Monday, October 31, 2011

Mrembo wa leo-Fatma






@unique entertainment

Ndege za KENYA zaua raia 10 na kujeruhi 50 SOMALIA


Raia 10 waripotiwa kuuawa na wengine 50 kujeruhiwa baada ya ndege za kivita za Kenya kuwashambulia wapiganaji wa al-shabaab kusini mwa Somalia.

Msemaji wa Jeshi la Kenya amesema hayo alipohojiwa na BBC kuwa ndege hizo zilishambulia maeneo yaliyo viungani mwa mji wa Jilib.

Amesema waliouawa ni wapiganaji wa kundi hilo lililo na ushirikiano na mtandao wa Al-qaeda.

Lakini shirika la madaktari wasio na mipaka la Medecins Sans Frontieres (MSF) limesema kwa sasa linawatibu watu waliojeruhiwa baada ya kambi ya wakimbizi kushambuliwa na kusababisha vifo vya watu watatu.

Majeshi ya Kenya yaliingia hadi Somalia ili kukabiliana na wapiganaji wa al-shabaab.

Nchi hiyo ya Afrika Mashariki inawalaumu wapiganaji wa al shabaab kwa kuvuka mpaka sehemu za Kaskazini Mashariki na kushambulia vikosi vya Kenya na pia kwa visa kadhaa vya utekaji nyara.

"Tulipokea taarifa za kijasusi kuwa kiongozi mmoja wa al-shabaab alikuwa amepanga kuzuru kambi ya Jilib na ndipo tukafanya mashabulio kutoka angani " msemaji wa jeshi la nchi kavu la Kenya Meja Emmanuel Chirchir ameiambia BBC.

" Taarifa tulizo nazo ni kuwa wapiganaji 10 wa al-shabaab wameuawa na wengine 47 kujeruhiwa", aliongezea kusema.

Amekanusha habari kuwa kambi ya raia ilishambuliwa akisema taarifa kuwa kambi ya wakimbizi ilishambuliwa na raia wa kawaida kuuawa ni propaganda za al-shabaab.

Hata hivyo katika taarifa yake ya Jumapili ,shirika la MSF limesema kuwa wahudumu katika hospitali iliyoko Marere inawahudumia watu kadhaa waliojeruhiwa kufuatia shambulio la angani katika mji wa Jilib.

Shirika hilo limesema kuwa kambi ya wakimbizi wa ndani kwa ndani ilishambuliwa majira ya saa saba na nusu mchana, saa za Afrika mashariki na waliopokelewa ili watibiwe wengi wao ni wanawake na watoto.

Kundi hilo la al-Shabaab limekanusha kuwa linahusika na visa vya utekaji nyara nchini Kenya na linataka Kenya iondowe wanajeshi wake au wakabiliwe vikali.

Arsenal ilivyoigaragaza Chelsea Stamford Bridge

Arsenal yaigaragaza Chelsea 5-3 darajani Van Persie abeba mpira

Mshambuliaji hatari wa Arsenal Robin van Persie amefunga mabao matatu wakati Arsenal ilipoichakaza Chelsea mabao 5-3 katika mchezo wa kusisimua uliochezwa katika uwanja wa Stanford Bridge.
Robin van Persie
Robin Van Persie atia kambani mara 3

Kiungo wa Chelsea Frank Lampard alikuwa wa kwanza kufungua mlango wa Arsenal kwa bao la kichwa lakini Van Persie akasawazisha muda mfupi.

John Terry akaipatia bao la pili Chelsea kwa mkwaju wa karibu kiasi cha yadi 16 kabla beki Andre Santos kusawazisha kipindi cha pili kwa mkwaju uliompita katikati ya miguu mlinda mlango wa Chelsea Petr Cech.

Theo Walcott aliiongezea uhai Arsenal kwa kufunga bao la tatu baada ya kupenya katika msitu wa mabeki wa Chelsea na Juan Mata baadae akaisawazishia Chelsea kwa kufunga bao la tatu kabla ya Van Persie kuongeza bao la nne katika lango lililokuwa wazi baada ya beki na nahodha wa Chelsea John Terry kuteleza.

Van Persie mabao yake mawili ya mwisho aliyafunga katika kipindi cha dakika tano.

Na baadae mshambuliaji huyo wa Arsenal akichezeshwa na Mikel Arteta kwa pasi murua dakika za nyongeza na akafumua mkwaju mkali ambapo mlinda mlango Petr Cech hakuweza kufanya lolote na kushuhudia nyavu zikicheza na kuiandikia bao la tano.

Ushindi huo umeiinua Arsenal hadi nafasi ya sita katika msimamo wa ligi.

Hernandez
Hernandez alifunga bao pekee

Nayo Manchester United ilizinduka baada ya kipigo cha Jumapili iliyopita cha mabao 6-1 kutoka kwa Manchester City baada ya bao moja alilofunga Javier Hernandez kuwapa mshindi mgumu katika uwanja wa Everton.

Hernandez alitengewa mpira wa krosi kutoka kwa Patrice Evra katika dakika ya 19.

Bao hilo lilikuwa ni zawadi nzuri kutokana na kandanda nzuri waliyocheza United, lakini Everton walikuwa wakiisumbua sana Manchester United katika dakika zote zilizosalia.

Leighton Baines wa Everton alikosa bao baada ya mkwaju wake wa adhabu ndogo kugonga mwamba na mkwaju wa Louis Saha nao hakukuweza kulenga lango.

Matokeo hayo yameiimarisha Manchester United katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 23.

MB DOGG AFUNGUA STUDIO











MB DOGG 

Mwanamuziki wa muziki wa bongo fleva aliyetamba vilivyo katika  mwa miaka ya 2000 Mb Dogg alitamba na vibao kama Mapenzi Kitu Gani, Si Uliniambia, Latifa, Naona Raha na nyinginezo. Hivi ni baadhi ya vibao ambavyo viliweza kumweka juu msanii huyu Afrika Mashariki.

Ni wazi kuwa wasanii wote wanaoimba hivi sasa ni chimbuko la Mb Dogg japokuwa hili wengi hawalifahamu, au kutokana na kutojua chimbuko la muziki huu wa kuimba ambao nao ni miongoni mwa muziki wa bongo fleva.

Awali wasanii wengi wa Tanzania walikuwa wakiimba hiphop zaidi na kurap kuliko kuimba muziki ulioonekana hauna soko.

Mb Dogg ambaye hufanya misafara ya kibiashara mara kwa mara huko Pretoria nchini Afrika Kusini ameweka bayana mpango wake alionao hivi sasa katika kuuendelea muziki wa kizazi kipya, ikiwa ni pamoja na kufungua studio ya kisasa.

Yafuatayo ni mahojiano ya mwanamuziki huyo alipofika katika ofisi za gazeti moja la habari hapa nchini la Mwananchi, msanii huyu aliweka bayana maisha yake kwa sasa, muziki, matukio mbalimbali na nini anatarajia kufanya baada ya kukaa kimya kwa miaka mitatu sasa.

Swali: Mbona umekaa muda mrefu pasipo kutoa wimbo wowote?

Jibu: Niliamua kupumzika, tangu nilipotoa kibao cha Natamani na baadaye Sagablasha niliamua kukaa kimya kwa muda nifanye mambo mengine kwanza, maisha sio muziki peke yake, ukiamua kufanya mambo mengine unaendelea pia.

Swali: Mashabiki wamjue vipi Mb Dogg wa sasa?

Jibu: Si kama wa zamani, hivi sasa anaitwa mwalimu wa wasanii, najivunia kwani ni kundi kubwa la wasanii waliopo juu hivi sasa, wamepita katika mgongo wangu ule ule ambao niliuanzisha mimi, namaanisha muziki wa kuimba.

Swali: Inakuwaje kuhusu Tip Top Connection unadhani baada ya kuondoka huko ndio sababu ya wewe kushuka kimuziki?

Jibu: Sijashuka kimuziki, ila niliamua kukaa kimya kwa muda nifanye mambo mengine kwanza, kuondoka Tip Top si sababu kuu ya mimi kushuka kuna sababu nyingine nyingi tu ambazo zinamfanya msanii kukata tamaa.

Swali: Nini sababu nyingine zilizokukatisha tamaa?

Jibu: Msanii unaweza kufanya kazi na wakubwa wako wasiithamini nguvu yako na hivyo unakata tamaa, ni mambo mengi sana yaliyotokea ambayo kiukweli nilishayaongea sana na sipendi kuyarudia kwani, Tip Top Connection hivi sasa ni watu wangu wa karibu ila sitaweza kufanya nao kazi na sitarajii.

Swali: Unadhani sababu ya wewe kutoka katika kundi inaweza kuwa sababu nyingine ya kukosa muda wa hewani katika redio za FM?

Jibu: Swali gumu sana hilo, na halijibiki ingawa nadhani inaweza kuwa sababu ya mimi kukata tamaa japokuwa sina uhakika na hilo kwamba ndio sababu ya kazi zangu kutochezwa.

Swali: Nini unafanya kwa sasa ili kuuendeleza muziki huu wa kizazi kipya?

Jibu: Safari yangu ya mwisho nikitokea Afrika Kusini ilikuwa ni kwenda kuchukua vifaa vya kuikamilisha studio yangu ya kisasa iliyopo maeneo ya Ubungo Makuburi itayoitwa Makopa Record, itakayorekodi audio na video. Imeshakamilika na muda wowote itaanza kazi, nimefanya hivi ikiwa ni mchango wangu wa kuendeleza muziki huu. Hata hivyo ninaendelea na muziki na nimeshafanya kazi kadhaa nikiwa na P Funk Majani pamoja na Man Walter na ninataraji kuziachia hivi karibuni.

Swali: Wiki hii vyombo vya habari vimeripoti kuwa ulipigwa risasi nchini Afrika Kusini je kuna ukweli wowote?

Jibu: Ninashangaa kisa hicho hakinihusu kabisa, yaani mama yangu alipatwa na presha baada ya kusikia habari hizo kwani alikua mbali na mimi kwa wakati huo, nimesikitika kwani ni vema wangenitafuta mimi mwenyewe ili wahakikishe taarifa hizo kuliko kuzianika hadharani pasipo utafiti wowote.

Swali: Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, inasemekana kuwa ulikuwepo eneo la tukio na ni wapi makazi yako kwa sasa kati ya Tanzania na Afrika Kusini?

Jibu: Nilikuwepo eneo la tukio, lakini sijahusika watu hao walikuja kumtafuta mtu wao na kumpiga risasi, ni Mtanzania ambaye amefariki siku chache zilizopita. Ila tukio hilo lilitokea Septemba 28, nikiwa Afrika Kusini. Kwa sasa makazi yangu ni Tanzania lakini hufika mara kwa mara nchini huko kibiashara zaidi.

Swali: Suala la kutangazwa kuwa umemiminiwa risasi nchini humo unadhani limekuathiri kwa namna moja ama nyingine.

Jibu: Limeniathiri tena kwa kiasi kikubwa, kwani hivi sasa wengi wanadhani ninajihusisha na vitendo vya kiharifu ndio maana nimepatwa na maswahibu hayo, kitu ambacho si kweli.

Saturday, October 29, 2011

SIMBA NA YANGA LEO HATUMWI MTOTO GENGENI NI VUTA NIKUVUTE TAIFA













Patashika ya ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, leo kwa mara ya kwanza tangu kuanza msimu inafikia hatua tamu kwa mechi ya mahasimu wa jadi Yanga na Simba kuvaana kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Miamba hiyo, Yanga mabingwa watetezi, na Simba vinara wa msimamo, wanakutaka katika mechi yao kwanza msimu huu, lakini ikiwa ni ya tano kwa mwaka huu pekee.

Zilikutana, mwanzoni mwa mwaka huu Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi, zikakutana tena Ligi Kuu-raundi ya pili, zikashuka tena dimbani fainali ya Kombe la Kagame, na kumaliza kwenye mechi ya Ngao ya Hisani.

Simba imeshinda (2-0) mara mbili, fainali ya Mapinduzi na Ngao ya Jamii lakini Yanga ikashinda fainali ya Kombe la Kagame bao 1-0, na kwenda sare ya 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu.

Dakika 90 za mwamuzi Oden Mbaga atakayesimama kati 'kuzihukumu' timu hizo zitatosha kuhitimisha, majigambo, mbwembwe, sifa na visasi vya kishabiki vilivyopendezesha jiji karibu wiki nzima sasa.

Yanga inashuka dimbani ikiwa bado na upya wa mabadiliko ya kocha waliyofanya siku chake kabla ya pambano la leo, ikiwa ni mara ya pili wanabadilisha kocha ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja.

Pamoja na kuiwezesha Yanga kutwaa ubingwa Ligi Kuu kutoka mikononi mwa Simba, na Kombe la Kagame kwa kuifunga Simba, iliamua kumtema kocha Mganda, Sam Timbe na kumrejesha Kostadin Papic.

Papic atakuwa na jukumu kubwa la kupoza 'mgawanyiko' wa uteuzi wake kama kocha mpya kwa kuifunga Simba na kurejesha matumaini ya kutetea ubingwa.

Kwa upande wao Simba wanajivunia rekodi nzuri tangu kuanza kwa msimu, na mpaka sasa ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mchezo na inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi sita dhidi ya Yanga.

Safu ya Simba itakayoongozwa na Felix Sunzu, Emmanuel Okwi na Haruna Moshi, itakuwa na jukumu zito kuipenya ngome ya Yanga itakayokuwa chini ya Nadir Haroub 'Cannavarro' na Shadrack Nsajigwa.

Nayo ngome ya Simba itakayokuwa chini ya Juma Nyosso, Victor Costa, Said Cholo na Juma Jabu itakuwa na kazi ya kuwazuia Kenneth Asamoah na Hamis Kiiza pamoja na Shamte Ali.

Kocha wa Simba, Moses Basena, alisema jana kwenye kambi ya timu hiyo, Bamba Beach, Kigamboni kuwa kikosi chake kiko kamili kwa mchezo huo, na kueleza wazi kuwa amejiandaa kushinda.

Kwa tathmini yake binafsi anasema Simba ndiyo iliyo bora kwa sasa kulinganisha na wapinzani wao, jambo ambalo kwa upande wa kocha Papic yeye anamini matokeo ni baada ya dakika 90.

Papic atawategemea pia Jerry Tegeta na Davis Mwape katika kulitia misukosuko lango la wapinzani wao.

Mbali na mwamuzi Mbaga ambaye amelalamikiwa na Yanga na Simba kuchezesha mechi hiyo akisaidiwa na Hamis Chang'walu na Mohamed Kanyenye wakati mwamuzi wa mezani ni Soud Abdi wa Arusha huku kamishna wa mechi akiwa Mohamed Nyange.