Thursday, September 15, 2011

SIMBA IKO JUU KAMA "ROCKET" YAWACHEZESHA KWATA POLISI DODOMA


Ulimboka mwakingwe akijaribu kuska mpira bila mafanikio

MSHAMBULIAJI Gervais Kago aliisaidia timu yake ya Simba kuichapa Polisi Dodoma bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu uliofanyika kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi.

Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi 13 na kuendelea kubaki kileleni mwa ligi kuu wakifuatiwa na JKT Ruvu wenye pointi tisa, huku Yanga ikishikilia mkia ikiwa na pointi tatu.

Kocha wa Simba, Moses Basena alisema amefurahishwa na matokeo yaliyompa pointi tatu muhimu.

Mshambuliaji Kago alifunga bao lake la pili msimu huu kwa Simba katika dakika ya 25 akipokea pasi ya kifua kutoka kwa Felix Sunzu na kupiga shuti kali lililojaa wavuni.

Katika mechi hiyo Bryton Mponzi alipoteza nafasi ya kuisawazishia Polisi Dodoma baada ya kushindwa kuunganisha krosi ya Salmin Kiss Kiss huku kiungo wa Simba, Jerry Santo naye alijitahidi kufunga bao katika dakika ya 22 kwa kichwa, lakini beki wa Polisi alizuia mpira huo kwenye mstari wa goli.

Wakati Polisi Dodoma wakijitahidi kutafuta bao la kusawazisha Mponzi alipiga kichwa dhaifu kilichoishia mikononi mwa kipa Juma Kaseja, ambapo Simba walijibu mapigo katika dakika ya 43, baada ya Kago kujaribu kumtungua kipa wa Polisi Dodoma, Agathon Mkwandiko, lakini mpira huo ulitoka nje.


Uhuru Selemani wa Simba akichuana na beki wa Polisi Dodoma

Simba walirudi kipindi cha pili kwa kasi hasa katika dakika za 53, 56, ambapo Kago na Emmanuel Okwi walipoteza nafasi za kufunga wakiwa wao na kipa Mkwandiko kwa mashuti yao kutoka nje.

Mwamuzi Charles Mchau alitoa kadi za njano kwa Bantu admin wa Polisi Dodoma na Nassoro Said wa Simba kwa mchezo mbaya katika mechi hiyo.

Kocha wa Polisi Dodoma, John Kanakamfumu akizungumzia mechi hiyo alisema makosa ya mabeki wake katika kipindi cha kwanza ndiyo yaliyosababisha matokeo hayo.

"Nimegundua mapungufu kidogo, lakini tunakwenda kurekebisha kabla ya mchezo ujao," alisema Kanakamfumu.
Licha ya uwanja wa Azam kuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 5000, mashabiki walishindwa kuujaza uwanja huo na sababu mojawapo ikiwa ni ulanguzi mkubwa uliokuwa ukifanywa na wauza tiketi katika vituo mbalimbali.


Uhuru Selemani akikwepa daruga la mlinzi wa Polisi Dodoma

Hamasa kubwa ya mashabiki wa Simba waliotaka kuiangalia timu yao ikicheza kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi ilitumbukia nyongo kutokana walanguzi wa tiketi hizo.

Pamoja na TFF kutangaza tiketi ya kiwango cha chini kuwa shilingi 7,000 baadhi ya magari yalionekana yakiziuza tiketi hizo kati ya Sh 9,000 hadi 10,000.

Gari lililokuwa linauza tiketi Mbagala mwisho Toyota Hiace namba tunazo walitoa tiketi kwa watu waliokuwa wakiziuza eneo la Big Bon Mbagala kwa bei ya ulanguzi.

Huku gari hilo lilikuwa likizunguka mitaani na kusimama kwenye kituo cha mabasi yaendayo Mbande na Msongola na kuuza tiketi kwa bei kubwa kinyume na eneo walilotakiwa kusimama na kuuza tiketi.

Pia, nje ya eneo la TFF majira ya saa tano asubuhi watu wengi walikuwa wanauza tiketi za Sh 7000 kwa sh 10,000 wakati huo magari yalikuwa hayajaanza kuuza tiketi.


No comments:

Post a Comment