Nakwazika sana na matukio na shida zinazowakabili wananchi wa Tanzania bila ya viongozi wanaohusika kuwajibika ama kuwajibishwa..mfano hili swala la ajali ya meli kama ingekuwa limetokea nchi zenye viongozi wanaojua nini uongozi na wenye maadili katika utumishi wa umma lazima wahusika wangejiuzulu,
Tumeshaona mifano nchi nyingi viongozi wakijiuzulu pindi mambo yanapokwenda kombo katika idara ama vitengo vyao iwe wamesababisha wao ama wamesababisha watendaji wao likishatokea janga ni kujiuzulu tu hakuna mjadala..kwa masikitiko hali ni tofauti hapa Tanzania, madaraka yanatumiwa vibaya na waliopewa dhamana kwani wanajali zaidi maslahi yao kuliko Taifa lenye watu waliowachagua. Na hii inatokana na udhaifu wa kiongozi mkuu ambaye ni Raisi, yeye ndie mwenye kusimamia Taifa na viongozi wake lazima awe na msimamo katika kuhakikisha watendaji wake wanawajibika kwa mujibu wa kanuni na taratibu za nchi.
Sioni sababu ya Viongozi ambao wizara ama idara zao zina kashfa za mikataba mibovu,matumizi mabaya ya ofisi,maafa kutokana na uzembe wa watendaji wao,hali ya maisha kuwa ngumu kutokana na upandaji na ukosekanaji wa bidhaa muhimu katika taifa,wizi na ufujaji wa mali za umma na wengineo wengi kuendelea kubaki katika nyazifa zao.
Kwa staili hii ya viongozi wazembe kuendelea kuonekana kama miungu watu Daima taifa litaendelea kuwa masikini, kwani kutokana na ajali na vifo vya majanga ya kizembe vinapoteza watu ambao ni nguzo muhimu katika ujenzi wa Taifa, Kutokuwa na uwajibikaji katika idara nyeti zinadumaza huduma muhimu kwa wananchi na kufanya kuwa na maendeleo duni,hivyo kama wananchi hawana la kufanya taifa haliwezi kupata kipato.
Inauma na inakera sana kuona nchi inakosa mwelekeo kwasababu ya watu wachache, Jamani enyi viongozi hivi mliingia katika uongozi ili muwatumikie wananchi kweli?
Nilichogundua ni tofauti ya kuwa kiongozi hapa Tanzania na kuwa kiongozi nchi zingine, tofauti ni hii:
Nchi zilizoendelea mtu anagombea uongozi kwa hulka ya kuwa kiongozi ya kuwatumikia wananchi waliomchagua tofauti na viongozi wetu swala la kuwa kiongozi wameligeuza ajira, hapa ndio matatizo yalipo ndio maana kiongozi ukimwambia ajiuzulu ama awajibike inamuwia vigumu kwasababu hana mbele wala nyuma uongozi ndio kila kitu kwake.
Imefikia wakati sasa viongozi muone uongozi kuwa ni dhamana halisi ya kuwatumikia watu na sio ajira kama mlivyogeuza kwa hivi sasa, mkiwa na jinsi nyingine ya kuishi na mkauchukulia uongozi kuwa ni dhamana ya kuwatumikia wananchi lazima mtakuwa na maadili mema ya utumishi wa umma, pindi unapoonekana umeshindwa kuwajibika basi swala la kuachia ngazi halitokuwa gumu kwako kwani ilikuwa ni sehemu ya maisha yako na sio maisha yako.
Watanzania wenzangu kwa kulifahamu hili na mkagundua viongozi wetu wameufanya uongozi ndio njia yao ya kuishi hamtoshangaa kwanini wanafanyaufisadi na wamekuwa wagumu kuwajibika ama kuchukua maamuzi magumu. Uongozi sio ajira kama tunavyofikiria,mshahara unaopewa kiongozi ni malipo ya muda na busara zako unazozitumia katika kuwajibika kwa wanachi na Taifa kwa ujumla. Na sababu hizi za kuufanya uongozi kama ajira zinapelekea viongozi kutokuwajibika ipasavyo katika nyazifa zao kwakuwa muda mwingi wanapanga mipango ya kujipatia pesa ama kufanya kazi aile tu zenye kuwapatia pesa ama zenye 10% na kazi za mshahara huwa hazifanyiki kwa jinsi inavyotakiwa zifanyike.
Nitaendelea na mada hii........+255 684 887 525.
No comments:
Post a Comment