Thursday, April 19, 2012
KIBELAAAAAA SIMBA S.C NI NOMA YAICHABANGA JKT RUVU ,YANGA NYAVU HAZIJATEMA
Wachezaji wa simba wakishangilia goli la Uhuru Suleysh
Mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara Yanga, wamechomoka ramsi kwenye mbio za ubingwa Ligi Kuu Bara na kuicha fursa hiyo kuwaniwa na mahasimu wao wakubwa Simba na Azam FC baada ya jana kupata kipigo wasichotarajia cha bao 1-0 toka Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Mahasimu wao Simba walijiimarisha kileleni mwa msimamo baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Ruvu, matokeo yanayowafikisha pointi 56 ambazo kimsingi haziwezi kufikiwa na Yanga hata kama itashinda mechi zake tatu zilizosalia.
Suleysh akishangilia bao
Wachezaji wa Simba wakishangilia Ushindi dhidi ya JKT Ruvu
Yanga inabaki katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 43, na hata kama itashinda michezo yake mitatu iliyobaki, itafikisha pointi 52 ambazo zimeshapitwa na Simba, huku Azam yenye pointi 50 ikihitaji ushindi kwenye mchezo mmoja tu kuzipita pointi hizo za Yanga.
Lakini hata kama watakata rufaa na kurejeshewa pointi walizopokwa na Kamati ya Usuluhishi na Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), bado Yanga watafikisha pointi 55 ambazo tayari zimeshapitwa na Simba.
Katika mechi hiyo iliyojaa kila aina ya ushindani, shujaa wa Kagera Sugar aliyeipoteza Yanga kwenye ramani ya mbio za ubingwa alikuwa Shija Mkina aliyefunga bao pekee dakika ya 26.
Shija alifunga bao hilo akitumia makosa ya kipa wa Yanga, Yaw Berko aliyeshindwa kulinasa vizuri mikononi mwake shuti la adhabu ndogo lililopigwa na Mike Katende na mpira kumponyoka kabla ya kumkuta mfungaji.
Kocha wa Yanga, Costadin Papic ambaye hakuwapo kwenye benchi wakati Yanga ilipolala 3-2 na Toto African mechi iliyotangulia, alisema ameyakubali matokeo lakini bila kuwa tayari kusema lolote kuhusu kuutema ubingwa.
Kabla ya bao hilo, Mkina alifunga lingine dakika ya 8, lakini mwamuzi Rashid Msangi alilikataa kwa madai mfungaji alikuwa ameotea, uamuzi uliolalamikiwa na kocha wa Kager Mlage Kabange.
Kabange alisema mwamuzi alichezesha mechi hiyo chini ya kiwango na hakuwa makini katika maamuzi mengi yaliyofanya kiasi cha kuifanya mechi hiyo kuwa na makosa mengi yasiyo ya lazima.
Kipigo hicho ni mwendelezo wa mkosi kwa Yanga, kwani imemaliza ziara ya mechi za Ligi Kuu bila bila kupata pointi Kanda ya Ziwa, lakini pia siku mbili kabla ya kipigo cha jana TFF ikitupa rufaa yake ya kupinga kupokwa pointi.
Jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa, Simba ikitumia mfumo wa pasi fupi-fupi, Simba ilitawala sehemu kubwa ya mchezo na ingeweza kufanya matokeo kuwa tofauti kama washambuliaji wake wangekuwa makini na nafasi nyingi walizopata.
Uchu wa mabao kwa Simba ulianza dakika ya kwanza baada ya Uhuru Seleman kuunganisha wavuni kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na mshambuliaji wa kimataifa kutoka Uganda, Emmanuel Okwi.
Kiungo Haruna Moshi alifanya matokeo kuwa 2-0 katika dakika ya 17 baada ya kuwatoka mabeki wa JKT na kupiga shuti lilokwenda moja kwa moja wavuni na matokeo kubaki hivyo mpaka nusu ya kwanza ilipomalizika.
Gervais Kago nusura aipatie Simba bao la tatu katika dakika ya 41 kama mpira wake wa kichwa aliopiga usingekosa shahaba sentimita chache toka lango la JKT.
Baada ya kuona upepo unakwenda vibaya, Maafande wa JKT walikaribia kufunga katika dakika ya 44, lakini Hussein Bunu alishindwa kuusukumizia wavuni mpira uliotokana na krosi ya Emmnuel Pius.
Mwinyi Kazimoto aling'arisha zaidi ushindi wa Simba baada ya kiki yake ya mwendo mrefu mita 25 kwenda moja kwa moja kwenye kamba za JKT likiwa bao la tatu katika dakika ya 64.
Timu zote zilifanya mabadiliko ambapo, JKT ilimuingiza Samwel Kamtu badala ya Emmanuel Pius (64) na Mohamed Banka alikwenda benchi na kuingia George Mketo, wakati Simba iliwatoa Juma Nyoso na Kago na kuingia Obadia Mungusa na Ally Mtinge.
Kocha wa Simba Cirkovic Milovan alisema kikosi chake kilicheza vizuri na hakuna shaka ndicho kilishostahili ushindi kwenye mchezo huo.
"Nina uhakika wa kutwaa ubingwa, matokeo haya yamefungua njia," alisema huku kocha wa JKT, Charles Kilinda akigoma kuongea na waandishi baada ya mchezo.
Katika mchezo mwingine, Coastal Union imeichapa Polisi Dodoma mabao 3-1.
Coastal walienda mapumziko wakiwa wanaongoza bao 1-0 lililofungwa na Ally Shiboli katika dakika ya 30 kwa shuti kali.
Bao la pili la Coastal Union lilifungwa dakika ya 80 na Mbwana Kibacha kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa Polisi, Frank Sindato kuunawa mpira ndani ya 18.
Washindi walipata bao la tatu lililofungwa na Lameck Dayton katika dakika ya 89, huku Polisi wakipata bao la kufutia machozi katika dakika za nyongeza lililofungwa na Bashiru Yahaya.
Kwa matokeo hayo Coastal imefikisha pointi 35 wakati Polisi Dodoma imeendelea kushikilia mkia ikiwa na pointi 17.
Aidha, Ruvu Shooting nao waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Moro United katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. Bao la Ruvu lilifungwa na Kitala Ayoub katika dakika ya 90.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment