakili Mwandamizi wa Serikali Elizabeth Kaganda aliiomba Mahakama iamuru watu wote watoke nje kwa sababu walikuwa wamefunga njia ili mtuhumiwa huyo aweze kupitishwa.

Hakimu Tarimo alikubaliana na ombi hilo na kuwaamuru askari kusafisha njia ili waweze kumpitisha msanii huyo kwa kile alichosema kuwa Lulu bado ni mtuhumiwa na anaweza kuumizwa.
“Askari safisheni njia ili mtuhumiwa aweze kupita kwa sababu yeye bado ni mtuhumiwa anaweza kuumizwa,"alisema Hakimu Tarimo.

Baada ya kutolewa kwa amri hiyo, askari walitimiza wajibu wao na muda mfupi njia ilipatikana na msanii huyo kutolewa mahakamani hapo.

Jopo la mawakili
Katika kesi hiyo, Lulu anatetewa na jopo hilo la mawakili akiwemo Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Joaquine De- Melo, Kenedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Massawe.

De- Melo pia aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) na mshindi wa Tuzo ya Mwanamke Jasiri Tanzania ya Martin Luther King.

Fungamtama ambaye ndiye kiongozi wa jopo la mawakili hao wanaomtetea Lulu, anakumbukwa kwa kuitetea kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans, katika kesi dhidi ya Tanesco, ambayo alishinda na shirika hilo kuamriwa kuilipa kampuni hiyo zaidi ya Sh94 bilioni kwa kuvunja mkataba.
Kibatala ambaye pia anamtetea kada wa Chadema, Fred Mpendazoe katika kesi ya uchaguzi Jimbo la Segerea, pia ni Makamu wa Rais wa TLS, wakati Massawe anatoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Mawakili hao walijitokeza jana mbele ya Hakimu Tarimo tayari kumtetea Lulu na baada ya mawakili hao kujitambulisha, Wakili Kaganda alisema upelelezi wa kesi bado haujakamilika na kuiomba Mahakama iipangie tarehe nyingine.

Hakimu Tarimo aliiahirisha kesi hiyo hadi Mei 7, mwaka huu itakapofikishwa mbele ya Mahakama hiyo kwa ajili ya kutajwa.

Kwa mara ya kwanza Lulu alifikishwa mahakamani hapo Aprili 10, mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando akikabiliwa na la shtaka hilo la mauaji.

Wakili Kaganda alimsomea hati ya mashtaka alidai kuwa Aprili 7, mwaka huu katika maeneo ya Sinza Vatican, Wilaya ya Kinondoni, mtuhumiwa alimuua Kanumba. Kanumba alifariki dunia siku hiyo saa 9:00 usiku kwa kile kilichodaiwa kuwa ni baada ya ugomvi baina yake na Lulu

Monday, April 23, 2012

SHAMPOO HIZI NI HATARI





Aina ya Shampoo zilizooneshwa hapo juu ni hatari kwa afya yako, Habari za kuthibitika zinasema kuwa serikali ya Dubai imechoma moto shehena ya shampoo hizo.
Taarifa za kitaalamu zinasema shampoo hizo zina kemikali kali inayoweza kuharibu ngozi yako kwa haraka zaidi kwani kemikali zilizotumika kutengenezea Shampoo hizo ni kali katika ngozi ya binaadamu na ni za matumizi ya maabara!

NGORONGORO HEROES YAIADABISHA SUDAN


Thomas Ulimwengu

Timu ya taifa ya Tanzania chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, imepata ushindi kwa kuwachabanga vijana wenzao kutoka Sudan jumla ya magoli 3 -1 katika mechi ya mkondo wa kwanza kufuzu fainali Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20.

Mechi hiyo ilichezwa Jumamosi katika uwanja mkuu wa taifa mjini Dar es Salaam.

Thomas Ulimwengu, mchezaji anayechezea klabu ya TP Mazembe ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo ndiye aliyeanza kufunga goli la kwanza kwa upande wa Tanzania katika dakika ya 13 kipindi cha kwanza.

Iliwachukua timu ya Tanzania dakika tano ambapo katika dakika ya 18 Ramadhani Singano alipachika goli la pili na hivyo hadi mapumziko matokeo yalikuwa 2-0.

Katika kipindi cha pili timu ziliingia uwanjani kwa ari kubwa ya kupata magoli ambapo zilionekana kushambuliana kwa zamu.

Ni Tanzania tena waliobahatika kupata goli mwishoni mwa kipindi cha pili katika dakika ya 43 kupitia Simon Msuva.

Hata hivyo Sudan walionekana kutokata tamaa ambapo katika dakika ya 46 Ahmed Nas Eldin alipachika goli la kufuta machozi kwa upande wa Sudan, na mpira ukamalizika kwa matokeo ya 3-1.

Timu hizi zinatarajiwa kucheza mechi ya mkondo wa pili wiki mbili zijazo mjini Khartoum, Sudan, kati ya Mei 4, 5 au 6 mwaka huu.

Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 zinatarajiwa kuchezwa nchini Algeria mwaka 2013.

Bingwa mtetezi ni Nigeria.

Thursday, April 19, 2012

NAHODHA WA UINGEREZA APIGWA MIMBA, KUIKOSA OLIMPIKI


Nahodha wa timu ya soka ya wanawake ya Uingereza Faye White

Kukiwa kumesalia siku mia moja kwa michezo ya Olimpiki kuanza kutimua barafu mjini London ,Kapteni wa timu ya Soka ya Uingereza ya wanawake Bi Faye White atayakosa mashindano hayo.
Bi White hataichezea timu yake ya taifa Uingereza wakati wa Olimpiki kwa sababu ana mimba.
Bibi huyo mwenye umri wa miaka 34 ambaye nyumbani anachezea timu ya soka ya wanawake ya Arsenal amesema anatarajia kujifungua mwezi wa Oktoba.

Faye awapo uwanjani shughuli yake si ndogo hata kidogo

Bi White amedokeza kuwa huenda pia akajiuzulu kutoka timu hiyo ya taifa mara tu baada ya kujifungua
" Nina mimba na kwa mara ya kwanza kufikia mwezi wa Oktoba nitakuwa mama” aliiambia BBC.
Kapteni huyu atakumbukwa kwamba wakati wa robo fainali ya kombe la dunia kwa akina dada mwaka wa 2011 walipochuana na Ufaransa alikosa mkwaju wa penaliti.
Bi White anasema hana uhakika kama baada ya kujifungua ataendelea kuchezea klabu yake ya Arsenal au atastaafu kabisa kutoka mchezo huo.

Bi Faye akiwa kwenye uzi wa chama lake la Arsenal

BARCELONA YABONYEZWA "KIZENJ" NA CHELSEA


Didier Drogba akitia kambani huku Golikipa Valdes akichumpa bila mafanikio

Didier Drogba aliishangaza Barcelona alipofunga bao la Chelsea na la pekee katika mechi dhidi ya Barcelona, na kuiongezea timu yake matumaini ya kufika katika fainali ya klabu bingwa barani Ulaya itakayopigwa katika dimba la Allianz Arena mjini Munich Ujerumani.


Nani kama mimiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii

Drogba alitupia kambani katika kipindi cha kwanza, baada ya dakika mbili kuongezwa, huku vijana wa meneja wa Chelsea, Roberto di Matteo wakiimarisha ngome kali katika uwanja wao wa Stamford Bridge.
Barcelona waliumiliki mpira na kuutawala mchezo huo lakini walishindwa kumtungua kipa wa Chelsea, Petr Cech.
Michomo miwili ya Barcelona iligonga mwamba na ilionekana dhahiri kuwa bahati haikuwa yao.
Hayo yalimpata Alexis Sanchez katika kipindi cha kwanza, na baadaye naye Pedro akitumaini kufunga bao la chini kwa chini bila mafanikio na baadaye mkwaju wake pia ukigonga mwamba.
Kiungo cha kati wa zamani wa Arsenal, Cesc Fabregas al manusra atupie kambani lakini mpira alioupiga wakati ukielekea kambani uliokolewa na Ashley Cole.
Ingawa Chelsea imefanikiwa kuongoza mkondo wa kwanza wa nusu fainali baada ya timu hizo kukutana Jumatano jioni, bila shaka wachezaji hao wa timu ya England wanafahamu watakuwa na kibarua kigumu katika uwanja wa Nou Camp wiki ijayo katika mkondo wa pili wa nusu fainali hiyo itakayoamua nani ataelekea mjini Munich katika fainali.

Drogba akichuana vikali na beki wa Barcelona Puyol
CHELSEA 1-0 BARCELONA

KIBELAAAAAA SIMBA S.C NI NOMA YAICHABANGA JKT RUVU ,YANGA NYAVU HAZIJATEMA


Wachezaji wa simba wakishangilia goli la Uhuru Suleysh

Mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara Yanga, wamechomoka ramsi kwenye mbio za ubingwa Ligi Kuu Bara na kuicha fursa hiyo kuwaniwa na mahasimu wao wakubwa Simba na Azam FC baada ya jana kupata kipigo wasichotarajia cha bao 1-0 toka Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Mahasimu wao Simba walijiimarisha kileleni mwa msimamo baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Ruvu, matokeo yanayowafikisha pointi 56 ambazo kimsingi haziwezi kufikiwa na Yanga hata kama itashinda mechi zake tatu zilizosalia.


Suleysh akishangilia bao

Wachezaji wa Simba wakishangilia Ushindi dhidi ya JKT Ruvu

Yanga inabaki katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 43, na hata kama itashinda michezo yake mitatu iliyobaki, itafikisha pointi 52 ambazo zimeshapitwa na Simba, huku Azam yenye pointi 50 ikihitaji ushindi kwenye mchezo mmoja tu kuzipita pointi hizo za Yanga.

Lakini hata kama watakata rufaa na kurejeshewa pointi walizopokwa na Kamati ya Usuluhishi na Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), bado Yanga watafikisha pointi 55 ambazo tayari zimeshapitwa na Simba.

Katika mechi hiyo iliyojaa kila aina ya ushindani, shujaa wa Kagera Sugar aliyeipoteza Yanga kwenye ramani ya mbio za ubingwa alikuwa Shija Mkina aliyefunga bao pekee dakika ya 26.

Shija alifunga bao hilo akitumia makosa ya kipa wa Yanga, Yaw Berko aliyeshindwa kulinasa vizuri mikononi mwake shuti la adhabu ndogo lililopigwa na Mike Katende na mpira kumponyoka kabla ya kumkuta mfungaji.

Kocha wa Yanga, Costadin Papic ambaye hakuwapo kwenye benchi wakati Yanga ilipolala 3-2 na Toto African mechi iliyotangulia, alisema ameyakubali matokeo lakini bila kuwa tayari kusema lolote kuhusu kuutema ubingwa.

Kabla ya bao hilo, Mkina alifunga lingine dakika ya 8, lakini mwamuzi Rashid Msangi alilikataa kwa madai mfungaji alikuwa ameotea, uamuzi uliolalamikiwa na kocha wa Kager Mlage Kabange.

Kabange alisema mwamuzi alichezesha mechi hiyo chini ya kiwango na hakuwa makini katika maamuzi mengi yaliyofanya kiasi cha kuifanya mechi hiyo kuwa na makosa mengi yasiyo ya lazima.

Kipigo hicho ni mwendelezo wa mkosi kwa Yanga, kwani imemaliza ziara ya mechi za Ligi Kuu bila bila kupata pointi Kanda ya Ziwa, lakini pia siku mbili kabla ya kipigo cha jana TFF ikitupa rufaa yake ya kupinga kupokwa pointi.

Jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa, Simba ikitumia mfumo wa pasi fupi-fupi, Simba ilitawala sehemu kubwa ya mchezo na ingeweza kufanya matokeo kuwa tofauti kama washambuliaji wake wangekuwa makini na nafasi nyingi walizopata.

Uchu wa mabao kwa Simba ulianza dakika ya kwanza baada ya Uhuru Seleman kuunganisha wavuni kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na mshambuliaji wa kimataifa kutoka Uganda, Emmanuel Okwi.

Kiungo Haruna Moshi alifanya matokeo kuwa 2-0 katika dakika ya 17 baada ya kuwatoka mabeki wa JKT na kupiga shuti lilokwenda moja kwa moja wavuni na matokeo kubaki hivyo mpaka nusu ya kwanza ilipomalizika.

Gervais Kago nusura aipatie Simba bao la tatu katika dakika ya 41 kama mpira wake wa kichwa aliopiga usingekosa shahaba sentimita chache toka lango la JKT.

Baada ya kuona upepo unakwenda vibaya, Maafande wa JKT walikaribia kufunga katika dakika ya 44, lakini Hussein Bunu alishindwa kuusukumizia wavuni mpira uliotokana na krosi ya Emmnuel Pius.

Mwinyi Kazimoto aling'arisha zaidi ushindi wa Simba baada ya kiki yake ya mwendo mrefu mita 25 kwenda moja kwa moja kwenye kamba za JKT likiwa bao la tatu katika dakika ya 64.

Timu zote zilifanya mabadiliko ambapo, JKT ilimuingiza Samwel Kamtu badala ya Emmanuel Pius (64) na Mohamed Banka alikwenda benchi na kuingia George Mketo, wakati Simba iliwatoa Juma Nyoso na Kago na kuingia Obadia Mungusa na Ally Mtinge.

Kocha wa Simba Cirkovic Milovan alisema kikosi chake kilicheza vizuri na hakuna shaka ndicho kilishostahili ushindi kwenye mchezo huo.

"Nina uhakika wa kutwaa ubingwa, matokeo haya yamefungua njia," alisema huku kocha wa JKT, Charles Kilinda akigoma kuongea na waandishi baada ya mchezo.

Katika mchezo mwingine, Coastal Union imeichapa Polisi Dodoma mabao 3-1.
Coastal walienda mapumziko wakiwa wanaongoza bao 1-0 lililofungwa na Ally Shiboli katika dakika ya 30 kwa shuti kali.

Bao la pili la Coastal Union lilifungwa dakika ya 80 na Mbwana Kibacha kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa Polisi, Frank Sindato kuunawa mpira ndani ya 18.

Washindi walipata bao la tatu lililofungwa na Lameck Dayton katika dakika ya 89, huku Polisi wakipata bao la kufutia machozi katika dakika za nyongeza lililofungwa na Bashiru Yahaya.

Kwa matokeo hayo Coastal imefikisha pointi 35 wakati Polisi Dodoma imeendelea kushikilia mkia ikiwa na pointi 17.

Aidha, Ruvu Shooting nao waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Moro United katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. Bao la Ruvu lilifungwa na Kitala Ayoub katika dakika ya 90.