Friday, June 8, 2012

EURO 2012 NYASI KUANZA KUCHIMBIKA LEO, POLAND Vs UGIRIKI KUFUNGUA PAZIA


Mwenyeji mwenza, Poland leo inaanza kutupa kete zake katika mchezo mgumu wa ufunguzi wa mashindano ya Euro 2012 ikiikaribisha Ugiriki.

Poland imekutana na Ugiriki mara 15 katika mashindano ya Ulaya na mara zote wamekuwa wakiisumbua Ugiriki baada ya kushinda michezo 10, kutoka sare mara mbili na kupoteza mechi tatu walipokutana.

Poland euro 2012 national team
Kikosi cha POLAND

Greece euro 2012 national team
Kikosi cha UGIRIKI

Kikosi cha kocha Franciszek Smuda cha Poland kinaingia dimbani leo kwenye Uwanja wa Taifa mjini Warsaw bila majeruhi tayari kuwakabili mabingwa wa Ulaya mwaka 2004 Ugiriki.

Katika mchezo wa leo, Smuda anatarajiwa kupanga kikosi ambacho kinaongozwa na mshambuliaji Robert Lewandowski anayecheza soka Ujerumani katika kikosi cha Borussia Dortmund ambao ni mabingwa mara mbili wa ligi hiyo.

Lakini, huyu hatakuwa pekee yake ila atasaidiwa na wakali wenzake wa Borussia Dortmund, Lukasz Piszczek na Jakob Blaszczykowski pamoja nao, Rafal Murawski na Eugen Polanski katika kiungo kukiwezesha kikosi hicho maarufu kama 'White Eagles' kuanza kwa malengo.

Lakini, Ugiriki inaingia dimbani kwa matarajio ya kucheza mfumo wa 4-3-3 dhidi ya Poland.

Mchezaji tegemeo atakuwa Vasilis Torosidis ambaye awali alidhaniwa kuwa angezikosa fainali hizo baada ya kuumia katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Slovenia wiki iliyopita.

Beki huyo wa kulia amepona na kurejea na yupo tayari kwa mashindano hayo ambayo macho na masikio ya wengi yapo kwa Sotiris Ninis, chipukizi wa miaka 21 ambaye amekuwa akifanya vizuri.

Wengine ni Dimitris Salpingidis ambaye ataongoza mashambulizi ya watu watatu mbele.

Poland au White Eagles walifuzu kwa mara ya kwanza mwaka 2008, lakini walishika mkia katika kundi lao wakiwa na pointi moja.

Pia, kikosi cha Smuda kimecheza mechi tano na kutoruhusu bao na kwa dakika 461 hawajafungwa bao tangu lile la Tamas Priskin katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Hungary, Novemba 15, 2011.

Nao Ugiriki ambao hawakuwahi kushinda mechi wakicheza soka Poland walifuzu kushiriki Euro 2012 wakiongoza Kundi F kwa pointi 24 bila kufungwa wakizitangulia Croatia na Israel.

Timu hiyo inao wachezaji watatu pekee kutoka kikosi cha ubingwa cha mwaka 2004 ambao ni, Giorgos Karagounis, Kostas Katsouranis na Kostas Chalkias.

Habari zaidi ya Euro 2012 UK 30.

KITU CHA "BWAX" RUKSA KOMBE LA DUNIA BRAZIL 2014

Rais wa Brazil akiwa na viongozi wa Fifa pamoja na Pele
Rais wa Brazil akiwa na rais wa FIFA Sepp Blatter,Pele na viongozi mbalimbali wa soka

Rais wa Brazil Dilma Rousseff amesaini kuwa sheria muswada utakaoruhusu uuzwaji wa bia wakati wa mechi za Kombe la Dunia mwaka 2014.
Shirikisho la Kandanda Duniani, Fifa, lilikuwa linataka mabadiliko katika sheria ya Brazil inayopiga marufuku pombe kuuzwa kwenye mechi za mpira wa miguu.

Muswada huo mpya, umeweka sheria kadha kwa ajili ya Kombe la Dunia, haujaelezea kuweka pingamizi lolote la kuuzwa pombe.

Waandishi wa habari wanasema magavana wa majimbo bado wanaweza kupiga marufuku uuzwaji wa bia wakati wa mashindano hayo.

Uuzaji bia umekuwa mwiko katika mechi za kandanda nchini Brazil tangu mwaka 2003.

Upigwaji huo marufuku uliwekwa ikiwa ni sehemu ya hatua ya kupambana na vurugu miongoni mwa mashabiki wa timu zenye uhasama pamoja na kukabiliana na wahuni.

Mapema mwaka huu Katibu Mkuu wa Fifa, Jerome Valcke, aliweka bayana kwamba haki ya kuuza bia ni lazima irejeshwe kuwa sheria wakati wa michuano ya Kombe la Dunia kwenye Bunge la Brazil.

Wakati wa ziara ya kukagua viwanja kwenye miji 12 ya Brazil itakayochezewa mechi hizo, alionesha hisia zake kwa jambo hilo.

"Unywaji wa pombe ni sehemu ya patashika za Kombe la Dunia, kwa hiyo tutahakikisha unaruhusiwa. Mtaniwia radhi iwapo nitakuwa nawakwaza kwa kiasi fulani lakini hilo ni jambo ambalo halina mjadala," alisema.

Kampuni ya bia ya Budweiser ndio wadhamini wakubwa wa Fifa.
Vyombo kama hivi kombe la dunia Brazil 2014 ruksaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa!!!!!

KOCHA ASAINI MKATABA AFARIKI SIKU MOJA KABLA YA KUANZA KAZI


Kocha aliyefariki dunia Manuel Preciado

Kocha mpya aliyeteuliwa juzi Manuel Preciado amefariki saa 24 baada ya kutangazwa kama Kocha wa klabu ya Uhispania, Villarreal.

Kocha huyo ambaye hapo zamani alikua kocha wa Sporting Gijon alifariki kutokana na mshtuko wa moyo akiwa na umri wa miaka 54.

Kifo chake kimetokea saa 24 baada ya kukubali mkataba wa kuiongoza klabu ya Villareal iliyoshuka daraja, ambapo mkataba wake ulikua wa kuanza msimu wa mwaka 2012 hadi 2013.





Kocha Preciado enzi za uhai wake viwanjani

Preciado aliefungashiwa virago na Sporting Gijon mnamo mwezi Januari licha ya kuiwezesha klabu hio kupanda daraja mara mbili kuingia Ligi kuu ya Uhispania, La Liga.

Mnamo mwezi Aprili mwaka 2011, klabu yake ya Sporting Gijon iliikwamisha klabu maarufu ya Real Madrid kwa kuvunja rekodi yake ya miaka tisa bila kupoteza kwenye uwanja wa nyumbani safari hii ikiwa chini ya Jose Mourinho.

Wakati akisakata soka Preciado alicheza kama beki na alianza kukipiga katika klabu ya Racing Santander na pia kushiriki mechi za vilabu kama Linares, Mallorca, Alaves, Ourense na Gimnastica.

Baada ya kustaafu kama mchezaji mwaka 1992, akaanza shughuli za ukufunzi akianzia klabu ya Gimnastica na pia kuinoa Racing B, Racing Santander, Levante na Murcia kabla ya kujiunga na Sporting Gijon mwaka 2006.

Baadaye aliiwezesha klabu hio kupanda daraja hadi Ligi kuu ya Uhispania katika msimu wake wa pili na kukaa na klabu hio kwa kipindi cha miaka sita.

Thursday, June 7, 2012

NAMBA YA BAHATI YA KELVIN YONDANI YAFYATUKA SIMBA YANGA WAMGOMBANIA


Kelvin Patrick Yondani akisaini mkataba na Yanga

Sehemu ya mkataba baina ya Yondani na klabu ya Yanga

Pamoja na mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage kufunguka kuwa beki wa timu hiyo Kelvin Yondani ni mchezaji wao halali, klabu ya Yanga nayo imefunguka kivyake kwa kusema, ilimsajili beki huyo kwa Sh30 milioni. Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema walimsajili rasmi Yondani Februari 20 mwaka huu.

Katika msimu uliopita Yondani aliingia katika mgogoro na klabu yake ya Simba kutokana na kutofautina na uongozi wa Simba."Yondani alimwaga wino wa kuichezea Yanga kwa mwaka mmoja na mkataba alisaini rasmi Februari 20 mwaka huu na utafikia kikomo Machi 20 mwaka ujao, ambapo atakuwa akipokea mshahara wa Shilingi 800,000,"alisema Sendeu.

Alisema,"Tumefuata taratibu zote zinazostahili za kumsajili mchezaji kwa mujibu wa kanuni na sheria za Fifa, tulizungumza naye miezi sita kabla ya ligi kumalizika mwezi Mei mwaka huu."

Sendeu alisema hawatakubali kuyumbishwa na vitisho vya uongozi wa Simba kwa kuwa, sheria zote wanazifahamu na wamezifuata na kama wakigundua kuwa kuna udanganyifu wowote umefanyika, basi watachukua hatua kali za kisheria bila kujali hadhi ya mtu.


Ofisa habari wa Dar Young Africans (Yanga) Louis Sendeu

Kauli ya Sendeu imekuja saa chache baada ya Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage kudai kuwa Yondani bado ni mchezaji wao halali na kwamba waliomsajili wanajisumbua na watawachukulia hatua za kisheria.

"Msimu uliopita tuliwapa tahadhari wasimsajili mchezaji wetu mmoja ambaye tulitaka kumsajili, lakini wakaendelea na harakati zao wakatumia nguvu kubwa na kupoteza fedha matokeo yake wakasajili bomu na sasa tunawatahadharisha waache hizo harakati zao wanazozifanya, Yondani bado ana mkataba wa mwaka mzima wa kuichezea Simba tutawashtaki," alisema Rage.


Mwenyekiti wa Simba Sports Club Ismail Aden Rage

Yondani ataingia kwenye orodha ya wachezaji, ambao wamewahi kuzisumbua klabu hizo mbili kwenye usajili wake akiwamo Victor Costa, Athuman Idd Chuji, Kenneth Asamoh ambaye awali alitaka kusajiliwa na Simba, lakini Yanga wakawapiga bao na jana Rage aliwapa dongo kuwa mchezaji huyo ni bomu.

Ndoto za Yondani kukipiga kwenye klabu ya Yanga msimu uliopita zilisababisha vuta ni kuvute ya muda mrefu kabla ya baba yake mzazi kuingilia kati na kumaliza mgogoro huo na kurejea tena kundini kukipiga kwenye timu ya Simba.

Sendeu alisema Yondani ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga watakaoingia kambini Juni 14 kujiandaa na mashindano ya Kombe la Kagame pamoja na Ligi Kuu ya Tanzania Bara.


Yondani kushoto akikabiliana na Tegete katika moja ya mechi za watani wa jadi Simba na Yanga

OKWI ANA THAMANI YA Tshs BILIONI 1


Emmanuel Okwi katika uzi wa Klabu yake ya Simba Sports

KLABU ya Simba imesema iko tayari kumruhusu mshambuliaji wake wa kimataifa toka Uganda, Emmanuel Okwi kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya, lakini hilo litawezekana iwapo klabu itakayomuhitaji itakubali kulipa ada ya uhamisho ya Pauni 500,000 (Sh1.3 Bilioni).

Okwi aliyetoa mchango mkubwa na kuiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa Bara msimu huu, amepata ofa ya kwenda kufanya majaribio katika nchi tatu, Uingereza, Serbia na Austria.

Akiongea jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage alisema kimsingi klabu yake imekubali maombi kutoka nchi hizo ili nyota huyo aende kufanya majaribio.

"Kwa kuzingatia sera ya klabu, tumekubali maombi hayo na tuko tayari kumruhusu Okwi kwenda kufanya majaribio wakati wowote atakapohitajika kufanya hivyo," alisema Rage.

"Kumekuwa na maneno mengi kuhusu Okwi, hapa napenda kutoa ufafanuzi sahihi kwamba, tumepokea maombi ya mawakala kutoka Uingereza, Serbia na Austria akihitajika kwenda kufanya majaribio," aliongeza.

Rage alisisitiza kuwa, klabu yake haina kinyongo na mchezaji huyo kwenda kucheza Ulaya, lakini kwa ada ya uhamisho inayokwenda sambamba na kiwango cha mchezaji huyo, ambacho ni Sh1.3 Bilioni.

Wolfgang Strainwender, wakala raia wa Austria ndiye ameonyesha kumuhitaji haraka Okwi baada ya kumwona kwenye mchezo kati ya Uganda na Angola uliokwisha kwa sare ya bao 1-1, huku bao la Uganda likitumbukizwa wavuni na Okwi, alifafanua Rage.

"Wakala wa Uingereza na Serbia hawajasema wanamuhitaji haraka kiasi gani. Nadhani kufikia kesho jioni tutakuwa kwenye nafasi ya kufahamu ni lini atakwenda Austria," alisema Rage.




Okwi akimwaga udambwidambwi na klabu yake ya Simba Sports

Okwi akiwa katika uzi wa Timu yake ya Taifa Uganda "The Cranes"

Wakati huohuo, Rage alisema kikosi chake kinatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam, Juni 15 kikiwa na wachezaji 25 kuelekea mkoani Shinyanga kwa ajili ya kucheza mechi ya kujipima nguvu dhidi ya Toto Africans.

Alisema baada ya mechi hiyo msafara wa Simba utakwenda Mwanza ambako pia utacheza mechi nyingine ya kujipima nguvu Juni 17.

"Nichukue fursa hii pia kuwaambia wale wanaotaka kujua Simba imemsajili nani na kumwacha nani, kufikia Juni 15 watafahamu kila kitu kwani kikosi chetu kitakuwa na sura mpya," aliongeza Rage

Tuesday, June 5, 2012

FAHAMU KWA UNDANI NCHI, MIJI, VIWANJA MICHUANO YA EURO 2012


POLAND
City
Stadium
Capacity
ChorzówSilesia Stadium50,000
WarsawNational Stadium55,000
PoznańMunicipal Stadium46,000
WrocławStadium in Maślice44,000
GdańskBaltic Arena44,000
KrakówWisła Stadium35,000

Ukraine

City
Stadium
Capacity
KyivNSK Olimpiyskyi73,000
DonetskShakhtar Stadium50,000
KharkivMetalist Stadium42,000
LvivUkraina Stadium32,000
OdesaChornomorets Stadium34,362
DnipropetrovskDnipro Stadium34,000

HAZARD ATUA CHELSEA


Eden Hazard

Klabu ya soka ya England ya Chelsea imetangaza katika tovuti yake kwamba hatimaye imekubaliana na klabu ya Lille ya Ufaransa kwamba mchezaji wa kimataifa ya Ubelgiji, Eden Hazard, atajiunga na klabu hiyo ya Stamford Bridge msimu ujao. Mchezaji huyo, mwenye umri wa miaka 21, tayari afya yake imekaguliwa na klabu ya Chelsea, na imeonekana hana tatizo lolote.

Walipochukua ubingwa wa ligi ya klabu bingwa, nilijiuliza, "Kwa nini sio Chelsea?", alisema Hazard.

"Kulikuwa na mvutano kati ya Chelsea na Manchester united, lakini binafsi naona Chelsea ndio mradi bora zaidi. Ni klabu cha ajabu."


Eden Hazard

Inaarifiwa kwamba Chelsea wameamua kutoa pauni milioni 32 kumpata kijana huyo, na ambaye akizungumza na kituo cha redio cha nchini Ufaransa, RMC, aliongezea: "Chelsea ni timu changa, na nitakuwa na nafasi bora zaidi ya kucheza."
"Ikiwa nitajitahidi kucheza vyema nikiwa Chelsea, huenda nikapata nafasi katika timu."






Hazard awapo uwanjani shughuli yake ni pevu kama inavyoonekana pichani amekusanya Vijiji

Hazard alikuwepo katika kikosi kilichoshinda ligi wakati Lille ilipopata ubingwa mwaka 2010-11 na katika msimu wake wa mwisho, alifanikiwa kufunga magoli 21 katika mechi 48.

Katika mechi yake ya mwisho dhidi ya Nancy mwezi uliopita, alifanikiwa kupata hat-trick (magoli matatu) wakati timu yake ilipocheza dhidi ya Nancy.

Lakini alishindwa kuvuma wakati Ubelgiji iliposhindwa na England katika mechi ya kirafiki Jumamosi iliyopita.

Hiyo ilikuwa ni mara yake ya 28 kuichezea timu yake ya taifa ya Ubelgiji.

Hazard sasa ni mchezaji wa pili kusajiliwa Chelsea tangu dirisha la usajili la mwezi Januari, wa kwanza akiwa ni mchezaji wa kimataifa wa Ujerumani, Marko Marinas.